Arusha. Mwanasiasa mkongwe, Edwin Mtei ameelezea kuridhishwa na rasimu ya Katiba Mpya, huku akikosoa kuruhusu mgombea binafsi nafasi ya Urais na kukataliwa kwa serikali za majimbo.
Akizungumza na Mwananchi jana, Mzee Mtei ambaye alikuwa Waziri wa Fedha Serikali ya Awamu ya Kwanza, alisema rasimu hiyo ni nzuri ila ana maoni tofauti kuhusu kuruhusiwa mgombea binafsi kwa nafasi ya Rais na kukataliwa pendekezo la serikali za majimbo.
“Urais ni nafasi ya juu kabisa katika nchi, lazima Rais ajulikane anatoka chama gani, ana sera gani na kundi gani linamuunga mkono ambako atateua mawaziri wake,” alisema Mzee Mtei.
Mzee Mtei alisema lazima rais awe anawajibika kwa wananchi kupitia chama chake ambacho kitaunda serikali, lazima sera zake zijulikane na kwamba, nafasi hiyo ikiachwa huru atapatikana rais wa ajabu. “Pia, rasimu imefanya vizuri kupunguza Mamlaka ya Rais, ikiwamo uteuzi wa viongozi mbalimbali kama tume ya uchaguzi, hili ni moja ya mambo tangu enzi za utawala wa kwamza nilikuwa nashauri,” alisema Mtei.
Kuhusu serikali ya majimbo, alisema ni vyema kuanza kufikiriwa kwani zitapunguza migogoro kama ulivyo sasa mgogoro wa gesi Mtwara.
“Serikali za majimbo zitaongeza uwajibikaji kwa viongozi, pia usimamizi mzuri wa rasilimali kila eneo kwa manufaa ya eneo husika ingawa ni kweli kuna gharama zake,” alisema Mzee Mtei.
Alisema utaratibu wa kupatikana wabunge wa viti maalumu na tume ya uchaguzi na viongozi wengine uliopendekezwa na tume ni mzuri.
Mzee Mtei alisema rasimu hiyo inajaribu kujibu malalamiko mengi ambayo yamekuwa yakitolewa.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment