AWALI ya yote nimshukuru Mungu kwa kunijaalia uwezo wa kuandika yale ambayo yana mchango mkubwa katika jamii inayonizunguka.
Utakumbuka wiki iliyopita nilianza kuzungumzia mada yenye kichwa cha habari kilichopo hapo juu na leo nitaimalizia ili wiki ijayo nianze nyingine.
Kama nilivyotangulia kusema, mapenzi yanachukua nafasi kubwa sana katika maisha yetu hivyo tunatakiwa kuwa makini nayo sana kwani tukiyakosea kidogo tu yanaweza kutufanya tukayaona maisha ni machungu kuliko hata shubiri. Mifano tunayo mingi huko mtaani. Tunawaona watu ambao wanaonekana kuchanganyikiwa kwa sababu wametendwa. Cha msingi ni kutokubali mapenzi yatutibulie maisha yetu.
Kama umeachwa, kumbuka wewe siyo wa kwanza kuachwa. Wapo walioachwa na wapenzi wao lakini waliweza kukabiliana na hali hiyo na leo wapo na wapenzi wengine na wanayafurahia maisha.
Wapo pia ambao walipewa talaka na waume zao kwa sababu zisizo na mashiko lakini waliona ni hali ya kawaida na wakakubaliana nayo, leo wamepata wanaume wengine ambao wamewaoa na wana amani mioyoni mwao.
Wapo pia ambao walipewa talaka na waume zao kwa sababu zisizo na mashiko lakini waliona ni hali ya kawaida na wakakubaliana nayo, leo wamepata wanaume wengine ambao wamewaoa na wana amani mioyoni mwao.
Kumbuka kila mmoja ana maisha yake, leo hii ukikubali kuchanganyikiwa na kushindwa kutimiza majukumu yako ya kila siku eti kwa sababu fulani kakuacha, utakuwa unakubali huyo aliyekuacha akuharibie na maisha yako, uko tayari kwa hilo?
Yaani mtu kakupa maumivu ya kukuacha halafu akupe na maumivu na kuwa na maisha mabaya kwa kushindwa kufanya kazi zako kwa ufasaha, inaingia akilini kweli?
Kamwe usikubaliane na hilo. Amekuacha, mwache aende na wewe baki na maisha yako na amini utampata mwingine ambaye atakuwa ni bora kuliko huyo aliyelipiga teke penzi lako.
Mwisho naomba niseme kwamba, mapenzi yasituharibie maisha yetu. Ni kweli inauma pale tunapowakosa wale tuliotokea kuwapenda lakini isiwe sababu ya kutuyumbisha kimaisha.
Tufahamu kwamba, kila kinachotokea katika maisha yetu ni mipango ya Mungu. Ukiachwa ujue huyo aliyekuacha hakustahili kuwa wako na kama utang’ang’ania kuwa naye ipo siku atakutenda na utajuta.
Ukimfumania, huyo hastahili kuwa wako. Anaonesha wazi si muaminifu na uamuzi sahihi ni kumuacha aendelee na maisha yake. Kumkumbatia eti kwa kuwa kakuomba msamaha na kueleza kuwa shetani kampitia, utakuwa unapalilia tatizo.
Ukiona dalili za wazi kwamba hana mapenzi ya dhati na wewe kwa kukufanyia vitendo ambavyo vimekuwa vikikukosesha amani katika maisha yako, fanya haraka kumuacha kwani kwa kufanya hivyo utabaki na amani kuliko kuendelea kumvumilia.
Kumbuka mtu anayeonesha dalili za wazi za kutokuwa na mapenzi ya dhati na wewe ipo siku atakuacha na utaumia sana. Utaumia sana kwa kuwa, utakuwa hujajipanga kuachana naye lakini ukimuacha wewe angalau utakuwa na nafuu kwa kuwa umejiandaa kumkosa.
Kikubwa ni kuyathamini maisha yetu kuliko kitu kingine.
Tusiwape nafasi watu watuharibie maisha yetu. Tuna haki ya kupenda lakini kupenda kwetu isiwe sababu ya maisha yetu kuwa katika mazingira mabaya.
No comments:
Post a Comment