ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, August 13, 2013

Kodi kuhamisha fedha yapingwa-Mwananchi

D’Salaam. Chama cha Benki Tanzania kinachohusisha benki na taasisi za fedha nchini (TBA) kimepinga Sheria ya Fedha ya mwaka 2013 iliyopitishwa na Bunge na kuchapwa kwenye Gazeti la Serikali toleo Na.27 juzuu 94 mwezi Julai mwaka huu.
Kwa mujibu wa sheria hiyo ambayo haikuwepo kwenye hotuba ya bajeti wala kujumuishwa kwenye muswada wa fedha, kutakuwa na ushuru kwa uhamishaji wa fedha kupitia benki, taasisi ya fedha au kampuni ya mawasiliano ya simu kwa kiwango cha asilimia 0.15 kwa kiwango kisichozidi Sh30,000.
Katika taarifa yao kwa vyombo vya habari iliyochapishwa kwenye magazeti jana, chama hicho kimesema kuwa hakikushirikishwa katika utungaji wa sheria hiyo bali kilipata taarifa kupitia mawasiliano yake na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Msimamo huo umekuja ikiwa ni siku chache tangu wadau wa sekta ya mawasiliano kupinga kodi ya kadi za simu ambapo kila mwananchi alitakiwa kukatwa Sh1,000 kwa mwezi.
Alipoulizwa kuhusu msimamo huo wa TBA, Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum licha ya kusita kuzungumzia alishangazwa na mtindo wa kupinga kodi tangu ile ya kadi za simu ambayo pia ilipitishwa katika Bunge la Bajeti la mwaka huu.

No comments: