
Bila kupoteza muda ningependa nianze mara moja mada yetu ihusuyo ‘thamani ya ndoa’. Naweza kusema nimeandika makala nyingi kuhusu uhusiano, wapo walioelimika kupitia makala hizo na wapo ambao ziliwapitia kulia na kutokea kushoto.
Ndoa ni nini? Ndoa ni baraka za uhalalisho wa watu wawili wenye jinsia tofauti kuishi pamoja, pia ni muunganiko wa halali wa mwanamke na mwanaume kuwa mwili mmoja. Nina imani mpaka hapo utakuwa umenielewa vizuri zaidi.
Nini thamani ya ndoa kwa mwanadamu? Ndoa ni kujitoa katika vitendo vya kuzini yaani kufanya mapenzi pasipo baraka toka kwa Mungu. Ndoa hujenga heshima ya mtu na kumwekea mipaka ya utaratibu wa maisha ambayo humpendeza Mungu.
Nini nia na madhumuni ya mada hii? Kutokana na utamaduni wa sasa watu kushindwa kuheshimu ndoa zao kwa kufanya mambo ambayo hayawatofautishi kabla na baada ya kuolewa au kuoa.
Tunashuhudia jinsi wanawake au wanaume wavyotawaliwa na tamaa za kimwili na hutoka nje ya nyumba zao na kuwaacha wenzao wao kama fenicha ndani.
Nini kusudio la kuoa au kuolewa? Kufunga ndoa ni kuanza maisha safi yampendezayo Mungu, pia kujenga familia nje ya wazazi wako. Mpaka unaamua kuoa lazima utakuwa umeridhika na mpenzi wako na kuwa tayari kuanza safari ya maisha mapya. Nini kinachotakiwa baada ndoa? Kwa vile mmeamua kuwa mwili mmoja, basi nyinyi huwa kama viungo vya mwili. Sidhani kama kuna kiungo kitamtegea au kumchukia mwenzake.
Kikiumwa kidole basi mwili mzima huwa taabuni, na katika mapenzi vilevile ni kuwa kitu kimoja au mwili mmoja katika taabu na raha na kuridhika na mwenzako.
Hii ni kwa mwanamume kumpenda mkewe na mwanamke kuhuheshimu mumewe. Wanandoa, lao huwa moja, hukaa chini na kujadiliana pamoja kuondoa kero zinazoweza kuweka nyufa ndani yao.
Kuoa ni kufunga mlango wa mabaya yote na kujenga pepo ya duniani. Wana ndoa pendaneni mapenzi ya kweli yenye upendo na huruma. Mke asimuudhi mumewe, vilevile na mume usimuudhi mkewe.
Ila kuna watu huingia kwenye ndoa kwa kufuata mkumbo hata hufanya jambo lolote lililo nje ya ndoa bila wasiwasi. Hawa si waoga, wenye kiburi, hawaridhiki na mpenzi mmoja, wametawaliwa na tamaa ya mwili zaidi, waongo na mambo yao mengi yametawaliwa na usiri zaidi.
Hawajutii makosa yao, huamini wapo sahihi kwa kila walifanyalo. Ndoa hizi hazidumu na huvunjika wakati wowote au huwa mateso kwa upande mmoja. Aliyeingia katika ndoa kwa dhamira ya kweli ni mpole, mnyenyekevu na mwenye huruma. Huchukia kila lililo baya, ni mwalimu mwema kwa mwenzake na kuwa mbunifu wa kuongeza furaha ndani ya nyumba yao. Ndoa hizi hujaa baraka na amani.
Thamani ya ndoa ni kubwa kuliko unavyofikiria, ndoa si maigizo bali kujitoa kwa ajili ya wenzako na lazima mtafanikiwa.
No comments:
Post a Comment