NAAMINI umzima bukheri wa afya na unaendelea vyema na majukumu yako ya kila siku kama kawaida. Mimi namshukuru Mungu kwa kila jambo na zaidi nimshukuru kwa kunipa nguvu na uwezo wa kuandika hiki ambacho naamini kina mchango mkubwa katika maisha yako ya kimapenzi.
Mpenzi msomaji wangu, utakumbuka wiki iliyopita nilianza kuzungumzia suala la mawasiliano imara kwa wapenzi huku nikijaribu kuonesha ni kwa jinsi gani penzi la kitapeli linaweza kubainika kwa kuwepo kwa mawasiliano finyu baina ya watu wawili waliotangaziana kupendana.
Niliwahi kusema huko nyuma na naomba nirudie tena kwamba, kama unaona mpenzi wako hayupo makini kwenye suala la mawasiliano, penzi lake litakuwa na walakini.
Hebu wewe mwenyewe fikiria, mpenzi wako anakuomba vocha, unamtumia! Lakini mpenzi wako huyohuyo anakuwa si mtu wa kukupigia wala kukutumia sms. Anasubiri wewe ndiyo umuanze.
Hata unapomtumia meseji nzuri, anapokujibu yake inakuwa kama amejilazimisha vile. Ukimpigia anaonekana yuko bize sana na anataka ufupishe maelezo.
Wakati mwingine unapiga simu haipokelewi au imezimwa bila sababu za msingi na baadaye ukimpigia na kumpata anaonesha kama vile hakuna kilichotokea. Yaani anaona ni poa tu yeye kuzima simu bila kukuambia.
Mbaya zaidi ukihoji na kuonesha kutofurahishwa na tabia hiyo, naye eti anakasirika na anaweza kutokukutafuta akisubiri wewe tena ndiyo umbembeleze.
Mimi nasema hii siyo sawa kabisa na ukiona mazingira haya kwa mpenzi wako, ujue tu huko na mtu sahihi.
Hata hivyo, hutakiwi kupaniki pale unapoona mazingira kama haya na ukachukua uamuzi wa kumuacha.
Kuna watu wengine wanahitaji kuelimishwa katika hili kutokana na uelewa wao mdogo wa mambo walionao.
Kama unaona mpenzi wako ni miongoni mwa wale ambao hawajali linapokuja suala la mawasiliano, tumia muda wako mwingi kumuelewesha na kumpa tahadhari ya kwamba kama hatabadilika hautakuwa na cha kufanya zaidi ya kumuacha.
Baada ya kuzungumza naye tena kwa lugha ya upendo kisha ukaona hakuna mabadiliko, basi ujue huyo ni shamba ambalo hata ukipanda mbegu zako za upendo haziwezi kuota. Muache aende zake huku ukiweka akilini mwako kuwa utampata mwingine ambaye huenda atakuwa na mapenzi ya dhati zaidi kuliko huyo.
Mbali na hilo la mawasiliano, pia ukiona mpenzi wako anakuwa mgumu kukutana na wewe jua penzi linaelekea ukingoni. Unaweza kuona ghafla anakuwa mtu wa mambo mengi, kumpata kwake siyo rahisi.
Anajifanya mtu wa kazi nyingi ambazo mwanzoni wakati mnaanza uhusiano hakuwa nazo! Kipindi hiki anakuwa na visingizio vingi visivyokuwa na maana lakini lililokuwa akilini mwake ni kukwepa kuonana na wewe.
Tamaa ya mwili wake imeshaisha kwa maana hiyo haoni kama kuna umuhimu wa kukutana na wewe tena. Ukimwomba mkutane naye, hutoa sababu nyingi ili mshindwe kuonana.
Hata hivyo, ikiwa utakwenda kwake bila kumtaarifu kabla ‘surprise’ inawezekana ukamkuta na mwanamke mwingine au akawa hana kazi kama alivyokudanganya awali.
Mbaya zaidi ni kwamba huweza kukubadilikia na wakati mwingine kukupiga kwa kosa la kwenda kwake bila taarifa. Je, mpenzi wa aina hii anakupenda kweli?
Jibu rahisi ni kwamba hakupendi, sasa ya nini kumng’angania?
Global Publishers
No comments:
Post a Comment