ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, June 2, 2013

Mauaji ya kutisha yaibuka msituni

Matukio ya mauaji ndani ya msitu wa Mwakijembe yameendelea kutishia usalama wa Watanzania, wanaoishi jirani na eneo la Horohoro linalopakana na nchi jirani ya Kenya.
Kwa kipindi kirefu msitu huo umekuwa eneo la kufanyia mauaji kwa watu wasio na hatia, ambapo genge la wahalifu kutoka Kenya limedaiwa kuhusika na mauaji hayo.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini msitu huo wenye rasilimali nyingi unaodaiwa kutumiwa na genge hilo kwa vitendo haramu vya ujangili, uchimbaji madini na uvunaji wa miti, ikiwemo uchomaji mkaa.
Taarifa za uchunguzi ambazo zilithibitishwa na viongozi wa Serikali ya Vijiji vinavyopakana na msitu huo, zilibaini genge hilo limekuwa likiua kila linayemhisi atafichua uhalifu wao.
Inatoka UK 1
Uchapisha wa Hati za Kusafiria (Kwa mujibu wa taarifa za karibuni, kwa mwaka huu pekee, watu wawili tayari wameshauawa kwa kuchinjwa ndani ya msitu huo.
Matukio hayo ya mauaji yalithibitishwa na Diwani wa Kata ya Mwakijembe, Ramadhani Mtiota ambaye alisema kwa sasa katika eneo hilo hali imekuwa ya hofu kutokana na kuongezeka kwa makundi ya vijana wa rika la Morani wa Kimasai, wanaojiandaa kuvishambulia vijiji vya Kenya.
Diwani huyo alisema ametoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Mboni Mgaza kuhusu hali hiyo pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Andrew Ngoda.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe alisema wanafahamu kuhusu mauaji yanayotokea kwenye msitu huo.
Alisema taarifa za mauaji ya hivi karibuni ya watu wawili, Ali Mohamed na msichana wa kabila la Kimasai Kendie Minja yanafahamika na yanafanyiwa uchunguzi na polisi.
”Ninachofahamu ni mauaji yaliyofanyika ya msichana Kendie kuchinjwa na kufichwa msituni upande wa Kenya, lakini upelelezi unafanywa na Jeshi la Polisi la wenzetu wa Kenya kwa hivyo sijui zaidi ya hivyo,” alisema Massawe.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Mboni Mgaza alisema anaandaa mkutano wa ujirani mwema utakaowahusisha viongozi wa Serikali Mkoa wa Tanga na Jimbo la Mombasa, Kenya.
Alisema mkutano huo utazungumzia hatima ya mauaji hayo, na pia kukomesha matukio ya kuuawa kwa wananchi ndani ya msitu wa Mwakijembe.
Uchunguzi unaonyesha kuwa wanaouawa ni wale wanaojaribu kufichua maovu yanayotendeka ndani ya msitu ikiwamo uvunaji wa miti, uchimbaji holela wa madini na wawindaji haramu wa wanyama.
Watu wanaoishi katika vijiji vinavyouzunguka Msitu wa Mwakijembe, kwa masharti ya kutotajwa majina yao walifichua kuwa ndani ya msitu huo yapo mambo ya hatari yanayotendeka bila kujulikana.
Kwa mujibu wa mashuhuda hao, uhalifu huo unapokuja kujulikana muda unakuwa umepita, na hata ufuatiliaji unakuwa mgumu.
Mmoja wa wanakijiji katika eneo hilo alisema kusikia kwamba mwenzao ameuawa msituni ni jambo la kawaida, kwani takriban kila wakati mauaji yanatokea.
Uchunguzi umebaini kuwa wapo viongozi wa maeneo hayo ambao wameuawa, pale walipojaribu kuanzisha mapambano na wahalifu wanaofanya mauaji msituni.
“Kuna kipindi wanamgambo wa eneo letu la Tanzania waliokuwa wakifanya doria msituni, walikuwa wakilawitiwa na wavamizi wa msitu na wengine kuuawa,” alisema John Juma (siyo jina lake halisi).
Gazeti hili katika uchunguzi wake lilishuhudia kundi la wafugaji wa kabila la Wamasai wa upande wa Tanzania, ambao wanaendelea kujikusanya kwa lengo la kuanzisha mapigano dhidi ya watu wa kabila wa Waduruma wa upande wa Kenya.
Wafugaji hao walisema wanajiandaa kwa mapigano kupambana na watu wa kabila wa Waduruma, kwa kuwa wamechoshwa na tabia yao ya kuwanyanyasa na kuwaonea wakazi wa Tanzania wanaofika katika Msitu wa Mwakijembe.
Kujikusanya kwa wafugaji hao kunatokana na tukio lililotendeka Mei 7, mwaka huu ambapo msichana wa kabila la Kimasai Kendie Minja alikutwa ameuawa msituni.
Taarifa zilidai kuwa mauaji ya Kendie yalifanywa na vijana wanaofanya shughuli ya kuchoma mkaa ndani ya msitu huo, wakitokea upande wa Kenya wa kabila la Waduruma.
Kabla ya kuuawa msichana huyo aliyekuwa akichungia ng’ombe sehemu ya Tanzania karibu na mpakani, alibakwa, akachinjwa na kuburutwa hadi umbali wa mita 500 ndani ya Kenya na kutelekezwa msituni.
Msichana huyo hakuonekana hadi ulipofanyika msako msituni na kufanikiwa kuukuta mwili wake, ukiwa umeanza kuharibika.
Ilielezwa kuwa mauaji hayo yameleta hofu kwenye eneo hilo, kwa kuwa jamii ya wafugaji wa kabila la Wamasai wamedai kushindwa kuwa wavumilivu.
Kuhusu mauaji ya Ali Mohamed yaliyotokea Aprili 26, mwaka huu, ilielezwa kijana huyo mkazi wa kata ya Mwakijembe alikutwa ameuawa msituni na vijana wanaodaiwa kutoka Kenya.
Wakazi wa eneo hilo walisema Ali aliuawa wakati akioga kwenye Mto Umba, ulio ndani ya eneo la Tanzania ambapo alicharangwa mapanga na vijana ambao baadaye walikimbilia kwenye vijiji vya Kenya walikojificha.
Mwananchi

No comments: