Dar es Salaam. Tume ya Kuchunguza Matokeo ya Kidato cha Nne iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda imebaini zaidi ya matatizo 20 yanayozorotesha kiwango cha elimu na hata kusababisha maelfu ya wanafunzi kufeli mtihani wa kidato cha nne mwaka 2012.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Profesa Sifuni Mchome alisema inachunguza mfumo mzima wa elimu na kuwa suala la Matokeo ya Kidato cha Nne mwaka 2012 ni moja kati ya mambo wanayoyafanyia kazi.
Mchome ameeleza hayo siku moja baada ya gazeti dada la ‘The Citizen’ kuchapisha habari za kujiuzulu kwa mmoja wa Wajumbe wa Tume hiyo, Rakesh Rajani aliyefikia uamuzi huo kutokana na kile alichosema ni kutoridhishwa na pendekezo la kufutwa kwa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne.
Alisema ripoti ya Tume hiyo itakayowasilishwa kwa Waziri Mkuu, Juni 15 mwaka huu, imebaini mambo mengi ikiwa ni pamoja na mitalaa kupitwa na wakati pia idadi ya wanafunzi kuwa kubwa na kuelemewa kwa mfumo wa elimu nchini.
“Kuna mambo ya kuangalia ubora, kuna suala la ofisi na taasisi mbalimbali zinafanya kazi gani? Vipi uwajibikaji wake, majukumu yake na mgawanyo ukoje, Ofisi ya Kamishna inahusika vipi na mitihani, huku kote tumeona kuna matatizo,” alisema.
Alisema pia morali ya walimu imeshuka, jambo linalofanya wengi kuwa tayari kuachana na kazi hiyo wakipata jambo jingine la kufanya.
“Wengi morali imeshuka, wangepata nafasi ya kuchoropoka (kuondoka) wangekimbia, lugha ya kufundishia ni tatizo na mchango wa wazazi kwenye elimu ni wa kuangalia, yote haya ni matatizo,” alisema.
Alisema kuna haja ya sera mpya ya elimu ambayo imekuwa ikizungumzwa tangu mwaka 2008 ili kutatua matatizo yaliyopo sasa.
Akizungumzia kujiuzulu kwa Rajani, alisema sababu aliyotoa haina msingi kwani muda mwingi hakuweza kufanya kazi na tume hiyo.
“Rajani ushiriki wake kwenye tume ni chini ya asilimia 10, muda mwingi alikuwa anasafiri au anakuwa kwenye kazi za asasi yake, mambo mengi alikuwa hajui na sisi tulikuwa kila kitu tunaamua kwenye vikao, kuna kazi tuliyompa ya kuangalia kama kila tulichojipangia kimefanyika kwa wakati, alishindwa kwa sababu muda mwingi hakuwapo,” alisema:
Alisema kuwa, msimamo wa Rajani ulikuwa ni kuachana na wanafunzi waliofeli na badala yake tume ijikite kuangalia mambo mengine, jambo alilosema lilikataliwa na wajumbe wengine.
“Sisi tuliona kuwa ni ukweli mfumo uliotumika kupanga matokeo ulikuwa tofauti na kukaonekana kwamba ukibadilishwa matokeo yatakuwa tofauti, ndiyo maana tukasema matokeo yapangwe upya.
“Angeeleza tu kuwa amejiuzulu kwa kuwa hana muda wa kufanya kazi za tume, (Mbunge wa Kuteuliwa James) Mbatia alifanya vyema alikataa kuwa mjumbe mapema akasema ameshatoa maoni yake kwa mfumo mwingine,” alisema.
Akizungumza jana, Rajani alisema kwenye barua yake ameeleza kwa kina sababu ya kujiuzulu na suala la msingi ni kujadili hoja na siyo kujiuzulu kwake... “Hapa tusiangalie juu ya mimi kujiuzulu, tuangalie kama ni sahihi kubadili matokeo yale.”
Sehemu ya barua ya Rajani kwa Waziri Mkuu inasema kuwa “Kiuhalisia, tulipoteza fursa ya kipekee kuelezea kwa umma kwamba alama za ufaulu zinazotumiwa siku zote zimekuwa wastani wa asilimia 35, kiukweli hiki ni kiwango cha chini cha viwango vya kimataifa na Afrika kwani nchi nyingi zinatumia alama za ufaulu kati ya asilimia 40 na 50 na utaratibu wetu kutumia asilimia 21 shuleni kama alama ya kufaulu ni kiwango cha chini mno na unapoteza thamani ya maana ya elimu.”
Mwananchi
No comments:
Post a Comment