ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 12, 2013

Kazi mtindo mmoja

Tido Mhando
Kwa miaka mingi Tido Mhando amekuwa akifanya kazi ya utangazaji redioni. Kazi ya ndoto yake. Kazi iliyomwezesha akutane na watu wengi, asafiri kwingi na aone mengi. Kwenye simulizi zake hizi za kila Jumapili, Tido anaelezea baadhi ya hayo aliyokutana nayo. Jumapili iliyopita alimalizia kuhusu safari yake ya kwanza nje ya Tanzania huko Uganda, enzi ya utawala wa kijeshi wa Jenerali Idi Amin Dada ambako alikwenda kutangaza mashindano ya mpira ya kanda, Tanzania ikashindwa na Uganda kwenye mechi ya fainali. SASA ENDELEA...
Kujikuta kwenye Uwanja wa Ndege wa Entebbe asubuhi ile ya Jumapili Septemba 30 mwaka huo wa 1973 tayari kwa safari ya kurejea nyumbani ilikuwa faraja kubwa, tena kubwa mno, maana hatimaye tulikuwa tunatarajia kuondokana na lindi la mawazo yaliyojawa na wasiwasi mkubwa kwa kipindi hiki cha majuma mawili tuliyokuwepo kwenye mikono ya Idi Amin asiyetabirika.
sKwa mantiki hiyo hiyo, bado tulikuwa kwenye hali ya tahadhari, maana tulikuwa bado Uganda, huku nikijisemea mwenyewe kuwa lolote lingeweza kutokea. Tulikuwa tumewasili uwanjani hapo mapema kuliko wenzetu wengi wa timu nyingine zilizoshiriki kwenye michuano hii na ambao nao pia walikuwa wanaondoka siku hiyo.
Wakati nikiwa natafakari hili na lile, mara likaingia basi lililokuwa limewachukua wachezaji wa Taifa Stars. Walikuwa wamechangamka licha ya kwamba walikuwa wamepoteza mechi yao ya fainali siku iliyopita. Hapana shaka walikuwa wamepigana kiume, walipigana kufa na kupona kama walivyokuwa wameagizwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira Tanzania (FAT) siku hizo, Said Hamad El Maamry.
Niliwaona wakishuka mmoja mmoja. Nilikuwa nimewazoea sana jamaa hawa, ungedhani nilikuwa mmoja wao! Alitangulia kushuka Mwalimu Paul West Gwivaha. Jamaa alikuwa anajiamini kwelikweli na bila ya shaka hii ilikuwa ndiyo sababu mojawapo ya mafanikio ya kikosi hiki, maana acha bwana, Taifa Stars ile ilitisha!
Wakati mwingi tulipokuwa tukizungumzia masuala ya mpira, tulikuwa tunasema kuwa, kama vile ilivyokuwa kikosi kile cha mwaka 1970 cha timu ya taifa ya Brazil, ambacho hadi leo kinaelezwa kuwa labda ndiyo timu bora ya taifa kuwahi kutokea, kwa Tanzania kikosi hiki cha miaka hii kilikuwa na sifa hizo hizo. Na ndiyo maana kilikuwa kinaondoka Uganda asubuhi ile kikiwa kimeacha gumzo kubwa.
Basi nikawaona wanaendelea kushuka mmoja baada ya mwingine. Alifuatia nguzo ya timu siku zile, Omar Zimbwe. Mtu wa uhakika, ukuta wa kweli kweli kwenye ngome ya timu hiyo, mwenye tambo lililojaa vizuri kiasi cha kuweza kumtisha labda hata Idi Amin mwenyewe, akiwa tayari kwenye timu hii ya taifa kwa zaidi ya miaka kumi mfululizo.
Halafu wakaja kina Shabani Baraza, Digongwa, Mwabuda, Omar Mahadhi, Willy Mwaijibe, Haidar Abeid (Muchacho) na Khalid Abeid. Hawa hawakuwa ndugu, ila walikuwa marafiki wakubwa. Akashuka Sunday Manara, Athumani Mambosasa, Abdalah King Kibadeni, Maulid Dilunga, Gibson Sembuli, Mzee wa Mtwara Mohamed Chuma, Khassim Manga na wengineo. Nilitabasamu na kujisikia fahari kubwa kuambatana na kikosi madhubuti kama hiki.
Hatimaye tuliondoka Entebbe, nikashusha pumzi kwa nguvu. Nikajua nimekamilisha kazi niliyokuwa nimetumwa kikamilifu na kwa uadilifu. Nilifurahi kwamba hatimaye na mimi nimeweza kukubalika kazini.
Nilirejea kituoni siku ya pili yake, yaani siku ya Jumatatu. Nikakutana na wenzangu, hasa kule kantini, wengi wakitaka kufahamu mambo yalivyokuwa huko Uganda. Walikuwa zaidi na hamu ya kujua maisha kwa jumla yalikwendaje kule Uganda. Sikuwa na mengi zaidi ya kuwaeleza kwamba safari yetu ilikuwa imejaa wasiwasi mkubwa na hivyo tulikuwa watu wa tahadhari sana.
Ingawaje hadi wakati huo nilikuwa bado najishughulisha pia kutengeneza vipindi vya muziki, kidogo kidogo nilikuwa naanza kuhamisha mapenzi yangu kwenda kwenye matangazo ya michezo, ikiwa ni pamoja na mara moja moja kutayarisha na kutangaza kipindi cha kila siku saa mbili kasorobo usiku cha “Michezo”.

Ukiondoa labda “Taarifa ya Habari”, hiki kilikuwa ni kipindi kilichokuwa kikipendwa zaidi. Kwa wakati huo aliyekuwa mtayarishaji wa “Michezo” hasa alikuwa Abdul Masoud. Kutokana na umahiri wake na mbwembwe za sauti yake alikipaisha sana kipindi hiki kikawa kinasikilizwa karibu na kila mtu aliyepata wasaa.
Kwa hiyo, pale ilipotokea kwamba Abdul hayupo kwa sababu moja ama nyingine, mimi nilishika usukani. Hata hivyo, mwenzangu alikuwa mpenzi zaidi wa habari za mpira wa miguu lakini mimi nilikuwa na mapenzi ya michezo mingine mingi ikiwa ni pamoja na riadha, ngumi, basketball, tenisi, mpira wa wavu (volleyball) na hata mbio za baiskeli na magari. Kwa jumla nilipenda michezo mingi.
Kwa hali hii, siku ambayo mimi nilishika usukani wa kipindi nilihakikisha kunakuwepo na mchanganyiko wa habari mbalimbali za michezo, tofauti na siku ambazo alikuwepo Masoud na hasa kwa kuwa mwenzangu tayari alikuwa pia kiongozi wa Klabu ya Yanga
Nakumbuka siku moja mwaka 1972 wakati wa zamu yangu ya kutengeneza kipindi hiki cha michezo, nikafunga safari hadi Sekondari ya Kibaha kulikokuwa kunafanyika mashindano ya riadha ya shule za sekondari za Mkoa wa Pwani siku hizo ikijumuisha na Dar es Salaam.

Nilipofika kule, nikashangaa kumkuta jamaa mmoja ambaye baadaye nilikuja kufahamu kwamba hakuwa mwanafunzi, bali alikuwa anashiriki tu kama sehemu ya mazoezi yake, akitimua mbio ambazo nilikuwa sijawahi kumwona binadamu mwingine yeyote akikimbia kwa kasi namna hiyo!
Nasema hivyo kwa kuwa na mimi nilikuwa na uzoefu mkubwa wa michezo hii ya riadha hasa nilipokuwa nikiishi Mpwapwa ambapo, kwa sababu ya kuwepo kwa shule nyingi pale, yalikuwepo mashindano ya mara kwa mara ya riadha kati ya shule na vyuo na baadaye wachezaji wengi walijumuishwa kwenye timu zilizoshiriki michuano mbalimbali ya kitaifa.
Namkumbuka mmoja wao alikuwa Erasto Zambi. Alikuwa mwanafunzi kwenye Chuo cha Ualimu cha Mpwapwa na ndiye aliyekuwa akishikilia rekodi ya taifa ya mita 100 siku hizo. Nilipendelea sana kumfuata kiwanjani ili kumwangalia akifanya mazoezi yake, kila jioni nikiwa na wenzangu kina Yassin Iddi na kaka yake Abasi, Martin Mganga, Martin Mwaimu, Alex Nhigula na wengine kadhaa tuliokuwa pamoja Mpwapwa Middle School.
Zambi alikuwa hataki utani hata kidogo awapo mazoezini. Alionekana wazi kwamba alikuwa ni mtu aliyekuwa na dhamira halisi ya kutaka kufanikiwa na kwa kweli baadaye alifanikiwa kwa kiasi kikubwa. Kwani baadaye alikuja akawa mkufunzi mkuu wa michezo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na pia Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki ya Tanzania (TOC), nafasi aliyodumu nayo kwa miaka mingi sana.
Halafu na mimi niliingia Mpwapwa Sekondari mwaka 1965, na hapo nikajenga urafiki wa karibu sana na kijana wa kutoka Kiomboi, Singida, Alfred Bernard Shillah Kinshwaga, aliyekuwa mwananafunzi mdogo kwa umbo kuliko wote pale shuleni, lakini nadhifu kupindukia. Pamoja na uwepo wa joto kali la Mpwapwa wakati wa mchana, Alfred siku zote alikuwa akinywa maji ya baridi kama yale yaliyohifadhiwa ndani ya friji, aliyokuwa akiyandaa mwenyewe kwenye chupa yake maalumu.
Nilipoingia shuleni hapo niliwakuta wanafunzi kadhaa waliokuwa wakitamba kwenye michezo mbalimbali. Miongoni mwao alikuwa ni John Zayumba ambaye pamoja na kucheza mpira vizuri, alikuwa pia akikimbia sana katika mbio za mita 100. Marafiki wakubwa wa Zayumba walikuwa Zablon Mhije na Alphonse Mkini, ambao pia walikuwa washiriki wa michezo mingi.
Kipindi ambacho wakazi wa Mpwapwa siku zile walikuwa wanakifurahia sana kilikuwa kipindi cha “Sikukuu ya Pasaka.” Kuanzia siku ya Alhamisi hadi Jumatatu ya Pasaka kila mwaka, kulikuwepo na mashindano ya kusisimua ya mpira wa miguu baina ya shule za maeneo ya karibu.
Zilikuwa zinashiriki shule za Alliance High School ya Dodoma, Dodoma Sekondari, Malangali Sekondari, Chuo cha Ufundi cha Ifunda, Iringa, wenyeji Mpwapwa TTC na Mpwapwa Sekondari na baadaye ikawa inakuja timu ya Sekondari ya St George na St Michael ambayo kabla ya uhuru ilikuwa ya wanafunzi wa Kizungu pekee na baadaye ikawa inachukua wanafunzi bora na pia kubadilishwa jina na kuitwa Mkwawa High School.
Wakati huu huwa ni kipindi cha msisimko kwelikweli pale Mpwapwa, kwani lilikuwa linapigwa kandanda la hali ya juu sana. Kulikuwa na upinzani uliokuwa dhahiri baina ya timu hizi. Ni hapa ndipo nami nilipojenga mapenzi makubwa, si kwa mchezo huu wa mpira wa miguu pekee, bali pia na michezo mingine mbalimbali.
Kwa hiyo, katika siku hii niliyofika pale Kibaha kutafuta habari za kipindi cha “Michezo” na kumkuta kijana huyu aliyekuwa mwembamba, mrefu kiasi, mng’avu, mwenye mvuto lakini akiwa anakimbia isivyo kawaida. Nilihisi moja kwa moja ya kwamba nilikuwa nimemwona mtu wa aina ya kipekee.
Nilimsubiri kwa muda baada ya kuwa amekimbia kwa kiasi hicho kilichonistaajabisha. Nikangojea apumzike. Nilitaka kufahamu zaidi juu yake. Nilijua kwamba haya yangekuwa mahojiano ya kihistoria. Nilikuwa na uhakika kuwa hakuna mtu aliyewahi kumhoji kijana huyu pale RTD, kwa hiyo hii ingekuwa, bila ya shaka, mara yake ya kwanza kuhojiwa redioni.
Naam, nafasi yangu ilifika muda siyo mrefu sana baadaye. Nilijitayarisha kwa maswali mengi, nikianzia na swali la kwanza la kutaka kufahamu jina lake na kazi anayofanya. Alinijibu kwa upole, “Naitwa Filbert Bayi, ni mwanajeshi.”
Miezi kadhaa baadaye, mapema mwaka 1973, kijana huyu mtanashati, kutoka Mkoa wa Arusha, aliushangaza ulimwengu kwa kumshinda mmoja wa wanariadha waliokuwa na majina makubwa duniani, mwanariadha aliyekuwa anawika zaidi ya radi ya umeme, mwanariadha nguli wa kutoka Kenya, Kipchoge Keino.
Bayi alimwangusha Keino kwenye mbio za mita 1,500 za mashindano ya Nchi za Bara la Afrika yaliyofanyika Lagos, Nigeria na huo ndiyo ukawa mwisho wa mkongwe huyo wa Kenya na ukawa mwanzo wa shani ya kijana Filbert Bayi wa Tanzania.
Aliporejea nchini Bayi alipokelewa kwa heshima kubwa na siku chache baadaye ikaandaliwa sherehe ya kumpongeza iliyofanyika kwenye Hotel ya Forodhani, jijini Dar (sasa ni Mahakama ya Rufaa), ambapo mgeni rasmi, Waziri Mkuu Rashid Kawawa, alitangaza kumpandisha cheo jeshini na kumpatia zawadi ya baiskeli.
Nilikuwepo kwenye hafla hii na vivyo hivyo kubahatika kuwepo kwenye hadhara nyingine kadhaa ambazo Filbert Bayi alilipatia heshima taifa letu la Tanzania.
Mwananchi
ITAENDELEA WIKI IJAYO

No comments: