ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 26, 2013

HESABU MAKOSA HAYA 7, HAKIKISHA HUYAFANYI KATIKA UHUSIANO WAKO - 8

Wiki iliyopita, tuliishia katika kosa la mwisho ambalo ni ubinafsi. Kama ilivyoelezwa ni kwamba ubinafsi una matawi mengi. Mtu anaposaliti, maana yake ametekwa na tamaa binafsi. Anashindwa kutambua kuwa yeye ni mpenzi wa mtu.
Ukweli ni kwamba unapoanzisha uhusiano na mtu, maana yake umeamua kumchagua yeye ndiye amiliki penzi lako.

Kwa hiyo ukienda kulitoa kwa mwingine, huo ni ubinafsi. Umeingiwa na umimi kwa kuona kwamba unatoa rasilimali za ndani ya mwili wako mwenyewe.
Usaliti ni ubinafsi. Umeingiwa na jeuri kwamba unacho ndani ya mwili wako, kwa hiyo unaweza kukitumia bila kumshirikisha mwenzi wako. Hiyo ni tabia mbaya mno. Kabla ya kusaliti, fikiria utakavyoumia pindi utakaposalitiwa.
Unapozunguka, usiwaze “upo”, unatakiwa kuwaza “mpo”. Hii itakusaidia kulinda siti ya mwenzako kila utakapokwenda. Hakikisha nafasi ya mwenzi wako haichafuliwi au kutolewa mkopo. Kama ilivyo kwenye soka, wachezaji huchezea timu nyingine kwa mkopo ndivyo na mapenzi ya sasa yalivyo.
Ni kweli mtu ana mpenzi wake lakini anavyojieleza anatoa picha kwa muulizaji kuona kwamba aliyepo si muhimu sana. Hii husababisha muulizaji aombe kukaa na baadaye hukaribishwa. Wengi walikaribishwa kwa mkopo, mwisho wakawa wamiliki wa jumla.
Si wakati wa kuchukia unapotendwa, bali unatakiwa uache ubinafsi. Haliitwi penzi bila kuwepo watu wawili. Lazima uhakikishe unalinda la mwenzako ili na lako lilindwe. Somo la mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu, linafundisha kuacha ubinafsi. Mfikirie mwingine.
Kama ambavyo ubinafsi unavyowatesa wananchi pale kiongozi mwenye dhamana kiserikali anaposhindwa kutimiza majukumu yake na kuamua kushughulikia shida zake binafsi, huku akitumia rasilimali za umma, ni kirusi hatari kila upande.
Baba anapoamua kufuja fedha wakati anajifahamu anayo familia inayomtegemea, huo ni ubinafsi. Anafikiria kutumbua yeye binafsi, wakati anatakiwa kujenga msingi wa familia. Anashindwa kujua kwamba fedha anazotafuta si zake peke yake.
Kama anaona anatakiwa kutumia fedha zake peke yake, basi hapaswi kujipa mzigo wa kumiliki familia. Mtu anapokuwa baba au mama, uamuzi wake unatakiwa uwe kwa ajili ya wengi. Kumaliza mshahara au kipato chake halali kwenye kumbi za starehe ni ukatili kwa familia hususan mtoto ambaye hakukuomba umlete duniani.
Usijidanganye kwamba unajimiliki mwenyewe. Wewe unamilikiwa na familia yako, kwa hiyo una deni na wajibu mkubwa kwa wale wanaohusika. Kabla ya kwenda nyumba ya kulala wageni na huyo unayemtamani, fikiria kwamba unamilikiwa.
Baba au mama, anapokwenda hoteli na mpenzi wa nje akakubali kuvua nguo na kufanya mapenzi. Ajitambue kuwa anachezea maisha ya watu wengine. Kuna maradhi, kwa hiyo unatakiwa uwe na afya njema ili wanaokumiliki waendelee kupata huduma yako.
Unafahamu kwamba mapenzi yanaua. Unaelewa kuwa unaposhindwa kuwa mtulivu nyumbani, unaiba muda wa familia yako. Kumbe sasa, fedha siyo zako ila ni za familia. Unaweza kupata picha kwamba viungo ni vyako lakini penzi si lako. Ukilitoa ni wizi, ni dhuluma iliyopitiliza.
Watu watakapoacha kujifikiria wenyewe, itakuwa mwanzo wa suluhu ya kimapenzi. Migogoro mingi itaondoka, familia nyingi zitakuwa imara, watoto wa mitaani watapungua kama siyo kwisha kabisa, kadhalika vitendo vya watu kutesana nyoyo, vitaadimika.
Sote tutakubaliana katika ukweli kuwa nafsi ya kwanza hutangulia kabla ya kufuata ya pili. Hiyo ndiyo imechochea tofauti za sasa. Kila mtu anakuwa anajijali mwenyewe bila kujua kwamba uhusiano wa kimapenzi na familia hauendi hivyo. Katika mapenzi hakuna maslahi binafsi. Nguvu, elimu na maarifa ni vyako ila ukishavitumia kuingiza fedha zinakuwa si zako tena. Zinakuwa za familia yako. Endapo utakuwa na nidhamu binafsi kwenye kutumia, utakuwa umeushinda ubinafsi. Hebu anza leo kupambana na ubinafsi kwa ajili ya maisha yako.
GPL

No comments: