ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 26, 2013

Simba yamtorosha Mcongo Uganda

Khatimu Naheka na Wilbert Molandi
SIMBA imeendelea na msako wa kusaka nyota wa kimataifa baada ya sasa kumshusha nchini straika Felix Kuipou raia wa DR Congo ambaye ameugomea mkataba.
Nyota huyo ambaye ana asili ya Uganda juzi jioni alitua katika mazoezi ya Simba na kujifua chini ya kocha Abdallah Kibadeni lakini akasema wasiwe na haraka ya kumpa mkataba mpaka atakapoonyesha vitu vyake uwanjani.

Straika huyo alitua asubuhi akitokea nchini Uganda alipokuwa akijaribiwa na klabu ya Kampala City Council (KCC) kabla ya kutoroshwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa Wekundu hao, Moses Basena
“Huyu alikuwa Uganda, lakini Basena ilibidi atumie mbinu kali na kumtorosha ili aje Simba kwa kuwa aliona kiwango chake ni cha hali ya juu, kama kocha atamkubali basi tutamsajili,” kilisema chanzo cha ndani ya Simba.
Akizungumza na Championi Jumatano muda mfupi baada ya kumalizika kwa mazoezi hayo, Kuipou alisema awali alikuwa ajiunge na KCC lakini akajikuta anabadili muelekeo na kuamua kuja Simba.
Kuipou alisema kabla ya kuja Afrika Mashariki alikuwa akiitumikia klabu ya Unisports inayoshiriki Ligi Kuu nchini Cameroon ambapo alifanikiwa kufunga mabao19 msimu mzima.
“Naweza kusema ni kama ajabu mpaka nafika Tanzania, nimeiona Simba ni timu nzuri nafurahi kuona mashabiki wamenipokea vizuri lakini sitaki mkataba kwa haraka, nataka kwanza Simba wanipe siku tatu niweze kuonyesha uwezo wangu na baada ya hapo tutazungumza,” alisema Kuipou.
Mapema Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang’are, maarufu kama Mzee Kinesi aliliambia Championi Jumatano kuwa straika huyo wamemkabidhi kwa Kibadeni ambaye atafuatilia uwezo wake na kutoa jibu kwa viongozi kuendelea na mazungumzo ya kumpa mkataba.
GPL

No comments: