ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, June 16, 2013

Jifunze Kiswahili, Uwafunze Wengine



WAHENGA walisema, ‘Kujifunza hakuna mwisho’. Nami nawasihi wasomaji wangu waendelee kuniunga mkono katika jitihada zangu za kuwaelimisha kwani kwa kupitia makala zangu mtajifunza na kuelewa mambo mengi mliyokuwa hamyajui.
Kwa mfano angalia sentensi zifuatazo ambazo zimeandikwa na kuhaririwa na kukubaliwa kuchapishwa katika magazeti lakini zina matatizo. Kwa mfano:
“ Kuna utofauti wa kasi ya maambukizi kati ya wanaume waliofanya tohara na wasiofanya.”
Sentensi hii ina makosa mawili. Kosa la kwanza ni matumizi ya neno ‘utofauti’. Neno ‘utofauti’ limebuniwa na waandishi kutokana na neno ‘tofauti’. Nyongeza ya herufi ‘u’ haifai kuwepo. Inaonekana kuwa herufi ‘u’ imeongezwa bila sababu za msingi.
Pia liko neno jingine ambalo linafanana na hilo nalo ni ‘umauti’ ambalo linashika kasi hivi sasa. Kwa mfano imeandikwa,“Wakati baba yake anapatwa na umauti, Emmily anakwenda jela kwa tuhuma za kuiba fedha za mishahara ya wafanyakazi.”
Ijapokuwa baadhi ya wasomaji watasema huu ni ubunifu lakini ningeshauri tusiiharibu lugha yetu kwa ubunifu wa aina hii. Tuendelee kutumia maneno tuliyozoea kama ‘tofauti na mauti’ ambayo yako wazi.
Kosa jingine ni kutumia maneno ‘waliofanya tohara’. Kwa kawaida tohara hufanywa (kauli ya kutenda) na mtu baki wa kati mhusika hufanyiwa tohara. Hili ni kauli ya kutendewa.
“ Kesi yao inatarajiwa kuendelea leo katika Mahakama katika Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.”
Mpangilio wa maneno ni mbaya. Ilipaswa kuandikwa: “ …”katika Mahakama Kuu Dar es Salaam, Kanda ya Mashariki.”
“ Tangazo hili huleta mihemko kwa watazamaji na siyo kufikisha ujumbe ambao ni kutumia condom wakati wa kujamiiana.”Tatizo liko katika tahajia ya neno ‘condom’. Neno hili limeandikwa kwa mtindo wa Kiingereza badala ya kufuata tahajia ya Kiswahili kama ‘Kondomu’ ambalo limetoholewa na kufuata misingi ya lugha ya Kiswahili. Endapo neno haliwezi kutoholewa linaweza kuandikwa kama lilivyo na kuwekewa alama za semi za“ “
“ Lakini hali ilivyo hivi sasa hatumheshimu mtu kwa historia na mambo aliyowahi kufanya.”
Ni kukosa uzoefu wa misingi ya sarufi ya Kiswahili kwamba neno ‘lakini’ likiwa ni kiunganishi halitakiwi kuanza sentensi. Badala ya kutumia neon lakini tungeweza kuandika ‘Hata hivyo’ na kusomeka,
“ Hata hivyo, hali ilivyo sasa hatumheshimu mtu kwa historia na mambo aliyowahi kufanya.”
“Kitu ambacho kinaweza kusababisha kupandikiza mbegu za chuki kwa Watanzania ambao ni wapiga kura muhimu.”
Iko kanuni isemayo kuwa wazo au dhana moja huwakilishwa kwa neno moja. Kwa mfano tunapoandika ‘vile vile’ au ‘mbalimbali’ tunakuwa nazo au dhana moja kwa hiyo huunganishwa na kuwa ‘vilevile na mbalimbali, n.k. Vivyo hivyo kwa maneno mpiga kura huwakilisha dhana au wazo moja na hivyo tunaandika ‘mpigakura.”
“Wananchi wengi wana sukumwa kutafuta huduma za matibabu kutoka kwa waganga na madaktari wa mitishamba kutokana na ada kubwa zinazotozwa katika hospitali na zahanati za Serikali.”
Tunatumia vibaya maneno ya waganga na madaktari na kupotosha maana iliyokusudiwa. Neno daktari asili yake ni lugha ya Kiingereza. Limetokana na utohozi wa neno la Kiingereza la ‘doctor’. Kwa hiyo daktari ni mganga aliyehitimu elimu ya tiba ya dawa za kisasa. Tunawakuta madaktari katika hospitali na zahanati za Serikali wakati waganga wa mitishamba wako mitaani na wachache sana wana vituo maalumu yva kutibia. Wanaitwa pia matabibu.
Katika matumizi ya kawaida ya waganga tunawaita ‘waganga wa jadi’ au ‘waganga wa kienyeji’ kwa maana ya watu wanaotibu kwa kutumia dawa za mitishamba.
“Masaki (alisema) majeruhi wa ajali hiyo wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya na miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti.”
Ni kawaida tunapoandika sentensi, tunatumia kitenzi kikuu na wakati mwingine kitenzi kisaidizi. Kitenzi kikuu kinajitokeza mara baada ya Nomino au Jina. Sentensi hii haina kitenzi kikuu. Kwa mfano
“Masaki majeruhi wa ajail hiyo…” ilitakiwa kuandikwa,
“Masaki alisema majeruhi wa ajali hiyo…”
0754 861664 0716 694240

No comments: