Mada bado inaendelea kuhusu kuwa kwenye uhusiano wenye mashiko au ule wa kukupotezea muda. Wiki iliyopita nilishaeleza mengi lakini niliishia katika suala la ushawishi ambapo nilisema kwamba, hata kama ukishawishiwa kwa kiwango gani kama unajitambua unapaswa kusimama kwenye mstari unaotakiwa.
Hebu sasa tuendelee kujifunza. Kikubwa kwako ni kutuliza akili yako na kufungua ubongo wako kujifunza. Twende darasani...
CHUNGUZA, CHUKUA HATUA
Inawezekana upo katika uhusiano na tapeli wa mapenzi bila kujua, hiyo ni sumu na unachotakiwa kufanya sasa ni kuanza kumchunguza mpenzi wako mapema isije kuwa upo kwenye foleni!
Hakuna kitu kibaya kama kuwa katika foleni ya wapenzi kwa mpenzi mmoja, tena mbaya zaidi awe ni yule ambaye moyo wako umempenda kwa dhati – ni maumivu matupu.
Kumbuka, kuwa katika uhusiano na mtu ambaye haeleweki ni sawa na kukaribisha matatizo katika maisha yako. Huna sababu ya kuishi kwa wasiwasi ukiwa hujui mpenzi wako anakuchukulia vipi.
Anza kumuwekea mitego mapema. Lakini katika mitego yako achana na simu yake kabisa, huna sababu ya kuchunguza simu yake lakini kama ni msaliti utajua tu! Unafikiri atajificha mpaka lini?
Atafanya mambo yake gizani mpaka lini? Kuna siku utagundua na kumuacha aendelee na ‘shughuli’ yake kama ameona ndiyo maisha aliyoyachagua.
Usikubali kuwa katika penzi la kitumwa. Penzi la kisaliti. Kuwa na mtu ambaye anakuchanganya wa kazi gani zaidi ya kukupotezea muda na kukukaribishia machozi? Mchunguze sana na mwisho wa siku utakuja kugundua uongo wake ulipo.
Kama mwongo, unasubiri nini tena? Tafuta malisho sehemu nyingine ndugu yangu.
UTAMJUAJE SASA?
Hapo ndipo kwenye kazi. Kwa bahati mbaya sana kama ikitokea ukampenda mtu sana hata kama akifanya mabaya kiasi gani unaweza usiyaone.
Kama wewe ni wa aina hii unapaswa kubadilika kifikra. Mwone wa kawaida, fanya uchunguzi wako polepole na kama ukiona moja kati ya mambo yafuatayo, ujue kuna kitu. Fuatilia zaidi nyendo zake.
*HATAKI UJULIKANE
Hii ni kati ya alama alizonazo tapeli wa mapenzi. Ni mtu wa kufanya mambo kwa upekee sana. Kila dakika hakaukiwi na neno nakupenda sana, lakini moyoni mwake hakuna alama hata moja ya mapenzi.
Ni vigumu kumtambua mtu wa aina hii lakini chunguza kuhusu hili; hapendi kabisa kukukutanisha na rafiki zake na hata mkikutana nao kwa bahati mbaya basi hatakutambulisha na kama akikutambulisha hatakutambulisha kama mpenzi wake rasmi.
Atasema wewe ni rafiki tu. Tangu lini mpenzi akatambulishwa kama rafiki? Mtu anapomtambulisha mpenzi wake humtambulisha kwa kujisikia furaha moyoni kwamba anamtambulisha mpenzi wake lakini inakuwaje kwako akutambuilishe kama rafiki?
Baadaye utakapomuuliza hawezi kuwa na jibu la maana, atabaki kukuambia hata kama akikutambulisha kama rafiki jamaa ataelewa kuwa ni mpenzi wake. Hiki ni kichekesho.
Hakuna ukweli kama huo ndugu zangu! Huo ni ulaghai na anaogopa kukutambulisha kama mpenzi maana tayari ameshaonwa akiwa na wengine. Atawatambulisha wangapi? Aseme wewe ni nani?
*PENZI LA SIRI
Siku zote mambo yake ni kwa siri kubwa. Mfano mna ahadi ya kukutana, hataki muongozane. Atakuambia mkutane moja kwa moja sehemu husika.
Hata muda wa kuondoka atafanya kila njia ili kila mmoja aondoke mwenyewe na kama mkiondoka pamoja basi ujue ni usiku na hakuna atakayewaona.
Ikitokea akakubali muongozane, atakutanguliza kwanza kisha yeye atafuata nyuma. Siri yote ya nini kama kweli anakupenda? Mapenzi gani hayo yanafanywa kwa siri? Anakupotezea muda huyo.
Bado tunaendelea kujifunza marafiki. Vuta subira hadi wiki ijayo nitakapokuja hapa kuhitimisha mada hii, SI YA KUKOSA!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika Vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.
No comments:
Post a Comment