ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 26, 2013

Wachezaji wasisajiliwe bila kupimwa afya

Wote tunafahamu umuhimu wa kupima afya na jambo hili siku zote limekuwa likisisitizwa na wataalamu wa afya duniani kote.

Wataalamu wanashauri umuhimu wa kufanya vipimo mara kwa mara, kwani kwa kufanya hivyo kunasaidia kugundulika mapema kwa baadhi ya magonjwa na hivyo kufanikisha matibabu yake mapema.

Lakini kama ilivyo kwa watu wengi kutokuwa na utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara, ndivyo ilivyo kwenye klabu zetu ambazo zimekuwa zikisajili wachezaji bila hata kuwapima afya zao.

Mifano ya namna utaratibu wa kuwapima afya wachezaji unavyopuuzwa, unaonekana zaidi kipindi hiki cha usajili wa wachezaji hasa wale wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Tumesikia mara kupitia vyombo vya habari taarifa za klabu kusajili wachezaji wapya kadhaa, lakini hatujawahi kusikia zoezi hilo likienda sambamba na upimaji wa afya za wachezaji hao.

Klabu zinafahamu kwamba ni utaratibu wa kawaida unaposajili wachezaji wapya kutoka timu nyingine, basi ni lazima kazi ya kwanza kabla mchezaji kuingia dimbani apimwe afya.Lakini kinyume chake jambo hili limekuwa likipuuzwa na viongozi wa klabu pamoja na kwamba wanafahamu taratibu zinawataka kufanya hivyo na hakuna hatua zozote zinazochukuliwa.

Suala la kupima afya halipaswi kufanya la siri, na kwa vile hatujasikia klabu zikieleza wazi kuwapima afya wachezaji wao wapya, basi tunashawishika kuamini kuwa halifanyiki.

Klabu zinajiridhisha na afya za wachezaji wanaowasajili kwa kuwaangalia machoni, jambo ambalo ni hatari na linaloweza kuwaingiza kwenye gharama kubwa mbele ya safari.

Leo hii klabu zinazocheza Ligi Kuu Tanzania Bara ziko 14, na kila siku tumesikia moja baada ya nyingine ikitangaza kusajili wachezaji wapya, lakini hatujawahi kusikia taarifa za afya za wachezaji hao.

Unaweza kusema, pengine suala la ukata limechangia kwa kiasi kikubwa klabu kupuuza zoezi hili. Lakini unapata shaka ni gharama kiasi gani klabu itatumia kumwita daktari kumpima mchezaji afya.

Tunaweza kuiga wenzetu, leo hii mchezaji Wayne Rooney wa Manchester United kama atahama kwenda Chelsea au Arsenal hawezi kuingia uwanjani bila kwanza kupimwa afya yake.

Ni utaratibu wa kawaida na taarifa za vipimo vya afya hutangazwa bila vificho tofauti na kinachoendelea kwenye klabu zetu. Wachezaji wanasajiliwa bila kupima afya.

Kuna faida nyingi za kupima afya mapema. Kwanza mchezaji atafahamu mapema kama ana tatizo, lakini pia upimaji wa afya huendana na ushauri wa kitaalamu wa namna ya kufanya mazoezi kutegemea na mwili wa mtu.

Inashangaza hata wachezaji wenyewe hawaonyeshi kuwa na moyo wa kupimwa afya zao wanapohamia timu zingine. Wakishasaini mikataba mipya na kupata mamilioni, basi wanadhani ndiyo mwisho wake.

Tumeshuhudia matukio mengi ya wachezaji kuanguka uwanjani na kufariki, na wengi wao baada ya uchunguzi walikuwa na matatizo ambayo mwanzo wake siyo ghafla ili uwepo wa matatizo ya muda mrefu.

Klabu lazima zijenge utaratibu wa kuwapima afya wachezaji wao, siyo tu wapya bali hata wale wa zamani kila baada kipindi fulani ili kuwasaidia kuendelea kucheza kwa muda mrefu kutegemea na afya zao.

Mwananchi

No comments: