Monday, May 27, 2013

Kesi ya Richmond kufufuliwa

Dar es Salaam. Wakati kesi ya Richmond ikiwa imepangiwa tarehe ya kuanza kusikilizwa tena Juni 6 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mshtakiwa katika kesi hiyo, Naeem Gire, ameanza mchakato wa kwenda Mahakama ya Rufani.
Gire ambaye alikuwa wakala wa kampuni inayodaiwa kuwa ni kampuni hewa ya kufua umeme wa dharura, Richmond Development LLC, alikuwa akikabiliwa na mashtaka ya kughushi nyaraka, kutoa taarifa za uongo na kuwasilisha nyaraka za kughushi serikalini.
Hata hivyo Julai 28, 2011, aliachiwa huru na Hakimu Mkazi Waliarwande Lema wa Mahakama ya Kisutu, kuwa hana kesi ya kujibu, lakini Mahakama Kuu ikaibua tena kesi hiyo na kumtaka Gire apande kizimbani kujitetea.
Mahakama hiyo ilitoa amri hiyo katika hukumu yake iliyotolewa na Jaji Lawrence Kaduri, katika rufaa ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) aliyekuwa akipinga uamuzi wa Mahakama ya Kisutu kumwachia Gire huru kuwa hana kesi ya kujibu.
Kutokana na hukumu na amri hiyo ya Mahakama Kuu kumtaka Gire arejee kizimbani kujitetea, tayari kesi hiyo ilikuwa imeshapangwa kusikilizwa June 6 kwa Hakimu Emilliu Mchauru.
Habari kutoka Mahakama Kuu zilizothibitishwa na Wakili Rweyongeza, zinasema kwamba tayari wameshawasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa katika Mahakama ya Rufani.
Kwa mshtakiwa huyo kupitia kwa wakili wake wanasubiri kumbukumbu za rufaa kutoka kwa Msajili wa Mahakama Kuu, ili waweze kuandaa na kuwasilisha sababu za rufaa zao ambazo ndizo zitakazosikilizwa na Mahakama ya Rufani.
Kesi ya awali ilifutwa baada ya ushahidi uliotolewa mahakamani na upande wa mashtaka kushindwa kukidhi vigezo vya kumwona ana kesi ya kujibu na kumtaka aanze kutoa utetezi wake.
Hata hivyo, ikiwa ni miaka miwili na zaidi sasa tangu aachiwe huru, Mahakama Kuu imeamuru arejeshwe kizimbani na kujitetetea, baada ya kuridhika kuwa ana kesi ya kujibu.
Kesi hiyo itaendelea kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na mahakama kuuu ambayo itaendelea kupanga ratiba ya kusikilizwa kwake.
Mwananchi

No comments: