Katika maadhimisho hayo, imebainika kuwa Watanzania bado wako nyuma katika unywaji wa maziwa ikilinganishwa na Kenya au nchi nyingine zilizoendelea kama Uholanzi na New Zealand.
Mwambungu, kwa upande wake akawataka wananchi kujenga utamaduni wa kupenda kunywa maziwa kila siku badala ya kusubiri wang’atwe na nyoka au wadudu ama washauriwe na madaktari.
Akasema Mwambungu kuwa watu wengi wamekuwa wavivu katika suala la unywaji wa maziwa ikilinganishwa na kasi wanayoitumia kwenye unywaji wa pombe ambapo baadhi yao wamekuwa mabingwa wa kushinda au kukesha baa.
“Kama ningekuwa daktari, ningetamani kumweleza kila mgonjwa anayekuja hospitali kupata matibabu kwamba ili apone vizuri anatakiwa kwanza kunywa maziwa. Ninadhani wengi wangefanya hivyo,” akasema Mwambungu. Akaongeza kuwa kasi ya unywaji wa maziwa mkoani Ruvuma ni wastani na lita 11.6 kwa mtu kwa mwaka na kuongeza kwamba takwimu za uzalishaji wa maziwa na unywaji wake nchini zinaonyesha kuwa Watanzania hutumia wastani wa lita 45 kwa mwaka.
Akaongeza kuwa viwango vinavyopendekezwa kimataifa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) na lile la Chakula na Kilimo (FAO) ni lita 200 kwa mtu kwa mwaka ambazo zinakaribiwa na Kenya wanaokunywa lita 140.
Kutokana na hali hiyo, RC Mwambgungu akawataka wananchi wa mkoa wake kuyatumia maadhimisho hayo kama darasa katika kujifunza mbinu bora za ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na usindikaji wa maziwa kwa ajili ya kuinua kiwango cha upatikanaji wa maziwa hayo.
Pia, aliwaasa wananchi hao kuacha kasumba kuwa kunywa maziwa ni mpaka mtu augue.
Akasema kuwa serikali itaendelea kuboresha sekta ya maziwa ili iendelee kutoa matokeo chanya na hatimaye kuhamasisha wananchi wengi kufuga ngombe wa maziwa kwa lengo la kuboresha afya kwa kunywa maziwa na kuongeza kipato na uchumi wa kaya na hatimaye taifa. Aliishauri Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi haina budi kuanzisha mradi wa maziwa katika shule nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji Maziwa, Hamis Mzee alisema kuwa maadhimisho hayo yalipelekwa Ruvuma baada ya kufanya tathmini na kuona mwamko wa unywaji maziwa ni mdogo.
Aliwataka wananchi hao kujenga utamaduni wa kuchemsha maziwa kabla ya kuyanywa ambapo alieleza kwamba familia isiyopenda kunywa maziwa ukuaji wake unakuwa wa shida.
Aidha, wananchi Ruvuma wakaitaka Kampuni ya Asas Dairies kupeleka huduma zake mkoani humo ili waweze kunufaika na huduma hiyo.
Katika maonyesho ya yaliyo fanyika Mkoani Ruvuma Mei 29 hadi Juni Mosi 2013 kwenye viwanja vya Manispaa Songea, baadhi ya wazalishaji na wasindikaji wa maziwa ikiwamo Kampuni ya Asas ya mjini Iringa walishiriki.
Asas, kwa upande wao ilijinyakulia medali tano (5), mbili za dhahabu , moja ya fedha , moja ya ushiriki na moja ya ushindi wa jumla.
Ushindi huo wa kishindo ulitarajiwa na wengi ambao walijaa katika banda la Asas kwa lengo la kununua na kuuliza mambo mbalimbali kuhusu bidhaa za kampuni hiyo.
Mafanikio yao
Asas Dairies kwa upande wake ikaeleza kuwa inajivunia ubora wa bidhaa zake ambazo zinapendwa na kutumiwa.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment