ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, June 27, 2013

SAFARI YA RAIS KIKWETE SUNDERLAND AFC : MPENDA KWAO HUTUNZWA.

 Bendera ya Tanzania inapepea nje ya Stadium of Light. Uwanja huu una uwezo wa kuchukua watazamaji 49,000
 Mh Raisi katika picha Ya pamoja na watoto wa Academy of Light.
 Mheshimiwa Rais akiongea na watoto wanaoendeleza ujuzi wa mpira Academy of Light. Kulia ni Waziri wa Habari, Vijana, Michezo na Utamaduni, Dk Fenella Mukangara.

Rais na msafara ulionyeshwa zana mbalimbali zilizomo chuo cha Academy of Light yakiwemo mabwawa ya kuogelea, sehemu za matibabu, mazoezi ya viungo, vyuma na mashine (Gym), viwanja vya ndani na nje, nk.

Huo ndiyo mpango wenyewe.

Tumeshaletewa vifaa vya mapishi; sasa “kazi kwetu. “

Siri kuu ya klabu na nchi zinazotuzidi duniani kimichezo ni matayarisho ya aina hii. Klabu maarufu ya Barcelona (na Spain yenyewe ambayo ni viongozi wa kandanda ulimwenguni sasa hivi) ni kuwa na wachezaji waliojengwa vizuri wakiwa watoto.

Lionel Messi, Xavi Hernandez, Andreas Iniesta walianzia chuo cha La Masia chenye zaidi ya wanafunzi 300. La Masia ilianzishwa mwaka 2002 na matokeo yake ndiyo haya.

Kwa maelezo na picha zaidi Bofya read more


Mfano mwingine mzuri zaidi (na unaotufaa sisi Tanzania) ni ule wa klabu ndogo isiyojulikana sana Bongo yaani Southampton FC, kusini ya Uingereza. Southampton Football Club ina chuo ambacho miaka ya karibuni kimechanusha wachezaji wazuri sana na watatu wameshajulikana ligi ya Uingereza : Theo Walcott (Arsenal), Gareth Bale (Tottenham) na Alex Oxlade- Chamberlain (Arsenal). Gareth Bale ni mmoja wa washambuliaji hatari duniani na klabu kubwa kubwa ikiwepo Real Madrid zinamwinda kama swala.

Na ndiyo maana Rais Kikwete alipoulizwa kwanini katembelea Sunderland (iliyoshika nafasi ya 17 ndani ya timu 20 zilizoshiriki ligi ya 2013) na sio Chelsea, Liverpool au Manchester City akajibu wao ndiyo walio tayari kutusaidia. Ikumbukwe kwamba Academy of Light, ni kati ya vyuo vinavyoheshimika Uingereza nzima.

Naam. Wako tayari kutusaidia.

Tuangalie tatizo letu kuu.

Hatuamini faida ya michezo. Hatuwezi kukataa kwamba si wazazi wengi wa Bongo wanaoamini kwamba mtoto wao akizama michezoni atajenga ajira. Hatuchangamkii michezo kiajira kama walivyo wenzetu. Mwangalie mchezaji mashuhuri Wayne Rooney wa Manchester United ambaye ingawa hakusoma sana leo katajirika, anasaidia familia na jamii yake. Mifano ni mingi sana. Afrika tunae mchezaji mstaafu wa Nigeria, Nwankwo Kanu (kaacha kucheza akiwa na umri mbichi wa miaka 36 na sasa tajiri); licha ya kuwa mgonjwa wa moyo akiwa mtoto, ilibidi atibiwe kutokana na kipaji chake na hatimaye akaiongoza Nigeria kushinda kombe la Vijana Afrika (1993), Olimpiki (1996) na tuzo kadhaa akiichezea kazuzu, Arsenal (1999-2005). Leo anafanya mengi Nigeria ikiwepo kudhamini hospitali ya watoto wagonjwa wa moyo.

Tubadili utayarishaji wetu. Twahitaji mosi, kuchangamkia michezo, pili, kuwasaidia watoto na vijana wetu wanaoanza ngazi za chini, vijijini hadi pembe za chaki mijini.

Leo kwetu Tanzania wachezaji wazuri “huanza” kuingizwa ulingoni wakiwa na umri wa miaka 17 kuendelea. Wenzetu wanaoshinda huzingatia methali ya “samaki mkunje angali mbichi.” Watoto wanaoonekana kuwa na vipaji kimichezo huanza kuokwa na kupewa misaada ya hali na mali, wakiwa na umri mdogo wa miaka mitano. Rais alijionea mwenyewe watoto hawa na kufurahia na wenzake akiwemo, Mheshimiwa Peter Kallaghe ambaye pamoja na Ubalozi wa Tanzania , London waliiratibu ziara na shughuli hii muhimu kitaifa.

Imeandikwa kwa ushirikiano wa Urban Pulse na Freddy Macha
 Mwenyekiti wa Sunderland AFC, Ellis Short akimwonyesha Rais Kikwete uwanja maarufu wa Stadium of Light.
 Rais akielezwa namna vijana wachezaji wanavyohudumiwa wakiumia. Majeruhi ni Tom Beedling na mganga wake , Jamie Oldroyd.
 Rais Kikwete akiongea na wanahabari wa SKY baada ya matembezi ya viwanja vya Stadium of Light na chuo cha Academy of Light.
 Rais Kikwete akionyeshwa mchoro wa chuo cha mpira kitakachojengwa Dar es Salaam na kampuni ya Symbion.
Watoto wenye vipaji wakionyesha ufundi wa kandanda, chuo cha Academy of Light. Samaki mkunje angali mbichi.

No comments: