Mkurugenzi wa Kamati ya Miss Tanzania, Hashim Lundenga, akizungumza na warembo wanaotarajia kushiriki shindano la Redd's Miss Tanzania, 2013 wakati alipowatembelea kwenye kambi yao ya mazoezi yanayoendelea katika Ukumbi wa Meeda Pub. Shindano hilo linatarajia kufanyika Juni 7 mwaka huu katika ukumbi huo huo.
Lundenga, akizungumza na Warembo hao leo kwenye ukumbi wa Meeda Pub.
NA MWANDISHI WETU
MKURUGENZI wa Kampuni ya Lino International Agency, waandaaji wa mashindano ya Miss Tanzania, Hashim Lundenga, leo Jumanne jioni alitembelea kambi ya washiriki wanaojiandaa kushiriki katika shindano la Miss Sinza na kusisitiza hakuna rushwa ya ngono katika mashindano yao.
Lundenga aliongozana na ujumbe wake, ambao ni Bosko Majaliwa, Katibu wa Kamati ya Miss Tanzania, Albert Makoye Mkuu wa Itifaki na Nidhamu wa kamati hiyo, Hidan Rico, Afisa wa Habari wa kamati hiyo, Yasson Mashaka, Mkuu wa Mipango wa Kamati hiyo na Lucas Luta, ambaye ni mjumbe.
Lundenga, alifika Meeda Pub, ambapo washiriki wa Miss Sinza wanafanya mazoezi, alifanya nao mazungumzo na washiriki hao kupata fursa ya kuuliza maswali yao yaliyokuwa yakiwakwaza kuhusu tasnia ya urembo.
Akizungumza na warembo hao, Lundenga aliwaonya washiriki hao kutojirahisi kutoa rushwa ya ngono ili kujihakikishia nafasi katika mashindano hayo.
''Msijirahisi kutoa rushwa ya ngono ili kupata nafasi, hata mimi nitakutafuna bure tu au mwandaaji yeyote atakudanganya tu na kukuacha kama ulivyo kwani mashindano haya yanafuata taratibu zake na kanuni za mashindsano yasiyoweza kutoa fursa kwa waandaaji kutoa upendeleo kwa yeyote'' alisema Lundenga
Ujumbe huo uliofika kuwatembelea katika shindano hilo, uliwataka kuwa makini kuepuka utapeli wa watu wanaowaomba ngono ili wapewe ushindi.
"Huwezi kupata ushindi kwa kutoa rushwa ya ngono, majaji wako wengi, je utawapa ngono wangapi ili uweze kufanikiwa kuwa mshindi. Hilo liko wazi kwamba huwezi kufanikiwa kwa kutoa ngono," alisema Lundenga.
Naye Mratibu wa mashindano hayo, Majuto Omary alisema kuwa katika shindano hilo litakalofanyika Juni 7, litasindikizwa na bendi ya Twanga Pepeta, itakayotumia fursa ya kutambulisha baadhi ya nyimbo zake mpya zilizomo katika albamu ya 12 ijulikanayo kwa jina la Nyumbani ni Nyumbani ambayo itazinduliwa rasmi Juni 30 kwenye viwanja vya Leaders Club jijini.
Aidha Majuto, alisema kuwa Twanga Pepeta itakuwa ikitumbuiza kwa mara ya kwanza tokea mwaka jana mwezi julai ambapo ilitumbuiza katika mashindano hayo hayo ya kumsaka mrembo wa Sinza. Alisema kuwa hii ni faraja kubwa kwa mashabiki wa muziki wa dansi na wa masuala ya urembo kwani Twanga Pepeta itakuwa ikimvua taji Redds Miss Tanzania, Brigitte Alfred ambaye atakuwa anavua taji lake la kwanza.
“Ikumbukwe kuwa twanga pepeta haijatumbuiza Sinza kwa kipindi kirefu na hivyo kuandaa zawadi maalum kwa mashabiki wake katika mashindano hayo yaliyodhaminiwa na Redds Original, Mtandao wa Sufianimafoto.com, Dodoma Wine, Chilly Willy Energy Drink, Fredito Entertainment, CXC Africa, Clouds Media Group na Salut5.com” alisema Majuto.
Alisema kuwa jumla ya warembo 12 wamejitokeza kuwania taji la mwaka huu la Sinza nan i matarajio ya waandaaji kuwa Miss Sinza wa mwaka huu atatwaa taji hilo na kufuata nyayo za Brigitte ambaye aliweza kutwaa taji la Miss Kinondoni na baadaye Miss Tanzania.
“Tuna warembo bora ambayo wamedhamilia kufanya kweli katika mashindano ya urembo mwaka huu, wamepania kulinda hadhi ya mwaka jana, hivyo mashabiki waje kuona warembo bora waliopania kufanya kweli katika mashindano hayo,” alisema.
No comments:
Post a Comment