Kocha wa Yanga,Ernie Brandts.
Kocha wa Yanga, Ernie Brandts ameelezea ushindani mgumu anaoutarajia katika mechi yao ya leo ya Ligi Kuu ya Bara dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, huku Simba wakifanya mazoezi kwa kujificha mkoani Arusha kuelekea mechi yao ya leo dhidi ya JKT Oljoro.Brandts alisema jana kuwa mechi ya leo kwenye Uwanja wa Taifa itakuwa ngumu kwa sababu Coastal imejiimarisha vyema katika kipindi hiki cha usajili tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita.
"Coastal ni timu nzuri, wana wachezaji wazoefu, itakuwa mechi ngumu sana," alisema Mholanzi huyo, aliyeiongoza Yanga kutwaa ubingwa wa bara msimu uliopita baada ya kuikuta timu ikiwa mkiani mwa ligi baada ya kumfukuza aliyekuwa kocha wao Mbelgiji Tom Saintfiet.
Mkoani Arusha, Simba ilifanya mazoezi katika viwanja tofauti na nia ya kujificha kuelekea mechi yao ya leo.
Meneja wa timu hiyo ya Msimbazi, Mosses Basena, aliiambia NIPASHE hapa Arusha kwamba walilazimika kufanya mazoezi katika viwanja tofauti ili kujiweka mbali na hujuma zozote zinazoweza kufanywa dhidi yao.
Basena alisema kwa kuwa wako ugenini, lolote lingeweza kufanywa ili kuwadhoofisha katika mechi yao ya leo ndiyo maana walikuwa wakifanya mambo yao kwa kujificha.
Hata hivyo, Wekundu wa Msimbazi walifanya mazoezi katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jana asubuhi kama kanuni zinavyoagiza kwa wageni kujifua katika uwanja wa wenyeji siku moja kabla ya pambano.
Wachezaji kadhaa wa Simba walisema hawako tayari kuzungumza jambo lolote kuelekea mechi hiyo bila ya ruhusa maalum.
Simba inahitaji kushinda leo ili kujiweka sawa baada ya kulazimishwa sare ya 2-2 dhidi ya timu iliyopanda daraja ya Rhino Rangers ugenini Tabora katika mechi ambayo kocha Abdallah Kibadeni alimlalamikia kipa Mganda Abel Dhaira akisema alifungwa kizembe na kusema: "Tuna makipa watatu, tutaangalia mechi ijayo tutamchezesha yupi."
Mabingwa Yanga walianza ligi kwa kishindo wakitoa kipigo kikubwa zaidi cha siku ya ufunguzi baada ya kuishindilia timu iliyopanda daraja ya Ashanti kwa magoli 5-1 kwenye Uwanja wa Taifa, lakini hawatarajiwi kupata mteremko leo dhidi ya Coastal ambayo ina morali baada ya kuwafunga Oljoro kwa magoli 2-0 katika mechi yao ya kwanza.
Yanga na Coastal zitakutana kwenye Uwanja wa Taifa kuanzia saa 10.30 jioni kwa kiingilio cha Sh. 5,000, Sh. 8,000, Sh. 15,000 na Sh. 20,000 chini ya mwamuzi Martin Saanya wa Morogoro.
Katika mechi nyingine za leo, Mtibwa Sugar itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro wakati Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora utakuwa mwenyeji wa pambano kati ya wenyeji Rhino Rangers na Azam.
Vumbi lingine litatimka kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani wakati maafande wa JKT Ruvu watakapokwaruzana na wenzao wa Tanzania Prisons kutoka Mbeya. Mbeya City na Ruvu Shooting zitacheza kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Jiji la Tanga litakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Mgambo Shooting na Ashanti United itakayochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment