Dodoma. Bunge la Muungano linaendelea na vikao vyake leo mjini Dodoma baada ya mapumziko ya siku moja, huku kukiwa na mabadiliko ya ratiba.
Katika mabadiliko hayo, hotuba ya Wizara ya Elimu imeondolewa kama ilivyotarajiwa na sasa italetwa bungeni Juni 3.
Taarifa zinaeleza kuwa, kusogezwa kwa hotuba hiyo kunatokana na mipango ya Serikali ambayo inatafuta namna na kukamilisha mchakato wa matokeo ya kidato cha nne ili kuipa mteremko hotuba ya Waziri wa Elimu, Shukuru Kawambwa (pichani) bungeni.
Tofauti na mapumziko ya siku mbili za kawaida kwa wabunge, safari hii walipumzika siku moja baada ya Jumamosi kutumiwa kwa ajili ya kuhitimisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini ambayo iliahirishwa Alhamisi iliyopita kutokana na vurugu za Mtwara.
Ratiba ya awali inaonyesha kuwa leo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilikuwa isome hotuba yake ikifuatiwa na Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kabla ya kuhitimisha wiki kwa kusoma Makadirio ya Wizara ya Mambo ya Nje.
Wizara ya Elimu ilikuwa katika ‘mtihani’ kwenye Kikao cha 10 cha Bunge mapema Februari, hasa baada ya Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia kuwasilisha hoja binafsi kuhusu udhaifu uliopo katika sekta ya elimu na zaidi ni kukosekana kwa mitalaa ya elimu.
Hatua hiyo ililazimisha Waziri wa Elimu, Shukuru Kawambwa kupewa muda kuwasilisha mtalaa huo na alifanya hivyo Februari 6, ukihusisha elimu ya chekechea, elimu ya msingi na sekondari kabla ya kupitishwa na Bunge.
Kamati ndogo iliundwa chini ya Magreth Sitta akiwemo Mbatia na wabunge wengine waliobobea katika masuala ya elimu kuangalia uhalali wake.
Hata hivyo, katika kile kinachoelezwa kuwa ni wasiwasi kwa Serikali kuhusu hofu ya vivuli vya wabunge wa upinzani, ratiba ilibadilishwa na kuisogeza mbele hotuba ya Wizara ya Elimu.
Ratiba mpya ya Bunge sasa inaonyesha kuwa, leo Bunge litapokea hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambayo itajadiliwa kwa siku mbili.
Hotuba hiyo pia haitegemei kuwa na mteremko kwani wabunge watakuwa na shauku ya kujadili kuhusu migogoro ya mipaka pamoja na masuala ya upimaji wa ardhi ili kuondoa kero za wakulima na wafugaji yakiwemo mashamba yanayomilikiwa bila kuendelezwa.
Baada ya hotuba hiyo yatafuata Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Wizara ya Kazi na Ajira na kufuatiwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Nchi kabla ya kuhitimishwa kwa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ambazo zote zitakuwa zikisomwa na kujadiliwa kwa siku moja.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment