ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 10, 2013

Mfanyabiashara adai fedha zake Sh. milioni 399.8 kuchotwa benki

Benki ya Barclays tawi la Morogoro imekumbwa na kashfa baada ya wafanyazi wake kwa nyakati tofauti kuchota kwenye akaunti fedha za mteja wake Sh. milioni 399.8.
Wizi huo unadaiwa kufanywa kati ya Septemba 2012 hadi April mwaka huu kwenye akaunti namba 0096000138 ya mteja huyo ambaye ni wafanyabiashara maarufu wa mjini Morogoro.

Mfanyabishara huyo, Ajay Gokal, alisema alibaini wizi huo mwishoni mwa mwaka jana baada ya kuona fedha katika akaunti yake zikipungua siku hadi siku na kuamua kuomba taarifa ya fedha kwenye akaunti yake Novemba mwaka jana na kubaini kuwapo kwa upungufu wa Sh. milioni 119 na kuamua kuomba taarifa ya mwaka mzima.Gokal ambaye ni mfanyabiashara wa moja ya kampuni ya simu ya mikononi, alisema baada ya kuomba taarifa ya mwaka alikuwa akizungushwa na uongozi wa benki hiyo hali iliyomlazimu kwenda kufungua jarada katika kituo cha polisi.
Alisema alilazimika kufanya hivyo kutokana na risiti za wateja wake walizoingiza fedha katika akaunti yake kuonyesha kuna fedha ziliingizwa, lakini kwenye akaunti hazionekani.

“Nina risti za benki hiyo kutoka kwa wateja wangu niliowapa mzigo na kuniingizia fedha hizo, lakini nikienda kuangalia katika akaunti hiyo sioni hizo fedha nikawafata wanipe taarifa za fedha wananizungusha mpaka nikaenda kufungua jarada katika kituo cha polisi,” alisema Gokal.

Alisema baada ya kufungua kesi maafisa wa Jeshi la Polisi waliamuru uongozi wa benki kumpatia taarifa hizo kwa kuwa ni haki yake, lakini cha kushangaza ilikuwa ikimpatia miezi miwili huku mingine ikirukwa.

Alisema baada ya kupitia kumbukumbu hizo toka Novemba mwaka jana hadi Aprili 13 mwaka huu, alibaini kuibiwa Sh. milioni 399.8.

Hata hivyo, alisema alipojaribu kuwasilina na uongozi wa benki, ulidai kuwa suala hilo wanalishughulikia na kumshauri asilifikishe suala hilo katika vyombo vya habari kwani haliwezi kupatiwa ufumbuzi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, alithibitisha kupata taarifa hizo. Alisema polisi ilianza kufanya uchunguzi baada ya uongozi wa benki hiyo kudai kuwa risiti zilizotumika kuweka fedha katika akaunti ya mteja huyo hawazitambui.

Kutokana na hali hiyo, jeshi hilo limewahoji wafanyakazi wa benki hiyo na kuwashirikilia watatu kwa tuhuma hizo huku uchunguzi zaidi ukiendelea na kwamba baada ya kukamilika jarada litapelekwa kwa Mwanasheria wa Serikali ili kufunguliwa kwa mashtaka.

Meneja wa benki hiyo tawi la Morogoro, Angelo Mahembe, alipotafutwa na nipaswe kupata ufafanuzi hakukubali wala kukataa. Hata hivyo, alishauri watafutwe viongozi wa makao makuu kwa maelezo kuwa yeye siyo msemaji.

No comments: