ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 23, 2013

jumuika na chaUKIDU Tukitoe Kiswahili Utumwani

Kutoka makavazini: “Tukitoe Kiswahili utumwani kwanza”
Katika toleo la gazeti la RAI la Agosti 11-17, 2005 Ndugu Prudence Karugendo aliandika makala nzuri iliyobeba kichwa cha habari “Tukitoe Kiswahili utumwani kwanza”. Mojawapo ya hoja zake ilisomeka hivi:

Kuazima, kukopa na kutohoa (kupora) maneno ya Kizungu na Kiarabu na kuyaingiza katika msamiati wa Kiswahili nakupinga kwa sababu zifuatazo: Kwanza, ni kudhoofisha Kiswahili kwa kukiwekea viraka, jambo linalokifanya kionekane kama lugha isiyo na msamiati unaojitosheleza. Pili, kunakiondolea uasili wake na kukipotezea maana mahususi ya ujumbe unaobebwa na lugha, yaani kueleza kwa watumiaji wapya mila na desturi za watu wa asili ya lugha husika. Tatu, hili neno ‘kutohoa’ naweza nikalitafsiri kama kupora. Kwa vile hakuna makubaliano yanayofanyika kati ya lugha mbili ili kuamisha neno kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine. Basi kutohoa neno au maneno ni kupora maneno ya lugha moja na kuyapachika katika lugha nyingine. Hivi kweli hili ni jambo la kujivunia na kuzunguka dunia kunadi lugha iliyojaa maneno yaliyoporwa? Kwa maana hiyo kutohoa maneno na kuyajaza kwenye Kiswahili chetu hakutufai.”

Maoni yangu:

Katika zama hizi za utandawazi, dhana mpya zinaingia kila siku na kwa kasi kubwa katika jamii ya wazungumzaji wa Kiswahili. Kila dhana mpya inapoingia huhitaji kupewa jina ili kuwezesha mawasiliano. Kukopa na kutohoa ni mojawapo ya njia mujarabu za kuziba mapengo hayo ya kimsamiati. Hata hivyo, utohozi unaweza kudhoofisha lugha iwapo unatumiwa vibaya. Katika tangazo hili bainisha utohozi mzuri na mbaya na toa sababu. (cbwenge@ufl.edu )
"pata intaneti na bado muda wa maongezi kwa miezi sita bure"

No comments: