Watoto wa nchini Afrika Kusini wakimwombea Rais Mstaafu wa nchi hiyo, Nelson Mandela nje ya Hospitali ya Medi Clinic alipolazwa kwa matibabu. Picha na AFP
Johannesburg: Wakati kukiwa na vita ya chini kwa chini dhidi ya vyombo vya habari vinavyofuatilia mwenendo wa afya ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, kumekuwa na pilika nyingi katika makazi ya kiongozi huyo yaliyopo eneo la Houghton, Mtaa wa Laan 12, jijini Johannesburg.
Leo ni siku ya 22 tangu Mandela alazwe katika hospitali ya magonjwa ya moyo, Medclinic iliopo Pretoria akiugua ugonjwa wa figo na katika siku saba zilizopota taarifa rasmi zinasema “hali yake ni mbaya”.
Usiku wa kuamkia jana, Mwenyekiti wa taifa wa chama tawala cha ANC, Baleka Mbete aliongoza maombi ya kumwombea Mandela kwa wanachama na makada wake waliopo majimbo ya Cape Town na Eastern Cape huku akisisitiza:
“lazima wananchi wa Afrika Kusini, wafike mahali wamruhusu Mandela ampumzike kwa mapenzi ya Mungu”.
Wakati hayo yakiendelea pilika katika makazi ya Mandela ziliwahusisha makundi ya watu na kampuni kadhaa za jijini Johannesburg, wakiwamo watu waliokuwa wakifanya usafi.
Kazi hiyo ilifanyika kwa kufagia na kuzoa taka, usafi wa vitalu na kubadilisha mawe, utengenezaji wa bustani za maua na pia mafundi waliokuwa wakifanya shughuli za marekebisho ya njia za umeme katika eneo hilo.
Mmoja wa majirani katika eneo hilo alyejitambulisha kwa jina la Jacob Brews alisema: “Huwa watu wanafanya usafi hapa lakini ninaona kama leo kuna jambo la ziada hapa. Maana watu ni wengi na kila mmoja anaonekana anatekeleza wajibu wake”.
Katika nyumba hiyo kulikuwa na idadi kubwa ya magari kuliko kawaida na ilipotimu saa 6.00 mchana magari saba yalikuwa yameegeshwa mbele ya lango la nyumba hiyo ikiwa ni ishara kwamba wahusika wake walikuwa ndani.
Mwananchi lilishuhudia magari mengine yakiingia ndani na kutoka kila baada ya muda, huku baadhi ya wageni wakiingia ndani wakiwa wamebeba maua. Kabla ya jana hakukuwa na watu wengi walioonekana wakiingia katika nyumba hiyo.
Watu wanaodhaniwa ni maofisa usalama pia walikuwa wametapakaa nje ya makazi hayo walikuwa wakifuatilia kwa karibu mazungumzo ya waandishi wa habari na walinzi pamoja na watu waliokuwa wakifanya shughuli mbalimbali.
Mmoja wa walinzi hao aliliambia Mwananchi kuwa hawezi kuzungumza chochote. “Tunafuatiliwa sana maana hawataki tuzungumze chochote kile ambacho kinatokea huko ndani, labda kama ungenitafuta nje ya hapa”.
Pilika zilivyokuwa
Kuanzia saa 2 asubuhi kundi la kinamama lilikuwa likifanya usafi katika eneo la mbele ya nyumba ya Mandela ikiwa ni pamoja na kufagia barabara na kuzoa uchafu. Kina mama hao ambao pia walikuwa na mbwa, ilibainika kuwa ni wafanyakazi wa kampuni ya usafi.
Baadaye lilifika kundi jingine la wafanyakazi waliokuwa kwenye magari mawili na mara moja walianza kutengeneza bustani za maua ambazo ziko kaskazini mwa makazi ya Mandela.
Baadaye yaliwasili magari mengine mawili ambayo yalikuwa yamesheheni mawe madogo na baada ya kuwasilia eneo hilo, ilianza kazi ya kusafisha vitalu vya mawe na maua ambavyo vimekuwa vikitumiwa na watu kwa ajili ya kuweka maua na kutoa salaam za pole kwa Mandela.
Usafi huo ulihusisha kuondoa maua yaliyonyauka na kukusanya na mabaki ya maua hayo chini ya mti uliopo kwenye lango la kuingilia nyumbani kwa Madiba. Ndani ya vitalu kuliwekwa mawe (babbles) mapya yenye rangi nyeupe, nyekundu, njano na bluu.
Saa tano na dakika kadhaa, yalifika magari mawili makubwa yaliyokuwa na mafundi wa umeme ambao walionekana wakiifanyia kazi njia ndogo ya nishati hiyo inayoingia katika makazi yaliyopo mtaa huo wa Laa 12 na baada ya saa moja hivi yaliondoka.
Muda wa mchana magari ya polisi yaliyokuwa yakipiga ving’ora yaliwasili eneo hilo yakiongozana na kundi la vijana na watoto ambao walianza kuimba, kuweka maua chini ya mti uliopo eneo hilo na baadaye kufanya sala.
Vijana na watoto hao walikuwa wamevalia fulana zinazowatambulisha kuwa na kundi linalojihusisha na usafi na baada ya maombi walichukua mifuko myeusi ya plastiki na kuanza kuokota takataka katika mtaa huo na walielekea upande wa kaskazini wakisindikizwa na magari manne ya polisi.
Hali hiyo iliufanya mtaa huo kuwa wenye pilika kwa saa zaidi ya saba huku waandishi wa habari wakipigana vikumbo kupata picha na mahojiano ya matukio hayo ambayo hayakuwa ya kawaida.
Viongozi wa makundi yote yaliyofika katika eneo hilo kwa shughuli hizo, hawakuwa tayari kusema chochote na badala yake walisisitiza kuwa shughuli zao zilikuwa za kawaida na hakuna tukio lolote maalumu.
“Tuko katika kazi zetu za kawaida wala hakuna tukio maalumu. Imekuwa ni bahati mbaya kwamba wote tumekutana hapa kwa wakati mmoja lakini naamini kwa upande wangu hakuna zaidi ya kazi hii ya kusafisha vitalu na kuweka mawe mapya,”alisema mmoja wa viongozi wa makundi hayo huku akikataa kata kata kutaja jina lake.
Polisi na waandishi
Jana asubuhi polisi mjini Pretoria waliwaamuru waandishi wa habari kuondoa magari na vifaa vyao nje ya hospitali ya wagonjwa wa moyo ya Medclinic alikolazwa Mandela, kwa kile walichosema kuwa “sababu za kiusalama”.
Hata hivyo hadi jana jioni, hakuna chombo hata kimoja cha habari katika eneo la hilo ambacho kilikuwa kimeondoa vifaa vyake na badala yake viliendelea kusubiri sehemu hiyo, ikiwa ni siku ya 21 tangu Mandela alipolazwa kutokana na ugonjwa wa figo.
Kadhalika amri hiyo ya polisi imekuja siku moja tangu binti mkubwa wa Mandela, Makaziwe alipovikosoa vyombo vya habari kwamba vimeshindwa “kuheshimu desturi za Kiafrika pamoja na hisia za familia” kuhusu ugonjwa wa baba yake.
Alitoa mfano wa uwapo wa kamera na vifaa vya kurushia matangazo katika njia kuu ya kuingilia hospitalini hapo kwa kusema:
“Huwezi kujua ni nini kinaendelea hospitalini, ni vigumu hata kuingia kwa sababu ya hali ya kutojali iliyopo”.
Wakati huohuo, Mahakama Kuu ya Mthatha, jana ilimwamuru mjukuu wa Mzee Mandela, Mandla kurejesha mabaki ya miili ya marehemu ambao ni wanafamilia wa Mandela aliyokuwa ameyahamisha kutoka eneo la Qunu.
Mandla ambaye hakuwapo mahakamani alihamisha mabaki ya marehemu watatu mwaka 2011 kutoka eneo la Qunu na kwenda kuyazika Mvezo ambako alizaliwa Mandela. Mjukuu huyo alishtakiwa na ndugu wengine wa familia hiyo.
Mandla amekuwa kwenye mvutano kati yake na ndugu zake hao akitaka babu yake atakapofariki azikwe Mvezo wakati familia inasisitiza kwamba matakwa ya Mzee Mandela mwenyewe kuzikwa
Mwananchi
No comments:
Post a Comment