ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 2, 2013

Jumuika na chaUKIDU, jivunie Kiswahili KILA SIKU YA IJUMAA

Lengo:
Hili ni jukwaa ambapo wataalamu, wakereketwa na wafurukutwa  wa Kiswahili - kupitia Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (chaUKIDU: www.chaukidu.org ) chenye makao makuu yake nchini Marekani – wanakuleteeni  makala au mijadala mifupi ya uchokonozi kuhusu masuala anuai ya Kiswahili kama vile ukuaji wa msamiati, aina za msamiati, mikanganyiko na mikengeuko ya kisarufi na hata ya kitahajia, miktadha ya mawasiliano na athari zake katika matumizi ya lugha, sera za lugha, Kiswanglish, nk. nk. Lengo ni kuwa na jukwaa shirikishi katika ukuzaji na uendelezaji wa lugha yetu pendwa. Jivunie Kiswahili

Kuna Kiswahili kimoja au Viswahili vingi?

Liliibuliwa ama liliibuka suala la ‘usahihi’ wa lugha: ni Kiswahili kipi ni sahihi na kipi sio sahihi! Mintaarafu hoja hii, nimevutiwa na kamusi hizi mbili zilizotungwa na taasisi mbili tofauti katika Jamhuri ya Mungano wa Tanzania zinazoshughulikia taaluma ya Kiswahili, BAKIZA na TUKI (sasa TATAKI). Ni taasisi ipi iko sahihi kuhusu neno ‘kamusi’? Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA) linakiita kitabu chake Kamusi la Kiswahili Fasaha (Oxford, 2010)na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) inakiita kitabu chake Kamusi ya Kiswahili Sanifu (Oxford, 2004). Kwa mujibu wa BAKIZA kuna ‘kamusi’  (li-) na ‘makamusi’ (ya-) na kwa mujibu wa TUKI, kuna  ‘kamusi’ (i-)/(zi-). Lakini pia vitabu hivi vinaibua dhana ya ‘Kiswahili Sanifu’ na “Kiswahili Fasaha’. Kwa maoni yangu, ‘kamusi la Kiswahili’ ni Kiswahili fasaha na ‘kamusi ya Kiswahili’ ni Kiswahili sanifu. (Charles Bwenge, cbwenge@ufl.edu )

No comments: