ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 30, 2013

jumuika na chaUKIDU-Mhafidhina vs. mhifadhina

 Mhafidhina vs. mhifadhina 
Maneno huwakilisha dhana. Dhana inayowakilishwa na neno ‘mhafidhina’ / ‘mhifadhina’ ni muhimu sana kwa sababu ni hali inayotutokea katika maisha yetu ya kila siku katika jamii zote duniani - nayo ni ‘mtu anayeshikilia na kuifuata falsafa na mfumo maalumu wa kuendesha jambo” (BAKIZA, 2010) au ‘mtu asiyependa mabadiliko’ (TUKI, 2004). Maumbo yote mawili yamekuwa yakiyumika kama visawe.  Je kuna umbo lililo sahihi zaidi ya jingine? Mimi binafsi nimekuwa nikitumia “wahifadhina” kwa kufikiri kwamba ni umbo linalotokana na kitenzi “hifadhi” (weka mahali pa salama; tunza) ambapo kitenzi hicho kimezaa nomino “mhifadhi” (mtu anayechunga na kuangalia kitu kisiharibiwe).  Kwa kuzingatia leksikografia ya Kiswahili (Swahili lexicography), historia ya neno “mhafidhina”  inaonesha kuwa neno hili halikuingizwa katika kamusi hadi miaka ya hivi karibuni. Hivyo kuashiria kwamba pengine haja ya kulitumia haikuwa kubwa sana miongoni mwa wazungumzaji wa Kiswahili. Kwa mfano, katika kamusi zote nilizochunguza (japo kwa haraka haraka) hakuna iliyoingiza umbo lenye tahajia ya “mhifadhina”. Swali: ni kwa nini basi watumiaji wanatumia tahajia isiyotambuliwa na watunzi wa makamusi?

Kamusi
mhafidhina
mhifadhina
mhafadhina
mhifadhi
Kamusi ya Kiswahili (J. Johnson, 1935
X
X
X
X
A Standard Swahili-English Dictionary (Frederick Johnson, 1939)
X
X
X
X
Kamusi ya Kiswahili Sanifu (TUKI, 1981)
X
X
X
V
Kamusi ya Kiswahili-Kiingereza (TUKI, 2001)
X
X
X
V
Kamusi ya Kiswahili Sanifu (TUKI, 1981, 2004)
V
X
X
V
Kamusi la Kiswahili Fasaha (BAKIZA, 2010)
V
X
X
X
[X = halimo; V= limo]
Mifano michache ya watumiaji kutoka mtandaoni
1. Salamu wahafidhina, watumwa na vibaraka. Nchi ishavimbiana, na punde itapasuka. Hamuna jengine tena, lisilo kubadilika (http://kurasampya.wordpress.com/2012/10/04/salamu-wahafidhina-watumwa-na-vibaraka/ )
2. Inakuwa vigumu kuwashawishi wahafadhina kwamba ujana na usomi ni mtaji katika uongozi (Dec 5, 2008 – JF)
3.  ... na vita kuna umuhimu mkubwa kwa vyama vya Wahafadhina na Demokrasia ya Kiliberali vilivyounda serikali mpya ya mseto ya Uingereza Jun 11, 2010  (http://kiswahili.irib.ir/uchambuzi/item/12917-safari-ya-waziri-mkuu-wa-uingereza-nchini-afghanistan )
4.  Wahifadhina wanofikiri, haikazo turujumuni. Tangu ndemi tangamani, Kiswahili tumekienzi, Mbona sasa lakini, kaja mja wa ushenzi, (http://redscarwrites.blogspot.com/2010/03/kiswahili-kitakithiri.html)

5. Bw. Lee Hoi-chang mwenye umri wa miaka 72 anachukuliwa kama ni mwakilishi wa kundi la wahifadhina, aliwahi kuwa jaji mkuu na waziri wa ... (http://swahili.cri.cn/1/2007/12/18/1@68834.htm )

No comments: