
Range (kushoto) akifanya mazoezi ya uashi katika banda la Veta huku baba yake (Jackson) akimwangalia.
Range Jackson anaonekana kwenye banda la maonyesho la Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) kwenye Viwanja vya Sabasaba , Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Anaonekana kama fundi mahiri kwa jinsi anavyofanya kazi kwa bidii. Hata hivyo, Range mwenye umri wa miaka 18 ana historia ndefu ya matatizo ya akili.
Baba yake mzazi, Jackson Range ambaye ni mfanyabiashara, ameachana na biashara na kurudi darasani kwa masomo ya ufundi.
Ni nini kimemsibu mzazi huyo hadi kurudi darasa la ukubwani? Yeye anajibu kuwa ni kuwa karibu na mwanaye, walau apate ujuzi wa kumsaidia kimaisha.
“Nina watoto sita na huyu ni wa pili. Hata hivyo, tangu azaliwe, hajaweza kupata elimu rasmi kutokana na matatizo ya kiakili.
Niligundua tatizo lake nilipowaanzisha shule ya awali yeye na dada yake ambaye sasa amemaliza kidato cha sita,” anasema Jackson na kuongeza:
“Alikuwa na utukutu uliopita kiasi. Awali, nilidhani ni utoto, lakini baadaye niliona anashindwa kabisa kuendelea na masomo.”
Mzazi huyo anasema wakati huo walikuwa wakiishi Morogoro, aliamua kumpeleka hospitali baada ya kushauriwa na wataalamu ya afya.
“Nilishawishiwa na muuguzi mmoja kumpeleka hospitali ili apimwe, wakati huo akiwa na miaka miwili na nusu. Kule hospitalini walimpima kama kwa ‘x-ray’ kama ubongo wake unaathari lakini hawakuona tatizo lolote, wakanipa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam ambapo alipelekwa wodi ya wagonjwa wa akili na kuanzishiwa dozi ya kutuliza akili,” anasema na kuongeza:
“Dawa alizopewa zilikuwa zinampa usingizi mzito, hivyo akawa analala na ilifika mahali akazizoea dawa, hivyo akizikosa anasumbuka.”
Anaendelea kusema kuwa alilazimika kumwona daktari bingwa anayemkumbuka kwa jina la Profesa Kilonzo (Gadi Paul) na kumwomba ambadilishie dawa.
“Profesa Kilonzo alisema kuwa hizo dawa za kumtuliza, hivyo nina hiari ya kumpa au kutompa. Kuna siku niliamua kutumia zile dawa name nikalala kupita kiasi. Nikaamua kumwondoa hospitali na kumpeleka kijijini kwetu, Nyamongo wilayani Tarime, Mkoa wa Mara,” anasema.
Anasema walipofika kijijini kwao aliwakabidhi wazazi wake ili wamtibu kwa njia za kienyeji, ambazo nazo pia hazikufaulu.
“Baada ya wazazi kuhangaika naye, nao wakashindwa, wakaniambia tu nirudi kanisani nimwombe Mungu.
Hapo niliwaza sana, kisha nikaamua kwenda kutafuta tiba Nairobi, Kenya, hiyo ilikuwa mwaka 2001,” anasema na kuongeza:
“Nilimpeleka Kituo cha Epren Academy Ltd kilichopo Nairobi ambako alipimwa na nikaambiwa kuwa ana tatizo la utukutu uliopita kiasi na kwamba hawezi kutulia ili kusoma. Nikaambiwa kuwa tatizo hilo linaitwa kitaalamu, hyperactive and destructive disorder.
Wao walinishauri nimpeleke Hospitali ya Aga Khan huko huko Nairobi ambako nako alipimwa na kuwa matibabu.”
Baada ya matibabu hayo, Jackson anasema alimtafutia shule huko huko Kenya, lakini Wizara ya Elimu ilimtaka awe na uthibitisho wa uraia wa Kenya, jambo ambalo lilimshinda.
“Niliporudi Dar es Salaam sikufanikiwa kupata shule inayomfaa kwani kuna Shule ya Uhuru Mchanganyiko inahudumia walemavu wa macho, wasiosikia na Shule ya Jeshi la Wokovu (Salvation Army) inahudumia walemavu wa viungo. Nikampeleka Shule ya Msingi Msimbazi, lakini walimu walishindwa kummudu kwani wakati wenzake wakiwa wapole, yeye alikuwa mtukutu,”
“Nilimpeleka Shule ya Sabasaba ambako iliwabidi kuajiri mtu wa kushinda naye, mwisho wakashindwa ndipo nikampeleka kwenye Shule ya Euris iliyoko Mbagala Zakhem, nako wakashindwa.”
Anaendelea kusimulia kuwa, mwaka 2003 kuna jirani yake anayeishi Mbagala alianzisha shule ya watoto wenye mahitaji maalumu, hivyo akamchukua Range ili amsaidie.
“Kuna siku alitoroka shule akaenda dukani na kuchanganya sukari na mchele, mwenye duka akakasirika na kumpiga na fimbo kichwani.
Anasema mtoto wake (Range) alilia kwa sauti kali, hadi jirani yake aliposikia na kwenda dukani ambako alipata mshtuko na kuanguka kwa alichokiona,” anasema Jackson na kuongeza:
“Baada ya hapo tukamwachisha shule na kuanza kumfungia ndani. Hapo nyumbani tunafuga ng’ombe, kwa hiyo alizoeana na mlisha ng’ombe wetu. Siku mlishaji huyo alipoacha kazi na kuondoka, Range alimtafuta hadi akapotea.”
Anasema kabla ya hapo, alikwenda kuomba ushauri katika Shirika la Haki Elimu ambako alishauriwa kusoma ualimu ya awali.
“Mwaka 2002 nilijiunga na Chuo cha Montesori, Dar es Salaam ili nipate ujuzi wa kumsaidia mwanangu, hata hivyo kabla sijaanza chuo nikapata ajali na kuvunjika mkono.
Hivyo, niliahirisha masomo hadi mwaka 2007, niliporudi na kusoma. Baada ya miezi sita nikapata ujuzi wa kumfundisha Range kusoma na kundika, akaweza ndipo nilipompeleka Shule ya Tuleane iliyopo Chang’ombe,” anasema.
Hata huko mzazi huyo anasema walimshindwa, hivyo akaenda kwa Ofisa Elimu, Manispaa ya Temeke ambaye alimshauri amwanzishe shule kwa walioikosa (Memkwa).
“Mwaka 2011 nilimwanzisha darasa la Memkwa katika Shule ya Msingi Mbagala, lakini mwalimu wake alisema kuwa alilazimika kutumia zaidi ya asilimia 75 ya muda wote kumfundisha yeye tu, hivyo nao wakamshindwa,” anasema.
Hata hivyo, anasema alipata taarifa ya kuwepo kwa chuo cha ufundi wilayani Kisarawe Mkoa wa Pwani, lakini alipompeleka hakudumu kwani chuo hicho hakikuwa na ulinzi hasa wakati wa usiku.
Alivyotua Veta
Mzazi huyo anasema baada ya mahangaiko ya muda mrefu, alikwenda kuomba Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta), Chang’ombe ambako aliwaomba wamtengenezee kozi maalumu kwa ajili ya mwanaye. Kozi hiyo inahusu kutengeneza bidhaa za vyuma.
“Niliamua kuuza gari langu ili kugharimia matayarisho ya kozi hiyo kiasi cha Sh4 milioni. Kozi hiyo iliunganishwa kwenye watu wenye mahitaji maalumu wakiwemo waathirika wa dawa za kulevya, wasiosikia na bubu,” anasema.
Hata hivyo, Veta walimtaka alete mtu wa karibu wa kumsaidia Range anapokuwa shule. Hivyo, yeye mwenyewe aliamua kuacha biashara na kujiunga na masomo hayo tangu mwaka 2012.
“Nilifanya hivyo nikitambua kuwa mwanangu ana thamani kuliko biashara zangu, nimeona bora nisome naye ili nimsadie kwa kila anachohitaji,” anasema.
Mwananchi
2 comments:
Mzee, Pole sana sana ndugu yangu, uamuzi wako ni wa kupongezwa sana sana.
Hata hivyo unahitaji SUPPORT GROUP, tafadhari sana wasiliana nami kwa e-mail yangu binafsi ili tuendelee kuwasiliana na kukupa nguvu. Ninaelewa sana ychungu ulio nao.
Niko hapa: Projectlync@gmail.com.
Pole sana.
Maselle.
kweli wakale walisema uchungu wa mwana ajua mzazi hakika huyu baba anampenda sana mwanae huu ni mfano mzuri wakuigwa na kila mzazi nimesoma hii habari ni kama movie vile baba hajakata tamaa na changamoto zooote big up baba Mungu atakusaidia na mtoto wako atakuwa sawa pia usipuuzie maombi pamoja na kumsurpport pia mshirikishe Mungu kwani hakuna linalomshinda
Post a Comment