
Kila mmoja kuna yanayomtokea lakini anachokifanya ni kuvumilia. Wapo wanaotendwa na wapenzi wao lakini wanafanya siri wakiamini ipo siku yatapita.
Lakini pia wapo ambao kulia ndiyo maisha yao ya kila siku, wanafanyiwa visa vya ajabu na watu waliotokea kuwapenda kinyume na matarajio yao.
Katika hili naomba niseme tu kwamba, kwanza ulimwengu wa sasa wa mapenzi umetawaliwa na usanii mwingi na ndiyo maana naweza kusema wengi wetu tumetamaniwa tu na wapenzi wetu na wala hatujapendwa.
Unaweza kukutana na mtu akakueleza hisia zake kwamba anakupenda sana na hayuko tayari kukukosa katika maisha yake lakini kumbe hana lolote, amekutamani tu.
Hivi unajua kuna kupendwa na kutamaniwa? Hivi unatambua kwamba wanaume wengi siyo kwamba wanawapenda kwa dhati wale walio nao bali wamewatamani tu kutokana na mvuto wa kimapenzi walio nao?
Kama ulikuwa hujui, huo ndiyo ukweli wenyewe na nasema hivyo baada ya kufanya utafiti kuhusu hilo. Unaweza kumkuta mvulana anakutana na msichana mrembo kisha kumtamkia wazi kwamba eti amemzimikia.
Hivi hujawahi kumsikia mtu anamtongoza msichana kwa kumwambia, ‘Anti nimetokea kukupenda ghafla, ningependa uwe mpenzi wangu’. Ni sawa unaweza kutokea kuvutiwa na mtu baada ya kukutana naye kwa mara ya kwanza lakini utafiti unaonesha wengi wetu tumekuwa tukiwatamani tu baadhi ya watu na sio kwamba tunakuwa na mapenzi ya dhati kwao.
Ni wazi wanaume wanapotokea kukutana na wanawake wenye makalio makubwa, vifua vizuri, macho yenye mvuto, ni wachache watakaovumilia kupishana nao bila kuwaangalia zaidi ya mara moja.
Wengine hawaishii kuwaangalia tu bali hudiriki kuwatamkia kwamba wamewazimikia ila kudhihirisha hawajawapenda kwa dhati, utakuta watakapokubaliwa na kufanya mapenzi mara moja ama mbili huachana nao. Hii inaonesha sio kwamba wamewapenda bali wamewatamani.
Kimsingi wapo wanawake wazuri tu ambao wameingia katika mapenzi yasiyo ya kweli kutokana na kutamaniwa. Utakuta mapenzi yao hayana muda mrefu lakini migongano ya hapa na pale haiishi ikiwa ni pamoja na kusalitiana.
Mwanamke atajuaje kwamba ametamaniwa na sio kwamba amependwa? Ni rahisi sana kugundua kwa sababu mapenzi ya dhati siku zote hayajifichi.
Mwanaume anapomtamkia mwanamke kwamba amempenda mara baada ya kukutana kwa mara ya kwanza kisha muda mfupi akataka kufanya mapenzi, huyo atakuwa hana mapenzi ya kweli na kama mwanamke atamkubalia eti kwa sababu naye amempenda ama naye amemtamani kwa jinsi alivyo, basi watakuwa wameingia katika penzi la muda.
Kikubwa ni kuwa makini na mtu anayekutokea na kukuambia kakupenda. Usikurupuke kumpa nafasi kwenye moyo wako kabla hujamfanyia utafiti. Ukifanya hivyo, tarajia penzi lenye ‘makengeza’.
Kumbuka walio wengi sasa hivi wako katika mapenzi ya muda na wengine wameingia kwenye ndoa za muda kwa kuwa hawajapendana kwa dhati ila wametamaniana na ndiyo maana kila siku unasikia watu ambao hawana muda mrefu kwenye uhusiano wameachana.
Kwa kuongezea ni kwamba ukitaka kujua mpenzi ambaye hajakupenda bali amekutamani wasiliana na mimi kwa namba za simu hapo juu.
Niishie hapo kwa leo, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine ila nichukue nafasi hii kuwatakia Waislam wote mfungo mwema wa Ramadhani.
GPL
2 comments:
Asante kwa maneno ya kutujenga akili hasa sisi akina dada tunaotaka kuolewa.
wanaume wote wasanii tu haswa mwana fulani yeye kila mwanamke akikutana naye anatangaza ndoa
Post a Comment