ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, June 27, 2013

CCM wang’ang’ania Serikali mbili katika Katiba Mpya

Dodoma. Kikao cha Kamati Kuu ya CCM, kimemalizika mjini Dodoma huku kukiwa na taarifa kuwa chama hicho kimeweka msimamo wa kutaka kuwepo kwa mfumo wa Serikali mbili katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mchakato wa Katiba Mpya ya Tanzania upo katika hatua ya rasimu na watu mbalimbali kupitia Mabaraza ya Katiba, wamekuwa wakitoa maoni yao.
Tayari Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete ametangaza kuwa chama hicho kitakuwa moja ya mabaraza ya katiba na kupata nafasi ya kuichambua, kuijadili na kutoa maoni kuhusu rasimu ilitolewa hivi karibuni na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya mwenyekiti wake Jaji mstaafu Joseph Warioba.
Habari za ndani zilisema kuwa kikao hicho kilichoongozwa na Rais Kikwete kilijadili mchakato wa Katiba Mpya, masuala ya maadili ndani ya chama na kuyatolea uamuzi.
Hata hivyo mmoja wa watendaji ndani ya chama hicho alisema kikao kilikuwa cha kawaida na kwamba kilikuwa kinapitia majukumu na kwamba hakuna kubwa lililojadiliwa. Habari zaidi zinadai kuwa mbali ya kuunga mkono mfumo wa Serikali mbili, CCM imetoa adhabu kwa wanachama wake wawili ambazo zitatangazwa katika siku iliyopangwa.
Mmoja wa watoa habari alilieleza gazeti hili kuwa uamuzi uliotolewa na kamati hiyo, utawasilishwa kwa wanachama wake kwa utaratibu uliopangwa na kwamba wabunge wa CCM wataelezwa katika kikao chao kitakachofanyika keshokutwa Jumamosi katika Ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma.
“Sisi wabunge tunategemea kuelezwa uamuzi wa CC katika kikao chetu cha Jumamosi, tumeambiwa kikao hicho ni muhimu na tuhudhurie bila kukosa,” kilieleza chanzo hicho jana jioni.
Habari zaidi zilisema wakuu wote wa mikoa na wilaya tayari wapo mjini Dodoma na kwamba watakutana na Waziri Mkuu katika mkutano wa kichama uliopangwa kufanyika jana usiku.
Zinapasha kuwa katika mkutano huo uliotarajiwa kufanyika katika Hoteli ya Dodoma, MaRC na MaDc hao wataelezwa mkakati na msimamo wa chama hicho kuhusu mchakato wa Katiba Mpya
Mwananchi

No comments: