ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, June 29, 2013

MARAFIKI, ULIMI WAKO, KABURI LA MAPENZI YAKO-11

LEO ikiwa ni sehemu ya mwisho ya makala haya, narudia swali ambalo niliuliza mwanzoni wakati nilipoanza uchambuzi wa mada hii.

Je, marafiki na mpenzi wako nani bora? Kabla hujajibu fumba kwanza macho kisha tafakari.
Je, umeshapata jibu? Usijibu kwanza, hebu vuta picha kwa mara ya pili, fanya tafakuri ya kina kisha lipime jawabu lako. Kile ambacho umekipata ndiyo muongozo wa kila siku katika maisha yako. Hakikisha mwongozo huo ni wa kukupa faraja katika maisha yako yote.
Ipo mifano ya watu wanaoteseka leo kwa sababu ya kupotoshwa na marafiki. Walikuwa na wapenzi wazuri, waliokuwa wakisikilizana lakini wakaachana baada ya kushauriwa ndivyo sivyo.
Kama marafiki wenyewe wanachukuliana wapenzi, ni kwa nini isikupe sababu ya kuamini kwamba wewe upo sahihi zaidi kwenye uamuzi wako kuliko mshauri? Pengine atakujaza maneno ya chuki kwa mwenzi wako, mwisho ukamwona hafai, baada ya majuma mawili unagundua yupo naye.
Hii ndiyo sababu wiki iliyopita nikatoa somo ambalo mara nyingi halipatikani kwa sura ya kawaida.
Uliona mfano wa Romeo, Jannine na Shantale. Romeo aliwekeza nguvu nyingi kwa Jannine akijua zawadi, unyenyekevu na uhusika wake wa kiungwana, vinaweza kumfanya mwanamke huyo abadilike na kuonesha mapenzi. Haikuwa hivyo, aliteseka mpaka akaamua kunawa jumla.
Ona sasa, wakati Romeo anateseka kwenye mapenzi ya Jannine, Shantale naye alikuwa mtu wa kulia, akiwaza jinsi anavyoweza kumfanya Romeo amwelewe ili mapenzi yao yawe na sura inayoeleweka. Kuna kipindi alijitahidi kuwa na mwanaume mwingine lakini ilishindikana. Moyo wake ulimpenda sana Romeo.
Kitu ambacho Romeo hakuwa akikijua ni kuwa, Jannine alishindwa kutulia kwake licha ya kupata mapenzi yenye thamani kubwa kwa sababu moyo wake ulikuwa kwa mwanaume mwingine. Yule mwanaume hakuhusika ipasavyo kwenye mapenzi na Jannine ndiyo maana mrembo huyo akaona awe na Romeo.
Kutokana na ukweli kwamba aliamua kuwa na Romeo si kwa mapenzi ya dhati, bali kwa kutapatapa baada ya kuteswa na mwenzi wake ambaye alikuwa haeleweki, alishindwa kuonesha mapenzi ya dhati. Asingeweza kwa sababu moyo wake unapenda kwingine, huku alikuwa anapitisha muda tu.

TUELIMIKE
Tunapaswa kutulia kwenye uhusiano na wapenzi wetu ili kuwafanya nao watulie. Tabia ya kutotulia inawafanya nao warukeruke huku na kule kutafuta furaha yao. Huko wanaporuka nako hawatafurahia kwa sababu wanapotua wanakuwa hawana mapenzi ya moyoni.
Juu ya yote hayo ni kwamba tumia ulimi wako vizuri kila siku. Zungumza maneno mazuri kwa mwenzi wako na si kumtamkia maneno yasiyofaa ambayo mwisho wake husababisha migogoro na kuifanya amani kwenye uhusiano wenu kuwa msamiati.
Hakikisha maneno ambayo ukiambiwa wewe na mwenzi wako yatakuudhi, basi usiyatamke kwake maana matokeo yake ni ugomvi.
Rafiki hawezi kukuchagulia mwenzi wako, kwa hiyo ushauri wake uchuje. Epuka kumpa kipaumbele rafiki na kumweka kando mwenzi wako maana hilo limesababisha kuvunjika kwa uhusiano wa watu wengi.
Mapenzi ni matamu kama utaishi kwa maelewano na mwenzi wako. Kanuni ipo hivi, mapenzi ya kweli hukaribisha maelewano, wanaoelewana huwasiliana kwa ukaribu, wanaowasiliana hushirikishana kwa kila jambo, wanaoshirikishana hushibana, hivyo kuufanya uhusiano wao uwe na afya.
MWISHO.

GPL

No comments: