Ndugu zangu waTanzania
wenzangu,
Sisi watanzania wapigania
maendeleo - CHADEMA UK tumelazimika kuwasilisha majonzi yetu kwenu kwa njia
hii, ikiwa ni katika kuonyesha mshikamano wa kitaifa kwa kujifariji na pia
kuwafariji ninyi waTanzania wenzetu kutokana na tukio kubwa la kuhuzunisha sana
ambalo limetokea hivi majuzi nchini mwetu huko mkoani Arusha.
Pamoja na kwamba pamekuwa na
matukio kadhaa yaliyoikabili nchi yetu hili la Arusha tumeonelea tulisemee kwa
njia ya kipekee,kwa sababu licha ya kwamba ni tukio la kigaidi, lisilokuwa na
mantiki yeyote ile zaidi ya umwagaji damu wa raia wasio kuwa na hatia,bali pia
utekelezwaji wake unaweza kutuachia athari kubwa sana kisaikolojia na
kimahusiano kama tusipojaribu kulitathmini na kulitafakari kwa upekee wake.
Wakati ambapo sala na maombi yetu
kwa sasa yawaeendee wafiwa na wale ambao wamedhurika moja kwa moja kimwili ama
kisaikolojia kutokana na tukio hili, tunapenda pia kupongeza juhudi
zilizofanywa na kila mmoja wetu aliyeweza kuwafikia na kutoa msaada wa aina
moja ama nyingine kwa wahanga wa janga hili bila kujali tofauti ya vyama, itikadi,
kabila, dini ama falsafa. Hiyo ndiyo Tanzania tunayoijua sisi. Pamoja na
tofauti zetu nyingi ki hali,afya ama kipato, lakini kamwe hatubaguani katika
misingi ya rangi, kabila ama dini. Na hili ndio haswa linalotusukuma sisi kuwasilisha
huu waraka wa rambirambi kwenu ninyi wenzetu leo hii.
Tuna imani kwamba vyombo
vyetu vya usalama vitafanya utafiti wa kina kuchimbua na kutujuza chanzo cha
ufedhuli huu, ni lazima sisi wenyewe pia tufarijiane kwa maombi, michango na
tafakuri mbalimbali zenye kutiana moyo katika kipindi hiki kigumu kwetu sote.
Tuna imani kwamba yeyote aliyehusika katika mkakati huu atapatikana na kupewa
adhabu inayostahili.
Kwetu sote watanzania, huu ni
wakati muafaka kuonyesha mshikamano wetu kuwatumia ujumbe hao wachache wenye
nia mbaya kwamba waTanzania tumeundwa kutoka jumuiya ya makabila zaidi ya mia
moja, wenye asili, rangi, dini na madhehebu mbalimbali na wasioamini. Na kati
yetu wote sisi ni marafiki na ndugu, wengine ni ndugu wa damu kabisa, kupitia
ndoa, wazazi n.k. Hivyo sisi hatuwezi kubaguana wala kuwa na chuki miongoni
mwetu kwani hiyo si asili yetu. Na yeyote yule atakayejaribu kupandikiza mbegu
hii chafu miongoni mwetu tumkatae na kumchukilia hatua stahiki kumtokomeza yeye
na kundi lake.
Ujumbe wetu kwa watanzania ni
huu:
HII NI VITA DHIDI YA UMOJA
WETU WA KITAIFA NA SIYO KUNDI AU IMANI FULANI.
Asanteni sana, Mungu
awabariki nyote. Mungu alibariki taifa letu Tanzania.
Kwa niaba ya CHADEMA UK
G Mboya
Secretary
2 comments:
TAMKO ZURI.
WATANZANIA TUSHIKAMANE KUWAFICHUA WOTE WANAOTUMBUKIZA AMANI YETU KABURINI ILI WACHUKULIWE HATUA STAHIKI...LIWE NI FUNDISHO NA KWA WENGINE WENYE NIA KAMA HIYO
Mungu atubariki Wa Tanzania tushikamane tulionewa wivu na mataifa mengi ya jirani yaliotumia ukabila na udini yasifike haya,na inawezekana mtu au watu waliohusika haihusiani na tofauti za dini wana tu sababu zao ila wanatumia nafasi hio ili watu wahisi ni mambo ya udini,tuna imani vyombo vya usalama vitashughulikia swala hilo ingawa walishindwa kutupa hatima ya waliomteka Dr ulimboka
Post a Comment