Moshi/Dar. Habari za uhakika kutoka ndani ya Jeshi hilo zimedokeza kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Said Mwema anatarajiwa kustaafu mwezi ujao na haijafahamika kama ataongezewa mkataba ama la.
Vyanzo mbalimbali vimedai kuwa japokuwa IGP Mwema anasita kukubali kuongezewa muda, lakini Rais Jakaya Kikwete anaonelea aongezewe muda ili wamalize pamoja uongozi wao mwaka 2015.
IGP Mwema ambaye alikuwa Ofisi ya Polisi wa Kimataifa (Interpol) Jijini Nairobi, Kenya, aliteuliwa kushika wadhifa wake huo mwaka 2006 na Rais Kikwete, kumrithi Omar Mahita ambaye alistaafu.
Habari zinasema endapo IGP Mwema hatapewa mkataba wa ama miaka miwili, basi ni dhahiri Rais Kikwete atakuwa na kibarua kigumu cha kuanza mchakato wa kumtafuta mrithi wake.
IGP Mwema anachukuliwa kama mmoja wa viongozi wa juu wa Jeshi hilo aliyelifanyia mapinduzi makubwa aliposhika madaraka hayo, ikiwamo kuja na dhana ya ulinzi shirikishi ama Polisi Jamii.
Tayari mabadiliko hayo yameaanza kufanyika kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni jijini Dar es Salaam, Charles Kenyela kuhamishiwa makao makuu ya jeshi hilo.
Taarifa zaidi zimepasha kuwa nafasi nyingine ya juu ambayo kuna dalili ya kuwepo kwa mabadiliko ni ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), inayoshikiliwa na Robert Manumba.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya jeshi hilo aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa (jina linahifadhiwa), amehamishiwa makao makuu wakati tayari kuna taarifa za yeye kustaafu.
Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso alipotakia kueleza juu ya taarifa hizo za mabadiliko ndani ya jeshi hilo, kutokana na muda wa kustaafu kwa maofisa hao kufika alisema hizo ni taarifa za hisia.
“Hizo ni taarifa za hisia zako tu, lakini huwezi kuniuliza swali la mwezi wa saba leo, tusubiri muda ukifika tuone itakuaje,” alisema Senso.
Pia kuhusu taarifa za Kamanda wa Polisi Kinondoni, Charles Kenyela kuhamishia makao makuu alisema; “Subirini nitatoa taarifa kwani mbona kila mabadiliko yanayotokea ya makamanda huwa ninatoa taarifa hivyo subirini”.
Habari zisizo rasmi zimelidokeza gazeti hili kuwa huenda DCI Manumba akapumzishwa kutokana na hali yake ya kiafya kuonekana kutorejea vizuri, licha ya kupatiwa matibabu nchini Afrika Kusini.
Kulingana na taarifa hizo, Kamishna Isaya Mngulu ndiye anayetajwa sana kuweza kumrithi Manumba na hata kupandishwa cheo kutoka Naibu Kamishna hadi Kamishina ni maandalizi hayo.
Inaelezwa kuwa Kamishna Mngulu alikuwa astaafu rasmi Oktoba mwaka huu, lakini kitendo cha kupandishwa cheo kunaongezea nguvu tetesi kuwa ndiye anayeandaliwa kushika wadhifa wa DCI.
Habari nyingine zinadai kuwa wapo makamanda wa polisi wa mikoa ambao nao wanapaswa kustaafu kwa mujibu wa sheria, baada ya kutimiza umri wa miaka 60, lakini kuna dalili ya kupewa mikataba.
Taarifa zilizopatikana zinaeleza kuwa mabadiliko hayo yanakuja huku Jeshi la Polisi likikabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo baadhi ya askari wake zaidi ya 70 kuuawa katika matukio mbalimbali, yakiwamo ya kushiriki katika uhalifu na wengine kukamatwa wakishiriki kufanya uhalifu.
Baadhi ya matukio hayo ni pamoja na lile la askari polisi aliyeuawa kwa kupigwa risasi mkoani Kagera, askari polisi waliochukua fuko la Sh 150 milioni walilookoa kutoka kwa majambazi jijini Dar es Salaam.
Matukio mengine ni gari la polisi kukamatwa likiwa limebeba bangi, pamoja na askari watatu kukamatwa wakiwa na kichwa cha mtu Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro.
Wakati jeshi hilo lilikabiliwa na matukio hayo, hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete aliwapandisha vyeo maofisa 21 wa Jeshi la Polisi kuwa Makamishna wa Polisi (CP) na Naibu Makamishna wa Polisi (DCP), huku wengine wakiwa tayari wamefikisha umri wa kustaafu.
Miongoni mwa waliopandishwa vyeo vya CP ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamhanda ambaye awali alikuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi na Suleiman Kova na Isaya Mngulu, ambao walikuwa Manaibu Kamishna wa Polisi.
Waliopandishwa vyeo kuwa Manaibu Kamishna wa Polisi ni Elice Mapunda, Brown Lekey, Hamdani Omar Makame, Keneth Kasseke, Abdulrahman Kaniki, Thobias Andengenye, Adrian Magayane, Sospeter Kondela, Simon Sirro na Ernest Mangu.
Wengine ni Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga, Hussein Laisser, Anthony Joel, S. Mwami, Adolfina Chialo, Mpinga Michael Gyumi, Ally Mlenge, Herzon Gyimbi na Jonas Mugendi.
Kabla ya vyeo vipya walikuwa Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi.
Habari hii imeandikwa na Daniel Mjema na Ibrahim Yamola.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment