ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 31, 2013

DAWA ZA KULEVYA: Kingunge 'amvaa' Lukuvi

  Ataka serikali iwataje vinara wanaohusika
  Awashukia pia walioficha mabilioni Uswisi
Mkongwe wa siasa za Tanzania, Mzee Kingunge Ngombale-Mwiru (Kushoto) akihoji kauli ya serikali juu ya vigogo kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya iliyotolewa hivi karibuni na Waziri wa nchi ofisi ya waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) William Lukuvi (kulia). Picha na Atuza Nkurlu

Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru amejitosa katika sakata la dawa za kulevya, akiinyoshea kidole serikali itaje majina ya watuhumiwa.

Tamko la Kingunge limekuja takriban siku tatu, baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, kuliambia Bunge kwamba, miongoni mwa watuhumiwa wa dawa za kulevya ni wabunge.

Hata hivyo, Lukuvi, alisema serikali haiwezi kuyatangaza majina hayo hadharani, isipokuwa hadi itakapojiridhisha kwa ushahidi na kuwafikisha (watuhumiwa) kwenye vyombo vya sheria.
Lakini, ingawa Kingunge katika mahojiano yake na NIPASHE Jumamosi jana hakumtaja Lukuvi, alihoji “kama una majina ya watuhumiwa, unashindwa nini kuwataja.”

Kingunge alihojiwa na NIPASHE Jumamosi jana, baada ya kumaliza mkutano wake na waandishi wa habari, akisisitiza umuhimu wa kuyaweka hadharani majina hayo.

"Kumbe wanawajua, tatizo ni nini, kwanini hawawaelezi vyombo vya usalama wawachukulie hatua, kuwachunguza, kuwapekua, ili wafichuke na hatua zichukuliwe,” alisema Kingunge aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini tangu utawala wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Aliongeza, “sijaelewa stahili gani inayotumika, maana na mimi nimesikia mtu kasimama na kusema wabunge ni miongoni wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya, inaonyesha anawajua kwa nini asiwataje."

Hata hivyo, Kingunge alisema mhusika wa taarifa hiyo (hakumtaja kwa jina), inaonyesha ana taarifa za kutosha na anashangaa ni kwa nini hapigi vita dawa za kulevya badala yake kuwaacha raia wanaumia.

"Hii ni sawa na ile ya kusema `vigogo’ wameweka fedha nyingi nchini Uswis. Ni kwa nini hao `vigogo’ hawatajwi wananchi tukawajua waliopeleka kuhifadhi fedha huko nje ya nchi," alihoji Kingunge
Alisema kwa sasa nchi imeingia kwenye udhaifu mkubwa, kwani watu wanathamini zaidi fedha na vyeo bila kujali utu wa mtu.

Alisema wanaotuhumiwa kwa dawa za kulevya wanapaswa kusakwa pasipo kuwaonea huruma.
Kingunge alisema watu walioweka fedha mbele kuliko utu, wanaweza kushawishika kiurahisi kujiingiza kwenye biashara kama ya dawa za kulevya.

Alisema kuna madhara makubwa katika utumiaji wa dawa za kulevya na kwamba kazi kubwa zaidi ni kuendesha kampeni ya kuelimisha vijana dhidi ya suala hilo.

Hata hivyo, alisema jambo la msingi ni kupambana katika kupiga vita dawa hizo na pia kuangalia upya sheria zilizopo kama zina upungufu, zirekebishwe ili kufanikisha adhabu kali kwa wahusika.

Alisema jambo jingine ambalo linatakiwa kushughulikiwa kwa umakini ni upatikanaji wa ajira hasa kwa vijana ili wasitumike katika biashara hiyo.
Aidha, alisema awali dawa hizo zilikuwapo hususani bhangi, na kwamba zilikuwa hazitumiki kibiashara kama ilivyo sasa kwani watu wamefanya ni sehemu ya kupatia utajiri.

Alisema Tanzania kwa kipindi cha nyuma ilikuwa inatumika kama ni kituo cha kupitishia dawa hizo, lakini sasa imegeuzwa kuwa kituo cha biashara hiyo kwa kupata wateja, jambo ambalo ni hatari kwa binadamu hasa kwa vijana.
Kingunge alisema dawa hizo zimewaharibu vijana wengi kiafya, akili, na zimewafanya watu kushindwa kujishughulisha katika kupata vipato halali badala yake kushiriki vitendo viovu.

Hivi karibuni kumekuwapo na wimbi la uingizaji na usafirishaji wa dawa za kulevya, unaofanywa na Watanzania hali iliyosababisha kuliharibu jina la nchi na watu wake mbele ya jumuiya za kimataifa.

Pia imedaiwa kuwa vijana hao ambao husafirisha mzigo wa dawa za kulevya wamekuwa wakitumwa na `vigogo’ wakiwamo wa wanasiasa.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Mheshimiwa Kingunge unataka kweli majina? Usije pata presha ukiona jina la mwanao limo! I'm just sayin......