KIJANA aitwaye Priscus Mushi, mkazi wa Mbezi jijini Dar ambaye ni muumini wa Kanisa la Efatha linaloongozwa na Mchungaji Josephat Mwingira ameanika masikitiko yake baada ya kutengwa na baadhi ya ndugu kufuatia kuoa mlemavu wa ngozi ‘albino’ aitwaye Tumaini Murungu.
Akizungumza katika Ukumbi wa Maji uliopo maeneo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo sherehe za ndoa zilifanyika, Mushi alisema alipotangaza nia ya kumuoa Tumaini baadhi ya ndugu zake walimtenga lakini hakukata tamaa kwani aliendelea na taratibu za ndoa.
“Nilimpenda sana Tumaini na niliamini ndiye mwanamke wa maisha yangu lakini nilipowaambia ndugu zangu kuwa nataka kumuoa, baadhi walinitenga kwa uamuzi wangu huo wa kumuoa Tumaini ambaye ni mlemavu wa ngozi eti nitakuwa nimeleta balaa nyumbani.
“Nilimuomba Mungu anisaidie na nikaongea na waumini wenzangu ambao walikubali kunifanyia sherehe.
Nawashukuru sana wakwe zangu ambao walinipokea na kunipa ushirikiano katika kulitimiza tukio hili. Pia nimshukuru mama yangu kwani uwepo wake umenipa faraja kubwa,” alisema Mushi.
Wakizungumzia kitendo cha Mushi kutengwa na baadhi ya ndugu zake, baadhi ya waumini walilaani wakieleza kuwa, si jambo zuri hata kidogo.
“Inaumiza sana, unajua binadamu wote ni sawa, kwani msichana albino hastahili kuolewa? Tuache ubaguzi usiyo na maana ambao unamchukiza hata Mungu.
"Eti kuoa albino ni mkosi kwenye familia, nani kasema? Imani hizi potofu zikemewa kwa nguvu zote,” alisema muumini mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Eliza.
-GPL
No comments:
Post a Comment