Advertisements

Wednesday, July 24, 2013

Akamatwa akitengeneza silaha kienyeji

Kaimu Kamishna wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Ally Mlenge,akizungumza na waandishi wa habari jana.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata majambazi wanane akiwamo mmoja ambaye amebainika kumiliki kiwanda cha kienyeji kinachotengeneza silaha.

Jeshi hilo limemtaja mtuhumiwa anayemiliki kiwanda hicho kuwa ni Charles Masunzu (30), ambaye ni Msukuma na mkazi wa Kawe Mzimuni, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Kamishna wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Ally Mlenge, alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa na silaha mbalimbali ambazo ni rifle tatu, risasi 36, pingu, mitutu mitano iliyotengenezwa kienyeji, Shortgun, mfuko wa kuhifadhia silaha na maganda 17.


Vitu vingine alivyokutwa navyo ni Pistol KJW works, cocking handle za silaha, ‘house’ ya silaha aina ya Greenel, Magazine iliyounganishwa na tiger guard ya silaha ya aina ya riffle, shortgun moja namba 2539 double bore na vikato vitatu vya silaha.

Aidha vifaa vingine ni meza moja yenye vice clamp kwa ajiri ya kutengenezea silaha kienyeji, mikasi minne ya aina tofauti, mipini mitatu ya silaha aina ya riffle, funguo mbalimbali, nyundo, makufuli, misumeno ya kutengeneza vyuma na vielelezo vingine vinavyohusiana na uhalifu.

Mtuhumiwa alikiri kuhusika na matukio mbalimbali ya unyang’anyi na kusababisha mauaji mengi sehemu mbalimbali. Jambazi huyo ameshikiliwa na jeshi la polisi na atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

Aidha, Jeshi la Polisi linawashikilia majambazi wanne waliokutwa na bunduki aina ya SMG iliyosajiliwa kwa namba 02704 ikiwa na risasi 20 ndani ya magazine yake na ikiwa imekatwa kitako.

Baada ya mahojiano na jeshi la polisi, majambazi hao walikiri kujihusisha na matukio ya uporaji na kwamba bunduki hiyo walimpora askari polisi Wilaya ya Rufiji akiwa anasindikiza magari kutoka Ikwiriri Mkoani Pwani mnamo mwaka 2007.

Kadhalika, jeshi hilo lilifanikiwa kumkamata tapeli aliyejulikana kwa jina la Mfaume Omari (29) mkazi wa Magomeni Kagera, aliyekuwa akitumia majina ya viongozi wa serikali, viongozi wa dini na watu maarufu kujipatia fedha kwa kuvaa uhusika wa majina hayo.

Mlenge alisema, baada ya kufuatilia nyendo za mtuhumiwa, jeshi la polisi lilipata taarifa kutoka kwa Mchungaji Getrude Rwakatare kuwa jina lake lilikuwa likitumiwa vibaya na mtuhumiwa huyo. Aidha jeshi la polisi lilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo akiwa anamiliki simu yenye namba 0659 736 454 ikiwa imesajiliwa kwa jina la Mfaume Saidi Omari na 0659 164 744 ikiwa imesajiliwa kwa jina la Alex Mtenga.
 
CHANZO: NIPASHE

2 comments:

Anonymous said...

Kazi ya kupongezwa kwa kuzawadiwa cha maana kutokana na ufanisi wa hali ya juu, hapo mmesha okoa maisha na mali za watanzania kibao. hongereni.

Anonymous said...

Sasa haya ndo mambo tunayo yataka nchiniii kamata wezi woote, majambazi, magaidi na vibaka wooote weka jela. Nchi yetu ilikuwa ya amani sasa wameiharibu kwa maovu mtu unaogopa hata kumtuma mtoto kibandani kununua sabuni ya kufua. Tunaitaka Tanzania yenye amani jamani sio malumbano na mauaji hovyoo.