ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 2, 2013

HATA KAMA UNAMPENDA, IWEJE UKUBALI KUCHUNWA KIJINGAJINGA!


NDUGU zangu, kuna haka katabia kameshamiri sana huko mtaani ka baadhi ya watu kuanzisha uhusiano kwa lengo la kujipatia sehemu za kutatulia matatizo yao.

Yaani anaweza kutokea kumpenda msichana flani, ukawekeza mapenzi yako yote ukiamini anafaa kuwa mwenza wako wa maisha lakini kumbe wala yeye hakupendi ila anajifanya anakupenda ili akuchune tu.
Si hivyo, msichana ambaye ana kazi yake inayomuingizia kipato anaweza kushangaa anatokea kupendwa ile mbaya na kumfanya ajihisi mwenye bahati.
Msichana huyo naye anajikuta amekufa na kuoza lakini kumbe ameingia kwenye penzi la kisanii la kutaka kugeuzwa mlezi. Hako kamchezo ka wanaume wengi kupenda kupata wanawake wa kuwalea kameshamiri sana.
Hali hii sasa inasababisha watu kushitukiana, unakaa na kujiuliza kama kweli huyo uliyenaye anakupenda kwa dhati au kakupenda kutokana na pesa zako? Hata kama atajifanya kukuambia anakupenda kutoka moyoni mwake, utathibitishaje hilo?
Hakika ni ngumu na ndiyo maana inafika wakati unalazimika kujenga tu imani kwamba umependwa wewe ni siyo pesa zako licha ya kwamba kinyume chake pia ni sawa.
Sasa inakuwaje wewe mwanaume unakubali kuchunwa kirahisirahisi na mademu? Yaani mpenzi wako lakini anakufanya kama kitega uchumi halafu eti kwa kuwa umependa unakubali kugeuzwa zoba!
Hivi hujawahi kumsikia msichana akitamba mbele za wenzake kwa kusema; “Mimi nina kibuzi changu bwana kila ninachotaka kinanipa, kinajua kisiponipa nakitosa tu, yaani nakichuna kama sina akili nzuri.”
Si hivyo tu, wapo wanaume ambao pia ni kero kwa wapenzi wao, yaani wamegeuka wanaume kama mabinti kwa tabia zao za kutegemea kupewa kila kitu.
Unaweza kumsikia mwanaume akisema; ‘Aah! Yule demu kazimika ile mbaya na mapigo yangu kila ninachotaka ananipa, anajua akinizingua namtosa.’
Ninachotaka kusema ni kwamba, mapenzi ya kweli hayana uhusiano wowote na pesa, ukiona mpenzi wako anaweka pesa mbele na ukishindwa kumpatilizia anachokitaka anakasirika, jua penzi lake ni la kitapeli.
Sikatai suala la kusaidiana kwa wapenzi halikwepeki, mpenzi wako akiwa na shida fulani akaomba umsaidie, kama unao uwezo msaidie na kama huna mueleze kwamba huna kisha muangalie jinsi mnavyoweza kusaidiana kulitatua tatizo linalomkabili.
Kinachokera ni kutoishiwa na matatizo na wakati mwingine unakuta kuchuna kwingine ni kwa mambo ya starehe. Yaani sasa hivi umemuomba mpenzi wako vocha, hajakaa vizuri umemtaka akija akuletee chipsi mayai, baadaye unataka akupeleke ‘out’, bila kujali kama fedha ipo au haipo.
Katika mazingira hayo unadhani mpenzi wako atashindwa kukuchoka? Akikuacha kwa sababu hiyo utamlaumu? Huwezi kumlaumu, hivyo tusiwageuze wapenzi wetu tunaowapenda kuwa vibuzi lakini na nyie wanaume nanyi hata kama mmependa msikubali kuchunwa kijingajinga.

Global Publishers

No comments: