ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, June 29, 2013

Kikosi Simba kuanikwa leo

Evodius Mtawala
Hatimae kikosi cha 'Wekundu wa Msimbazi', Simba kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara utakaoanza Agosti 24 kitajulikana leo wakati kamati ya utendaji ya klabu hiyo itakapokutana jijini Dar es Salaam chini ya mwenyekiti wake Ismail Aden Rage.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo imeeleza kuwa Rage na wenzake watapokea orodha ya majina ya wachezaji yaliyopendekezwa na benchi la ufundi la timu yao linaloongozwa na kocha Abdallah Kibaden ili kuyapitisha.


Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, alisema kuwa kikao hicho kitahudhuriwa pia na Kibaden ambaye ndiye atakayewasilisha majina ya wachezaji atakaowatumia msimu ujao.

Mtawala alisema kuwa kabla ya kufikia maamuzi ya kupitisha wachezaji, Kibaden atatakiwa kuwasilisha maelezo ya kiufundi ya kila mchezaji aliyemtaja kwenye orodha yake hiyo.

"Ilikuwa tukutane jana (Alhamisi), lakini wajumbe wengi walitoa udhuru na hivyo kuamua kuahirisha kikao hicho muhimu," alisema Mtawala.

Aliongeza kwamba kabla ya kikao cha leo, wajumbe wa kamati hiyo ya utendaji walipata nafasi ya kwenda kwenye mazoezi na kuona uwezo wa wachezaji hao ili watakaokutana wafanye maamuzi ya kuijenga Simba.

"Kikao kitakuwa na agenda moja tu, mengine yanayohitaji ufumbuzi yatafanyiwa kazi siku nyingine," aliongeza.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zimeeleza kuwa katika kikao kilichopita, wajumbe waliamua kufanya maamuzi ya usajili wa kipa Juma Kaseja kwa kupiga kura na inadaiwa ni wawili ndiyo waliompigia kura kipa huyo aliyeitumikia Simba tangu mwaka 2002 akitokea Moro United ya Morogoro.

Wakati huo huo, aliyekuwa kocha mkuu na mchezaji wa timu hiyo, Talib Hilal, ameibuka na kuyoa maoni yake kuhusiana na Kaseja kwa kusema kuwa kipa huyo chaguo la kwanza la Simba hastahili kuachwa katika kikosi cha timu hiyo msimu ujao.

Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu kutoka Muscat, Oman, Talib, ambaye kwa vipindi tofauti hurejea nchini na kuisaidia Simba, alisema kwamba  timu hiyo ilipaswa kujihakikishia kuwa na kipa mbadala kabla ya kufanya maamuzi ya kumtema Kaseja.

Talib alisema kwamba Kaseja bado ana uwezo wa kuisaidia timu na ili awe bora anatakiwa kupata mabeki wenye uzoefu na wanaojua kujipanga.
"Sikubaliani na bado sijaona kipa aliyeandaliwa, unataka kumuacha mtu wakati kiraka wake hujui atatokea upande gani. Kaseja anastahili na ndiyo maana ni Tanzania One," alisema Talib.

Hadi sasa, Simba ina makipa wawili ambao ni Mganda Abel Dhaira na Andrew Ntalla aliyetua Msimbazi hivi karibuni akitokea Kagera Sugar.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments: