ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 26, 2013

KUJITAMBUA; NGUZO MUHIMU KATIKA MAISHA YA UHUSIANO!-3

Naamini umeshajifunza mengi huko nyuma, leo tunakwenda kumalizia mada hii ambayo naamini itakuacha na kitu kipya maishani mwako. Karibuni darasani marafiki zangu.

HAKUNA WATU MAALUM
Kuna baadhi ya watu huwa na fikra kwamba, vitu vizuri vyote ni kwa ajili ya watu fulani maalum, si kweli. Kila mmoja anaweza kufanya jambo fulani kama akiweka misingi mizuri.

Kwa mfano unaweza kumsikia mtu akilalamika: “Watu na bahati zao bwana, mimi siwezi kupata mwanamke mzuri na mwenye mapenzi ya dhati kama huyu jamaa. Watu na bahati zao bwana.”
Mwingine anaweza kusema: “Wa kuolewa nani hapa? Umri umeshakwenda, nishajizeekea zangu, atakayenitaka ni nani? Acha niishi hivihivi, maisha yangu yameshaisha sasa.”

Haya ni mawazo mgando. Ni jambo baya sana kujikatisha tamaa au kuamini kila kilicho kizuri si kwa ajili yako. Nani amekuambia kuwa wewe upo kwa ajili ya vitu vibaya?

UNDA MAMBO KICHWANI
Jaribu kuunda vitu vyako kichwani. Sikia nikuambie...kama unaamini wewe si mtanashati na ni mbaya wa sura, hata upake mafuta ya aina gani huwezi kuonekana mzuri.

Inawezekana ukaonekana mzuri mbele za watu lakini kwa sababu sura yako inasoma maumivu, hasira na kujihisi mnyonge, hakuna atakayekusalimia. Kwa nini akusalimie wakati uso wako hauna matumaini?
Sikia...jiamini, hata tembea yako ioneshe kweli unajiamini. Hakuna mtu anayependa kuwa na mtu mwenye wasiwasi kila wakati. Ukijiamini hata mavazi yako yatakuwa nadhifu.

Kama kuna mtu alikudanganya kwamba eti huvutii au una nuksi, huyo ni adui yako. Moyoni mwako kuanzia leo gonga muhuri wa ushindi. Tengeneza kushinda siku zote na kweli utakuwa mwenye furaha kwenye ulimwengu wa mapenzi.
Acha kulalamika, hata kama umeachwa na wapenzi 12 (labda), usife moyo kwa sababu umri wako umekwenda, tuliza kichwa. Tafakari kwa kina kisha chukua hatua.

JAMBO LA KUZINGATIA
Usikurupukie uhusiano mpya kabla ya kupata muda wa kutafakari matatizo yaliyosababisha uhusiano wa awali kuvunjika. Ni vyema kupata muda wa kujiuliza kwanza, tatizo lilikuwa ni nini?
Nani alikuwa kikwazo? Angalau kuanzia hapo unaweza kujisahihisha na kupata mbinu za kudumu na mpenzi mwingine. Kuachana leo, halafu wiki moja baadaye una mtu mwingine siyo sahihi.
Utaishia kuanzisha uhusiano na kuacha/kuachwa au kuachana kila siku. Kumbe ilikuwa ni jambo dogo tu, kutulia, kutafakari na kujua cha kufanya katika hatua inayofuata ya maisha yako ya uhusiano.

UTAJUAJE KAMA ANAKUPENDA?
Kuna watu wanajiuliza sana kuhusu hili, hivi utamjuaje mwenzi anayekupenda kwa dhati? Rafiki zangu, hakuna kanuni ya moja kwa moja ya utambuzi wa mapenzi ya kweli.
Inawezekana kwa mpenzi huyu ikatumika kanuni moja, kwa mwingine ikatumika nyingine tofauti kabisa. Ndivyo mambo yalivyo. Lakini yapo mambo ya msingi ya kuangalia. 

Mwenye kukupenda atajitoa kwako. Ni msikivu na hapendi kukuudhi. Ukiondoa suala la umakini ambalo ni tabia ya mtu, suala la kujali na kuwa na huruma linapewa kipaumbele na mtu mwenye mapenzi ya kweli.
Tangu awali atakuwa mkweli kwako na hatapenda mapenzi ya vichochoroni. Atakuwa radhi uhusiano wenu ujulikane na yeyote kwa sababu anajiamini kwamba anakupenda.
Mawasiliano ni kiunganishi muhimu, hata kama yupo bize kiasi gani, mawasiliano atayadumisha kwa sababu huongeza chachu katika mapenzi na kusogezana karibu. Hizo ni baadhi ya sifa ambazo mwenye mapenzi ya kweli huwa nazo.

BADO NDOA NI BAHATI?
Eti, mpaka sasa bado unaendelea kuamini ndoa ni bahati? Kama unawaza hivyo, ondoka kwenye giza haraka. Weka mikakati. Usiingie kwenye ndoa kwa kuiga.
Mchunguze vya kutosha tena kwa umakini mkubwa. Ni kweli huwezi kumchunguza mpenzio kabla ya ndoa lakini kuna mengi ya msingi ambayo unatakiwa kuyafahamu.
Mambo kama mila, dini, elimu, tabia binafsi na mambo ya ukoo wao lazima uyajue kabla ya kuingia kwenye ndoa. Msingi wa yote haya ni upendo wa dhati. Penye upendo hakuna kinachoharibika!

No comments: