ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, July 2, 2013

HARUFU MBAYA SEHEMU ZA SIRI (VAGINOSIS) - 2



WIKI iliyopita tulijadili tatizo linalowasumbua wanawake wengi nalo ni la kutokwa na uchafu unaotoa harufu mbaya sehemu za siri.
Tukasema kitaalamu hali ya mwanamke kutokwa na majimaji yenye rangi nyeupe au ya njano, ni hali ya kawaida na wala siyo tatizo endapo majimaji hayo siyo mazito sana na wala hayatoi harufu mbaya.
Ila majimaji yanayotoka yakiwa katika hali ya ute mzito wenye rangi nyeupe au kahawia na yakiwa yanatoa harufu mbaya na yanawasha, basi hiyo ni ishara ya ugonjwa uitwao Vaginosis.
Tulieleza mengi na tukataja na sababu za kitaalamu kuwa imegundulika kwamba kuna sababu nyingi ambazo husababisha mwanamke kutoa ute au majimaji yasiyo ya kawaida kwenye sehemu zake za siri.
Leo tutaeleza dalili kisha tutaeleza vipimo na tiba ya maradhi haya ya kike katika jamii yetu.

DALILI
Wanawake wenye tatizo la Vaginosis huwa na dalili kubwa ya kutokwa na
uchafu usiyo wa kawaida kutoka sehemu za siri. Uchafu huu huwa unatoa harufu kali kama shombo ya samaki au kitu kilichooza na huambatana na maumivu makali ya tumbo chini ya kitovu.
Wakati mwingine uchafu wenye rangi kama ya kijani hutoka,kuwashwa sana sehemu za siri, mgonjwa asipopatiwa tiba haraka husababisha vidonda sehemu za siri kwa sababu ya kujikuna kutokana na mwasho anaoupata.
Kuna wakati mwingine mwanamke anatokwa na ute uliochanganyikana na damu hata kama hayupo kwenye siku zake, hii ni dalili nyingine ya Vaginosis. Mgonjwa pia anaweza kusikia maumivu makali wakati wa tendo la ndoa, hali ambayo pia inaweza kusababishwa na kuingiwa kwa bakteria katika mji wa uzazi.
Bakteria hao huweza kusababisha siyo harufu tu, bali mgonjwa anaweza kutokwa na usaha sehemu hiyo ya siri.

MATIBABU
Tatizo hili hutibika hospitalini baada ya vipimo vya kitaalamu kuchukuliwa na mtaalamu mwenye uzoefu wa kutosha juu ya magonjwa ya wanawake. Daktari anaweza kumpa mgonjwa dawa za kupaka na dawa za kumeza ambazo huweza kumaliza tatizo hili.

USHAURI
Mara nyingi nashauri kuwa ni makosa kutumia dawa bila kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa daktari aliye na ujuzi wa magonjwa hayo na siyo kupewa dawa na wauzaji wa maduka ya dawa.
Nasema hivyo kwa sababu watu wengi wana kawaida kwenda kwenye duka la dawa na kupewa dawa na muuzaji bila kupimwa. Kumbuka unaweza kupewa dawa ambayo siyo ya ugonjwa wako.
Nawashauri pia wale wanawake wenye kawaida ya kutumia pafyumu au kuweka dawa sehemu za siri kwa lengo la kuzifanya kuwa ndogo, waache kufanya hivyo kwani madhara yake ni makubwa sana kiafya likiwemo hilo la kutoa harufu mbaya sehemu hizo na zinaweza kusababisha madhara makubwa katika njia ya uzazi. GPL

No comments: