ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, July 9, 2013

WAJUE WANAWAKE NA UHUSIKA WAO KATIKA MAPENZI


TUMSHUKURU Mungu kwa yote ambayo sisi tunayaona na mengine yaliyo juu ya upeo wetu wa macho. Mzigo wa maisha umejaa changamoto nyingi, Mwenyezi Mungu anatulinda kila nukta, lakini hata kama hujui hilo, basi pumzi ya uhai ikupe sababu ya kuamini kudura za Maulana.

Kwa uwezo niliojaliwa na Mola Mpaji, leo nachambua mada inayohusu makundi ya wanawake na mitazamo juu ya wanaume. Ninachozingatia hapa ni fikra, katika makundi ambayo niyachambua hapa, vigezo vyao kwa wanaume vipo kimtazamo zaidi.
Fikra zao ndiyo zimetengeneza mtazamo kwa namna ambavyo wao wamepima masilahi yao kwa wanaume. Maisha yanavyosogea mbele ndivyo binadamu wanavyojihisi wana akili na maarifa zaidi. Sasa wanajiona wana uwanja mpana zaidi wa kuchanganua, kuchambua na kuchagua.
Wakati miaka ya nyuma kila mwanamke ndoto yake kuu ilikuwa kuolewa ili apate mume wa kutulia naye, hivi sasa mambo yamebadilika. Makundi ni mengi, hata hilo ambalo linaundwa na wale wanaoteswa na kupata waume lipo lakini halitambi, linabezwa.
Sababu ya kundi hilo kubezwa ni mtazamo uliopo kwenye makundi mengine mawili kuwa watu wanaoota kupata wanaume wa kuwaoa, mawazo yao ni ya kale. Kwamba hayajitoshelezi kwa kizazi cha sasa ambacho kimeegemea teknolojia na utandawazi.
Tamaa ya fedha na kupanuka kwa sanaa, video kuwaonesha mastaa wa Marekani na Ulaya pamoja na mitindo yao ya maisha, kumechangia kwa kiasi kikubwa kuwafanya baadhi ya wanawake kutengeneza mitazamo yao ya kupenda.

KUNDI LA KWANZA
Mara nyingi linaundwa na wasichana wadogo na hata wanawake wakubwa wenye fikra ambazo ni rahisi kuziita changa. Hawa hupenda wanaume kutokana na muonekano wao. Inawezekana ikawa ni mtindo wa mavazi au umbile lake.
Katika kundi hili, ni rahisi kukuta mwanamke ameangukia kwa mwanaume asiye na malengo yoyote ya maisha. Matokeo yake, mwanamke huyo ndiye anageuka mlezi wa mwanaume husika, akimhudumia kila kitu.
Mathalan, anavutiwa na urefu, atafanya juu chini mpaka ahakikishe amemtia kwenye himaya yake. Hata kama hana ujasiri wa kusimama mbele ya mwanaume na kuwasilisha hisia za moyo wake lakini namna atakavyokuwa anaonesha kupagawa, itatosha kufikisha ujumbe.
Inawezekana pia ikawa kwa umbo lake lililojengeka kimazoezi. Ipo mifano ya mabaunsa wengi tu mjini ambao kimuonekano tu, ipo wazi kuwa wana nguvu za kutosha ambazo wangezitumia katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali. Ajabu ni kuwa misuli na nguvu zao hazina faida, kwani wanalelewa tu na wanawake.
Hata mavazi, jinsi mwanaume anavyobadili mavazi, inaweza kumsababishia mwanamke kuingia kichwakichwa. Sura nayo ni kielelezo pamoja na sifa nyingine ambazo huonekana wazi katika mwili wa binadamu. Ongezea rangi, mpangilio wa meno, anaweza kupenda mwanya tu!
Yupo mwanamke ambaye anaweza kudondoka kwenye penzi kwa sababu mwanaume mwenyewe huwa anavaa miwani. Eti namna ambavyo ile miwani inamtoa, kwake hoi. Hata utembeaji na mikogo yake, sauti na jinsi mtu anavyoongea, vinaweza kushawishi wanawake ndani ya kundi hili.
Kimsingi, wanawake ndani ya kundi hili, huvutiwa kimapenzi kwa wanaume kutokana na muonekano wao au msemo wa kisasa ni kuwa swaga za mtu ndizo ambazo zinaweza kumpa alama ya kupendwa au kupotezewa.

TATHMINI KIMAPENZI
Wanawake wa kundi hili huwa na rangi mbili. Ya kwanza ni kwamba wanazo alama nyingi za kupenda. Anapompata yule anayemmulika, humpa mapenzi yote na kila kitu ambacho mwanaume atakuwa anakihitaji.
Rangi ya pili ni kuwa kama mwanamke mwenyewe ni mapepe, basi anaweza kuhamisha upendo kutoka kwa mwanaume mmoja hadi mwingine. Kama alimpendea urefu, warefu wapo wengi, ikiwa ni mavazi, wavaaji wamejaa kila kona, vivyo hivyo kwa sifa nyinginezo.
Mwanaume anapaswa kutathmini mwanamke wake yupo vipi. Utulivu wake unaweza kuwa kichocheo cha penzi la kudumu, umapepe ni kielelezo hatarishi katika uaminifu.
Ukweli ni kwamba wale watulivu huwa na mapenzi ya kweli lakini kasoro yake ni kuwa dunia inageuka, kama alikupendea gari, kuna siku unaweza usiwe nalo, hapo atakuacha. Kama ni sura, basi unaweza kupata ajali, ile ‘baby face’ iliyomvuta haitakuwepo tena.

Itaendelea wiki ijayo.

Global Publishers

No comments: