Advertisements

Wednesday, July 24, 2013

Dk. Mwakyembe awagwaya washirika dawa za kulevya



Katika hali ya kushangaza, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amepata kigugumizi cha kuwachukulia hatua maofisa wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) walioruhusu shehena kubwa ya dawa za kulevya kupita hadi Afrika Kusini.

Ni takribani wiki ya tatu sasa tangu wasichana wawili wa Tanzania walipokamatwa na kilo 150 za dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine zenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 6.8 nchini Afrika Kusini wakati zikisafirishwa kutoka Tanzania.

Jana NIPASHE lilizu ngumza na Dk. Mwakyembe kwa njia ya simu kutoka Kagera, lakini alijibu kwamba, hana taarifa za kina kuhusu sakata hilo.

Hata hivyo, alisema yeye hausiki nalo kwa kuwa suala la uhalifu linaihusu Polisi na kumwelekeza mwandishi awasiliane na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi au Jeshi la Polisi.


Alipoelezwa kwamba, suala hilo linamhusu kwa kuwa ni ngumu kwa kilo 150 za ‘unga’ kupita uwanja wa ndege wenye ukaguzi bila kujulikana, alisema hawezi kuzungumza chochote na kwamba, suala hilo aulizwe Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mhandisi Suleiman Suleiman.

“Sina taarifa za jambo hilo, waulize Polisi au mpigie Waziri wa Mambo ya Ndani. Au muulize Mkurugenzi Mkuu wa Viwanja vya Ndege. Maana mimi siwezi kuwaruka watu walio chini yangu na kufanya maamuzi, ndivyo utaratibu unavyoenda. Kwa hiyo, mtafute Suleiman,” alisema.

Hata alivyoambiwa watendaji walio chini yake wamekuwa wakipiga danadana bila hata kuchukua hatua ya kuwawajibisha walioichafua nchi, alisema: “Hebu kata simu kuna simu inaingia hapa, unajua niko kwenye ziara ya bwana mkubwa huku Bukoba (ziara ya Rais mkoani Kagera).”

Wakati Dk. Mwakyembe akieleza hivyo, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Manumba, amekwepa kuzungumzia sakata hilo na kusema liko kwa Kamanda wa Polisi, Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Geofrey Nzowa.

“Mtafute Kamanda wetu wa kitengo cha dawa za kulevya, mwambie Nzowa azungumze,” alisema. Nzowa alipoulizwa alisema upelelezi bado unaendaelea kubaini mambo mbalimbali yaliyoko nyuma ya tukio hilo. Alipoulizwa ikiwa Polisi wamebaini mmiliki pamoja na maofisa walioruhusu kupitishwa kwa dawa, Nzowa alisema uchunguzi unaangalia mambo mengi na ndiyo huo utakuja na taarifa kamili.

 Kamanda Nzowa alisema tukio hilo ni kubwa na ndiyo maana taarifa za uchunguzi huo haziwezi kutolewa haraka.

Alisema pamoja na uchunguzi huo unaoendelea kufanyika hapa nchini, pia unaendelea na nchini Afrika Kusini.

Wiki iliyopita NIPASHE lilimtafuta Nzowa pamoja na Kamanda wa Polisi Kikosi cha Viwanja vya Ndege Nchini, Deusdedit Kato, kufahamu uchunguzi umefikia wapi juu ya tukio hilo, lakini walisema upelelezi haujakamilika.

Kwa upande wake, Nzowa alisema upelelezi wa tukio hilo ni mkubwa, hivyo taarifa za uchunguzi zisingeweza kutolewa wiki iliyopita wala wiki hii, huku Kato akisema kwamba, umefikia katika hatua nzuri na ukikamilika watatoa taarifa.

Taarifa za kukamatwa kwa wasichana hao nchini Afrika Kusini zilipatikana Julai 5, mwaka huu.   Walikamatwa na maofisa wa Mamlaka ya Mapato ya nchi hiyo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo, uliopo eneo la Kempton Park.

 Taarifa hiyo ilionyesha wasichana hao walisafirisha dawa hizo kupitia ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini.

Waliokamatwa hivi karibuni ni Agnes Jerald (25), Melisa Edward (24), ambao wameshtakiwa Afrika Kusini.

Hata hivyo, kigugumizi cha viongozi hawa na hususan cha Waziri Mwakyembe, kinaibua maswali mengi, ambayo yanaashiria kwamba, biashara haramu ya dawa za kulevya itakuwa inahusisha mtandao wa watu wenye nguvu nchini.

Itakumbukwa kwamba, ni Mwakyembe huyu huyu, ambaye aliifumua Mamlaka ya Bandari (TPA), kwa kuwatimua kazi wakurugenzi wakuu pamoja na kutengua uteuzi wa wajumbe wa bodi ya wakurugenzi kutokana na utendaji usio na tija na hasa baada ya kutokea kwa wizi wa shaba bandarini.
Wizi huo ulitokea usiku wa kuamkia Septemba 8, mwaka jana jambo, ambalo lilimkasirisha Waziri Mwakyembe.

Alifanya ziara bandarini hapo na kuagiza watu wote waliohusika na wizi huo kukamatwa na kufunguliwa mashitaka.

Pia Juni 12, mwaka jana,  Mwakyembe baada ya kuwang’oa vigogo wanne wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), alisafiri kwa treni kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ili kujionea utendaji kazi wa shirika hilo.  Mara baada ya kuwasili katika Stesheni ya Dodoma saa 1:30 asubuhi,  alizungumza na waandishi wa habari na kusema akiwa katika safari hiyo, alipata fursa za kutembelea mabehewa yote na kuzungumza na abiria. Alisema alibaini hujuma nzito katika Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), ikiwamo ofisa mmoja kuwaibia abiria kwa kughushi viwango vya nauli na hivyo akaagiza afukuzwe kazi.

Licha ya kuagiza kutimuliwa kwa ofisa huyo, pia alitangaza kuandaliwa utaratibu wa kufanya mabadiliko kadhaa katika kuboresha usafiri huo, ikiwamo kuondoa malipo ya nusu nauli kwa watoto wadogo kuanzia miaka mitatu hadi miaka 10 na pia kuondolewa kwa utaratibu wa malipo ya mizigo midogo ya abiria.

Takwimu zinaonyesha kumekuwa na wimbi kubwa la Watanzania wanaojiingiza katika biashara haramu ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi na kwamba, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, watuhumiwa 10,799 walikamatwa kwa kujihusisha na dawa hizo.

Katika kipindi hicho, Watanzania 240 walikamatwa katika nchi za Brazil, Pakistan na Afrika Kusini, kuharibu taswira ya nchi na kusababisha Watanzania wasio na hatia kupata usumbufu na masharti magumu wanapotaka kusafiri kwenda nchi mbalimbali duniani.
 
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Ndugu zangu WaTanzania. Biashara ya madawa ya kulevya katika nchi yetu ina historia ndefu na hii habari ya kukamatwa kwa wabebaji au mitambo ya kuziandaa(kutengeneza) tumeshazisikia sana tena kwa miaka mingi na cha "kufurahisha" uchunguzi wa kina bado unaendelea na taarifa "zitatolewa" utakapokamilika. Ninachoona mimi ni kuwa kuna uwezekano mkubwa sana kwa WAKUBWA kuhusika na ndiyo maana inakuwa vigumu kulifikisha suala hili mwisho na watuhumiwa kuhukumiwa. Inawezekana pia baada ya kukamata shehena hasa ndani ya nchi, dawa hizo huhifadhiwa na kisha kesi ikipoa wananchi hatujulishwi kesi ilipoishia na hata madawa yenyewe hayajulikani yalikohifadhiwa maana hatuoni yakiharibiwa.Hebu tuone hili la sasa kama litatoa matokeo tofauti maana kilo 150 ni mzigo mkubwa na wabebaji wamekamatwa, kinachorefusha uchunguzi ni nini. Ukweli upo palepale kuwa waliokamatwa ni "Containers" tuu wamiliki ni akina NANI?? ugumu uko wapi kupata waliko?? waulizwe hao akina dada!!!

I WAS JUST SAYING!!!