ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 3, 2013

Mwathirika wa bomu anayeishi na chuma mwilini

Dar es Salaam. Juma lilipopita, tuliandika makala ambayo majeruhi walieleza jinsi ambavyo bomu hilo lilitupwa mpaka kutua chini na baadaye kulipuka. Fatma Tarimo (39), Mkazi wa Olasiti mkoani Arusha, anaendelea kusimulia mkasa wa bomu hilo. Endelea...

Alivyoumia
Mpaka Mwananchi inafanya mazungumzo na mama huyo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ambako amelazwa, tayari alikuwa amefanyiwa upasuaji mara tatu ili kutolewa vyuma kwenye maeneo mbalimbali ya mwili wake.“Mpaka sasa hivi nimetolewa vyuma vitatu, kwanza kilikuwa cha mviringo, kingine kama msumari, na kingine kilikuwa na umbo lilokaribia kuwa duara, nimeumia sana kwenye maeneo ya upande wa kulia kuanzia kwenye mguu, mbavu na mapafu,” anasema.

Chuma kwenye mapafu hakiwezi kutoka
Anasema mbali na upasuaji huo aliofanyiwa, kuna chuma ambacho kipo kwenye mapafu na amebainisha kwamba madaktari wamemwambia hakiwezi kutolewa.

“Madaktari wanasema kuna chuma kidogo kwenye mapafu, lakini wanasema hakina madhara na hakiwezi kutoka kwa sababu kipo karibu na sehemu ya hewa,” anasema.

Anaeleza kuwa, alipokuwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, alifanyiwa operesheni ambayo chuma kingine kilitolewa kwenye mapafu.

“Kwa sasa hivi madaktari wanasema vidonda vingine vitapona tu, kwakweli wametuhudumia sana. Kwa upande wa maumivu yapo kwenye mapafu,” anasema.

Bomu lilimgonga begani
Mtu mwingine aliyeumia kwenye tukio hilo ni Jenifa Joachim (34) na anasema kwamba bomu hilo lilimgonga begani na kutua chini.

“Nilidhani ni jiwe limerushwa na watoto, nilikuwa nimemshika mkono mtoto wangu kwa hiyo nikaendelea kufuatilia ibada wala sikuangalia lilipoangukia.

“Baada ya muda kidogo nilisikia kishindo kikubwa, nikasikia miguu inauma, ule moshi ulijaa mdomoni nikashindwa hata kuzungumza.

“Baada ya kike kishindo, nilisikia miguu inauma, sikuweza kukimbia nikawa nimekaa chini, kwa mbali nikaona mtoto wangu anatoa macho nikajua amekufa, sikuweza kumfuata wala kuomba watu wamsaidie kwa kuwa sikuweza kuzungumza wala kunyanyuka,” anasema.

Anasema hivi sasa mtoto wake amelazwa katika Hospitali ya KCMC mkoani Kilimanjaro.
“Sijamwona wala kuzungumza naye mpaka sasa, naambiwa tu kwamba ameumia sehemu ya kichwa, bega na mguu,” anafafanua.

Anaeleza kwamba kwa kawaida mwanaye huyo anakwenda kwenye ibada ya kwanza na kwamba siku hiyo alilazimika kwenda naye kwa sababu kulikuwa na misa moja tu.

“Kwa wiki nzima nilikuwa nimeipania hiyo siku, nilikuwa nimepanga kwa vyovyote siwezi kuikosa.

“Sikutegemea kama kuna kitu kama hicho kinaweza kutokea, wakati nikiwa chini nilishtuka nikasema labda ni mwisho wa dunia, kwa sababu niliona watu wameanguka wanatoka damu kila mahali, nikashtuka kweli,”anasema.
Mwananchi

No comments: