
Wiki iliyopita nilieleza ukweli kuhusu kuongozwa na hisia. Jitahidi uwe unazishinda kwa maana zinaweza kukuongoza ndivyo sivyo. Ukiongozwa na hisia utajikuta unafanya makosa mengi kila siku. Fikiria kuwa kuna kitu kinakunong’oneza kuhusu ubaya wa mwenzi wako. Kwa nini hali inakuwa hivyo?
Iwe umepata majibu ya swali hilo au hujapata, weka kituo halafu tafakari tena; Hisia kuhusu ubaya wa mwenzi wako zinakutesa, kila baada ya muda, zinakukumbusha ndani kwa ndani. Kama hutakuwa makini, unaweza kujikuta unafanya uamuzi wa kijinga ambao kwako baadaye utakusababishia mateso.
Ukweli; Hisia chanya siku zote zinatokana na mguso wa Mungu, hisia hasi huchagizwa na ushawishi wa Shetani. Hivyo basi, unaweza kumhukumu mwenzi wako kwa sababu hisia zako zimekutuma. Hisia hasi ni kichocheo cha jazba, kwa hiyo kuwa mwangalifu sana juu ya hilo, unaweza kujizulia aibu.
Hebu jiwekee utaratibu wa kupenda kusikiliza kutoka kwa mwenzi wako kabla ya kupandisha jazba na kumvaa ukiwa mbogo kisha kumshushia maneno mazito ukimtuhumu. Fanya mazoezi ya kuufuga moyo wako kwanza ili upate nafasi ya kumsikiliza mwenzi wako, usikie anakwambia nini.
Pengine katika maelezo yake ukapata suluhu itakayokuweka mbali na maumivu ya moyo kuliko hatua ambazo utazichukua kutokana na kuongozwa na jazba. Umeona SMS ya mapenzi kweye simu ya mwenzi wako kutoka kwa mtu mwingine, huwezi kujua kama iliingia kwa bahati mbaya kama hutataka kusikiliza.
Ni kazi sana kusikiliza wakati umeona kitu unachoweza kukilinganisha na ukweli. Hata hivyo, nakusihi ufanyie mazoezi suala la kuufunga moyo. Kwa maana moyo huamsha hisia zinazoweza kukupeleka kwenye uamuzi wa haraka, ukatoa hukumu ambayo siyo. Siku ukijua kama ulimhukumu mwenzi wako kimakosa, utaumia sana.
Ni ukweli kwamba kila mmoja wetu anapojisikia kuumia, lazima apatwe na hali ya hasira na kuchanganyikiwa. Ni hapo ndipo hutaka kufanya kitu cha kujiweka salama na wakati huohuo kumbomoa yule ambaye unadhani amekutenda. Hebu fanyia kazi hilo, hisia zisikuongoze. Kila hisia, ifanyie kazi kwanza.
9. TUNZA MIPAKA
Kuna mambo ambayo wakati mnaanza uhusiano na mwenzi wako, ulikuwa unamficha sana. Hebu angalia madhara ya kumfunulia leo. Kama unaona kutakuwa na chembechembe za kukushusha thamani au kukuona siyo mwaminifu baada ya kumweleza ukweli leo, ni bora uendelee kumficha.
Ulikuwa umemuwekea mipaka. Tafakari tena, je, kuna sababu ya kuifungua leo? Unaweza kumfungulia leo, ukamfanya naye akuone ulikuwa unamtenga na kumnyanyapaa siku za nyuma. Kuepuka hilo, ni bora uendelee kuifunga. Tena ikiwezekana endelea kuitunza na usiifungue ili kulifanya penzi lizidi kustawi.
Kuna faida kubwa katika kuweka mipaka. Siyo tu katika kuitunza ile ambayo tayari ulishamuwekea mwenzi wako tangu awali, bali pia kwa watu wengine ambao wanaweza kuharibu uhusiao wenu. Ishi kwa uangalifu, itakusaidia kumfaya mwenzi wako atulie na wewe.
Unahitaji maisha ya kimapenzi yawe matamu, kwa hiyo hutakiwi kuchokoza shari mweyewe. Unaposhindwa kuwadhibiti watu ambao wanaweza kumfanya mwenzi wako akose imani na wewe, unakuwa unajikaanga kwa mafuta yako mwenyewe. Mapenzi yatakutesa, utajuta.
Kuna shida kubwa kwa baadhi ya watu. Pengine mwanaume anamtuhumu mwenzi wake kwamba anatoka kimapenzi na mtu mwingine kutokana na mazoea waliyonayo. Mwanamke anashindwa kulifanyia kazi hilo na kuishia kutoa majibu mepesi bila kujua athari ya kinachoweza kutokea baadaye.
Kadhalika, mwanamke haamini uhusiano wa kirafiki alionao mwenzi wake na mwanamke mwingine. Badala ya kuheshimu hisia za mwenzake, anaendelea kuukenulia huo uhusiano wa pembeni wakati hauna faida. Ni ujinga wa hali ya juu kumchekelea mtu ambaye anamuumiza mwandani wako.
Huyo mtu unayemchekea, anapiga simu mpaka usiku wa manane. Mwenzi wako anaona anaonya lakini wewe unamjibu “aah, huyu ni mshkaji tu wa story”, hizo ni stori gani za usiku wa manane. Kwa nini halali? Anajua wewe upo na mwenzako, kwa nini anashindwa kumheshimu?
Pengine yeye yupo ‘singo’, kwa hiyo hana mtu wa kumzuia kukupigia ndiyo maana anapojisikia kukutwangia, haogopi hata ikiwa usiku wa manane. Anakufanya wewe ndiye liwazo lake la usingizi. Amekosa wa kumpa kampani, anaona wewe ndiye kimbilio lake.
Tambua kwamba kufanya hivyo ni kumvunjia heshima mwenzi wako. Kwa vile unaujua ukweli kuwa yeye akiwa anapigiwa simu nyakati za usiku na watu wa jinsi yako utakasirika, basi hupaswi kuzichezea hisia zake. Mwambie huyo rafiki yako na akuelewe ili aache hiyo tabia yake.
Itaendelea wiki ijayo.
Global Publishers
No comments:
Post a Comment