Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman akimpongeza Francis Mutungi baada ya kuapishwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Jaji wa Mahakama Kuu katika hafla iliyofanyika Ikulu, Juni 19,2012. Jaji Mutungi jana aliteuliwa kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa. Picha na Maktaba.
Dodoma. Msajili mteule wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amewataka Watanzania kutulia na kusubiri utendaji wake atakapokabidhiwa rasmi jukumu hilo jipya alilopewa na Rais Jakaya Kikwete.
Mutungi aliteuliwa kushika wadhifa wa msajili wa vyama vya siasa kuchukua nafasi ya John Tendwa ambaye amestaafu. Tendwa aliiongoza taasisi hiyo kwa miaka 13.
Mutungi alisema: “Ninafahamu nina majukumu mazito mbele yangu, lakini siwezi kusema chochote kwa kuwa sijakabidhiwa rasmi ofisi. Ninachotaka kusema ni kwamba nitakuwa mtumishi wa kila mmoja.”
Alikataa kusema kuwa akianza kuzungumza mambo mengi kwa sasa wakati hajaingia rasmi kazini haitakuwa na maana yoyote na badala yake ataonekana kuwa anawahisha mambo.
Jana katika Mahakama Kuu ya Dodoma, ilikuwa tabu kumpata kiongozi huyo hali iliyoonyesha huenda alikuwa katika maandalizi ya kuweka mafaili yake katika hali nzuri kabla ya kuwaaga watumishi wenzake na kwenda kuanza majukumu mapya.
No comments:
Post a Comment