Lengo:
Hili ni jukwaa ambapo wataalamu, wakereketwa na
wafurukutwa wa Kiswahili - kupitia Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (chaUKIDU: www.chaukidu.org ) chenye makao makuu yake
nchini Marekani – watawaleteeni makala au
mijadala mifupi ya uchokonozi kuhusu masuala anuai ya Kiswahili kama vile
ukuaji wa msamiati, aina za msamiati, mikanganyiko na mikengeuko ya kisarufi na
hata ya kitahajia, miktadha ya mawasiliano na athari zake katika matumizi ya
lugha, sera za lugha, Kiswanglish, nk. nk. Lengo ni kuwa na jukwaa shirikishi
katika ukuzaji na uendelezaji wa lugha yetu pendwa. Jivunie Kiswahili
makala – 1 [8/2/13]
:
Kama mgeni rasmi katika sherehe za kuadhimisha miaka
miatatu ya blogu ya VIJIMAMBO na Tamasha la Kiswahili lililofanyika huko
Capitol Heights, MD nchini Marekani tarehe 6 Julai, 2013, Mhe Ali Hassan Mwinyi
(Rais Mstaafu, JMT, Awamu ya Pili) alisisitiza katika risala yake haja ya kila
mtumiaji wa Kiswahili kuwa mhifadhi na mlinzi mwaminifu wa Kiswahili kwa
kuzingatia matumizi yake sahihi. Dhana ya ‘usahihi’ wa lugha ni pana na tata.
Kwa minajili ya kufungua rasmi jukwaa hili na kwa heshima ya Mhe Ali Hassan
Mwinyi, ebu tuangalie na kutafakari juu ya baadhi ya mifano aliyotumia katika
risala hiyo akibainisha matumizi sahihi na yasiokuwa sahihi:
sahihi
|
sio sahihi
|
Mifano hai (imepatikana
kwa ku-google)
|
upungufu
|
mapungufu
|
CUF yabainisha mapungufu
ya rasimu ya katiba (www.cuf.or.tz )
|
uamuzi
|
maamuzi
|
Lowassa:
taifa stars fanyeni maamuzi magumu
muwape raha Watanzania (http://www.mjengwablog.com/michezo/ )
|
uhusiano
|
mahusiano
|
Forum: mahusiano,
mapenzi, urafiki (http://www.jamiiforums.com/mahusiano-mapenzi-urafiki/
)
|
ushirikiano
|
mashirikiano
|
Jamhuri
ya Kiislamu ya Iran na Oman zikiwa ni nchi mbili muhimu na zenye kuleta
athari chanya katika masuala ya kiusalama katika eneo la Ghuba ya Uajemi,
daima zimekuwa zikiimarisha na kustawisha mashirikiano yao katika nyanja zote (http://kiswahili.irib.ir/uchambuzi/ )
|
hesabu
|
mahesabu
|
Ripoti na
Taarifa za Mahesabu (http://kiswahili.daraja.org/accountability/ )
|
mwendo wa saa nane
|
mwendo wa masaa nane
|
Natoka Arusha kwenda Singida kwa barabara hii mpya, ni
mwendo wa masaa 3 tu. (https://twitter.com/tonytogolani/status
)
|
USIKOSE KUANZIA KESHO IJUMAA AUG 2, 2013 NA KILA SIKU YA IJUMAA
5 comments:
Safi sana mdau.
Mimi sikubaliani na hayo maneno yanayosemwa sio sahihi.
Maneno yalioitwa "SIO SAHIHI" ni sahihi bali ni wingi (plural)wake.
Mfano:
1. uamuzi = decision
maamuzi = decisions
2. upungufu = shortcoming
mapungufu = shortcomings
Nimelazimika kuchungulia Kamusi ya Kiswahili Sanifu (TUKI, 2004) na Kamusi la Kiswahili Fasaha (BAKIZA, 2010) zote zinakubaliana - yaani zimeorodhesha maneno 'uamuzi' na 'upungufu' kama nomino (nm) ambazo hazina wingi!
Sina tatizo na matumizi ya neno 'maamuzi' na ninafikiri nimeishalitumia mara kadhaa. Hoja yangu ni kwamba kuna uwezekano Kiswahili cha'kamusi' hubakia hatua kadhaa nyuma na 'matumizi' ya wakati uliopo, na wale wahifadhina wa lugha kama Mzee A.H. Mwinyi wanajikuta wamefungwa pingu na Kiswahili cha kamusi au wao wanafunga Kamusi pingu na Kiswahili kisichobadilika!!!
Nilisoma na kutohoa lugha hii kwa miaka miwili. Labda wadau tujue upana wa maeneo ya lugha na kila eneo linavyotamkwa au kutamkwa. Kuna utamkaji usio rasmi ( usio wa kisarufi au fasihi au ulio nje ya kamusi) kwa mfano sentesi hii "mjomba amenipa bonge ya zawadi" hapo alitakiwa kusema mjomba amenipatia zawadi kubwa. Wapo wanaoongea nje ya muktadha hao ndio wanaharibu lugha. Hapo ndipo panazaa lugha za mitaani, lugha za uswahilini na lugha mchanyato (mixed laguage in linguitic ). Wataalamu kazi kwenu
ni "siyo sahihi" NOT "sio sahihi" au?
Post a Comment