ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, August 21, 2013

UPO KWENYE PENZI HAI AU LILILOKUFA?-3


MARAFIKI zangu bado tupo kwenye mada yetu kama inavyosomeka hapo juu lakini jambo la kufurahisha leo ni kwamba somo hili linafikia ukingoni.
Ni wiki ya tatu tunaendelea na somo hili. Kama mtakumbuka vizuri, wiki iliyopita niliishia kwenye kipengele cha penzi la siri. Hebu sasa tuendelee kujifunza...

*Hamjulikani kwa ndugu
Mpenzi wa aina hii ni mjanja sana, kwanza atajifanya mtu mwenye ubize kwa muda mwingi. Hii yote ni kukwepa kuwajua ndugu zako au wewe kuwajua ndugu zake!
Wakati mwingine anakuwa hapendi ndugu zako na wake wakutane wakijua wazi kuwa nyie mna uhusiano, hili ni tatizo. Hakuna uhusiano wenye heri na malengo ya kuishi pamoja ukawa wa kificho cha kiasi hicho.
Hii ni alama unayotakiwa kuitazama na kukufanya ujue kuwa upo kwenye penzi la maigizo tu.
*Chenga nyingi...
Hili ni tatizo lingine wenyewe wanaita majanga. Tamaa ya mwili wake imeshaisha kwa maana hiyo haoni kama kuna umuhimu wa kukutana na wewe tena – ataanza chenga.
Hataki mkutane kwa kisingizio cha kazi. Ikitokea ukaamua kumfuata kazini kwake au nyumbani anakasirika. Tayari ameshapata anachokitaka, huna thamani tena. Hili ndiyo jibu unalotakiwa kuwa nalo.

*Mawasiliano sasa
Haoni umuhimu wa kuwasiliana na wewe kama zamani na kama akifanya hivyo, ujue ana shida yake muhimu. Inawezekana alishakuzoesha kukupigia simu kila wakati au kukutumia meseji za kukujulia hali, sasa hawezi kufanya hivyo tena.
Ukiona alama hii ujue mwisho wa penzi lenu unakaribia. Mwanaume wa aina hii anaweza kukupigia simu anapohitaji uende kwake kwa ajili ya kumfulia nguo zake, kumfanyia usafi nyumba au chumba chake, kumpikia na mambo mengine ambayo yatakuwa na manufaa kwake.
Ikiwa ni tofauti na hivyo basi ujue anahitaji penzi tu, hakuna kingine. Je, wewe ni kiwanda cha kutoa burudani? Ni mfanyakazi wa ndani wa kumfanyia usafi?
Kwanza si busara mwanamke kujipeleka kwa mwanaume na kuanza kumfanyia usafi kabla ya ndoa. Nini basi kitakachomvutia na kumshawishi au kuuona umuhimu wa kukuoa wakati kila kitu kinapatikana kabla ya ndoa? Funguka!

*Ataanza mikato kwa sana
Wakati huu huwa hapimi ajibu nini na lipi aache! Thamani yako kama mpenzi imeshaisha na sasa anakuona kama dada yake tu! Sanasana atakujibu vizuri pale atakapokuhitaji.
Wewe kama mpenzi wake una haki ya kumwuliza sababu za kuzima simu kwa saa tatu bila kukutaarifu na inawezekana huo ndiyo utaratibu wenu wa siku zote lakini kwa sasa unaweza ukakutana na jibu ambalo linaweza kukuharibia siku!

*Hajali tena
Hana furaha anapokutana na wewe, wakati mwingine anaweza kujisahau na kuonesha wazi kuwa hafurahii uwepo wako nyumbani kwake. Anaweza kukuuliza muda utakaokaa ili ajue mapema.
Vyote ni visa tu anakufanyia ili ujue kuwa huna lako tena. Zaidi ya yote hakusikilizi kama zamani. Atapuuza kila unachomwambia.
Kama ni mjanja sana wa mambo, anaweza kukusikiliza mara chache lakini kwa mambo yanayomhusu yeye. Kwa kifupi thamani na utu wako vinashuka na unakuwa mtu wa kawaida kwake kama walivyo rafiki zake wengine.

FIKIRI TOFAUTI SASA
Ingiza hili ubongoni mwako; kila kitu kinafanyika kwa mipango! Hata Mungu mwenyewe wakati wa uumbaji alipanga kuumba kila unachokiona. Yeye ndiye anayejua mwanzo na mwisho wa kila kitu.
Kama ndivyo, una haja gani ya kuwa na wasiwasi? Una sababu gani ya kuhisi lazima uolewe na huyo anayekutesa na kuunyong’onyesha moyo wako? Huna haja ya kuumia kiasi hicho. Mungu amekuumba kwa makusudi, amekujalia ukakua, ukasoma hadi ukafikia hapo ulipo hivi sasa.
Anajua maisha yako. Using’ang’anie usipokubalika. Hebu mwache afanye kazi yake apendavyo. Atakupa aliye sahihi kwa ajili yako. Subira yavuta heri!
Darasa limekuingia? Kama ndivyo, wiki ijayo nitakuwa na mada nyingine kali zaidi, USIKOSE RAFIKI YANGU!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika Vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.

No comments: