ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, August 1, 2013

Jumuika na chaUKIDU, jivunie Kiswahili KILA SIKU YA IJUMAA

Lengo:
Hili ni jukwaa ambapo wataalamu, wakereketwa na wafurukutwa  wa Kiswahili - kupitia Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (chaUKIDU: www.chaukidu.org ) chenye makao makuu yake nchini Marekani – watawaleteeni  makala au mijadala mifupi ya uchokonozi kuhusu masuala anuai ya Kiswahili kama vile ukuaji wa msamiati, aina za msamiati, mikanganyiko na mikengeuko ya kisarufi na hata ya kitahajia, miktadha ya mawasiliano na athari zake katika matumizi ya lugha, sera za lugha, Kiswanglish, nk. nk. Lengo ni kuwa na jukwaa shirikishi katika ukuzaji na uendelezaji wa lugha yetu pendwa. Jivunie Kiswahili

makala – 1 [8/2/13] :
Kama mgeni rasmi katika sherehe za kuadhimisha miaka miatatu ya blogu ya VIJIMAMBO na Tamasha la Kiswahili lililofanyika huko Capitol Heights, MD nchini Marekani tarehe 6 Julai, 2013, Mhe Ali Hassan Mwinyi (Rais Mstaafu, JMT, Awamu ya Pili) alisisitiza katika risala yake haja ya kila mtumiaji wa Kiswahili kuwa mhifadhi na mlinzi mwaminifu wa Kiswahili kwa kuzingatia matumizi yake sahihi. Dhana ya ‘usahihi’ wa lugha ni pana na tata. Kwa minajili ya kufungua rasmi jukwaa hili na kwa heshima ya Mhe Ali Hassan Mwinyi, ebu tuangalie na kutafakari juu ya baadhi ya mifano aliyotumia katika risala hiyo akibainisha matumizi sahihi na yasiokuwa sahihi:



sahihi
sio sahihi
Mifano hai (imepatikana kwa ku-google)
upungufu

mapungufu

CUF yabainisha mapungufu ya rasimu ya katiba (www.cuf.or.tz )
uamuzi
maamuzi
Lowassa: taifa stars fanyeni maamuzi magumu muwape raha Watanzania (http://www.mjengwablog.com/michezo/ )
uhusiano
mahusiano
Forum: mahusiano, mapenzi, urafiki (http://www.jamiiforums.com/mahusiano-mapenzi-urafiki/ )
ushirikiano
mashirikiano
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Oman zikiwa ni nchi mbili muhimu na zenye kuleta athari chanya katika masuala ya kiusalama katika eneo la Ghuba ya Uajemi, daima zimekuwa zikiimarisha na kustawisha mashirikiano yao katika nyanja zote (http://kiswahili.irib.ir/uchambuzi/ )

hesabu

mahesabu
Ripoti na Taarifa za Mahesabu (http://kiswahili.daraja.org/accountability/ )

mwendo wa saa nane

mwendo wa masaa nane
Natoka Arusha kwenda Singida kwa barabara hii mpya, ni mwendo wa masaa 3 tu. (https://twitter.com/tonytogolani/status )

USIKOSE KUANZIA KESHO IJUMAA  AUG 2, 2013 NA KILA SIKU YA IJUMAA

5 comments:

Anonymous said...

Safi sana mdau.

Anonymous said...

Mimi sikubaliani na hayo maneno yanayosemwa sio sahihi.

Maneno yalioitwa "SIO SAHIHI" ni sahihi bali ni wingi (plural)wake.

Mfano:
1. uamuzi = decision
maamuzi = decisions

2. upungufu = shortcoming
mapungufu = shortcomings

Anonymous said...

Nimelazimika kuchungulia Kamusi ya Kiswahili Sanifu (TUKI, 2004) na Kamusi la Kiswahili Fasaha (BAKIZA, 2010) zote zinakubaliana - yaani zimeorodhesha maneno 'uamuzi' na 'upungufu' kama nomino (nm) ambazo hazina wingi!
Sina tatizo na matumizi ya neno 'maamuzi' na ninafikiri nimeishalitumia mara kadhaa. Hoja yangu ni kwamba kuna uwezekano Kiswahili cha'kamusi' hubakia hatua kadhaa nyuma na 'matumizi' ya wakati uliopo, na wale wahifadhina wa lugha kama Mzee A.H. Mwinyi wanajikuta wamefungwa pingu na Kiswahili cha kamusi au wao wanafunga Kamusi pingu na Kiswahili kisichobadilika!!!

Anonymous said...

Nilisoma na kutohoa lugha hii kwa miaka miwili. Labda wadau tujue upana wa maeneo ya lugha na kila eneo linavyotamkwa au kutamkwa. Kuna utamkaji usio rasmi ( usio wa kisarufi au fasihi au ulio nje ya kamusi) kwa mfano sentesi hii "mjomba amenipa bonge ya zawadi" hapo alitakiwa kusema mjomba amenipatia zawadi kubwa. Wapo wanaoongea nje ya muktadha hao ndio wanaharibu lugha. Hapo ndipo panazaa lugha za mitaani, lugha za uswahilini na lugha mchanyato (mixed laguage in linguitic ). Wataalamu kazi kwenu

Anonymous said...

ni "siyo sahihi" NOT "sio sahihi" au?