ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, August 29, 2013

USANII, UJANJA NA UTAPELI UNAVYOTUTIBULIA MAPENZI-2

AWALI ya yote naomba niseme kwamba nawapenda wote! Mapenzi yangu kwenu ndiyo yanayonifanya niandike mada ambazo naamini zitakuwa na manufaa katika maisha yenu ya kimapenzi.
Lengo ni lilelile la kuhakikisha tunakuwa na maisha yaliyotawaliwa na amani. Lakini wakati wengi wetu tukilihangaikia hilo, wapo ambao wanacheza ‘makidamakida’ kwenye ulingo wa mapenzi.
Kwao kuwaumiza wenzao ni jambo la kawaida. Yaani hawaoni hatari kuanzisha uhusiano kwa nia ya kupata sehemu ya kuchuna pesa tu.
Wapo vijana huko mtaani ambao wameingia kwenye uhusiano wa kimapenzi huku wakieleza kuwa wamependa kwa maana halisi ya kupenda kumbe hawana lolote, wana malengo yao na yakishatimia wanaingia mitini.
Mbaya zaidi na sisi tunaopenda tunajisahau kwamba kuna mapenzi ya kisanii na ya kitapeli ambayo yapo mtaani, tunapenda kupita kiasi na baada ya siku chache tunaachwa kwenye mataa na kubaki kujutia kutendwa.
Ninachotaka kukieleza hapa ambacho nilikianza wiki iliyopita ni kwamba, usanii katika mapenzi unatuharibia furaha ya maisha yetu. Tunatamani kupenda lakini tunapoingia kwenye uhusiano tunakuwa hatuna amani kwani tunahisi tunaweza tukawa tumeingia sehemu ambayo siyo.
Unaweza kutokea kumpenda sana mtu flani naye akakuambia anakupenda zaidi yako lakini kulithibitisha hili inakuwa ngumu sana. Matokeo yake unakaa roho juujuu. Ukimpigia simu akichelewa kupokea, unahisi umeshaachwa kumbe yawezekana yuko mbali na simu.
Mimi nadhani kikubwa hapa ni kila mmoja kutambua kuwa ulimwengu wa mapenzi wa sasa umejaa ulaghai uliopitiliza. Sehemu ambayo unahisi kuna penzi la kweli unaweza kukuta hakuna kitu bali usanii mtupu.
Ukishalitambua hilo inakuwa ni rahisi kwako kuwa makini sana na mtu ambaye unaingia naye kwenye uhusiano. Lakini pia ukilitambua hilo huwezi kuingia kichwa kichwa kwa kila atayekuambia anakupenda, hata kama utampa nafasi kwenye moyo wako lakini huwezi kumuamini kwa asilimia zote. Utaanza kwa mguu mmoja ndani, mwingine nje. Pale ambapo utabaini siyo msanii ndipo utaingia miguu yote kisha kumpa nafasi kubwa ndani ya moyo wako.

Kwenu wanawake
Wanaume wengi siku hizi hawapendi bali wanatamani. Anakuona leo anatamani uwe wake lakini huyohuyo ana mtu mwingine. Ukikubali ujue atakuvua na kesho hutamuona tena. Je uko tayari kuvuliwa nguo na wanaume wengi katika maisha yako?
Lakini lingine ni hili la tamaa. Hata kama maisha ni magumu vipi, acha tamaa za kutaka kupata pesa kwa kuutumia mwili wako. Eti kwa kuwa unataka kuvaa vizuri, kula vizuri, kuwa na simu kali basi utakuwa tayari kuwa na mwanaume yeyote mwenye nazo, unatambua uwepo wa Ukimwi?
Mimi niwashauri kitu kwamba, mapenzi yanachukua nafasi kubwa sana kwenye maisha yetu. Tuwe na nidhamu ambayo itatufanya tusiyahatarishe maisha yetu.
Tunayo mioyo ya kupenda kama ilivyo kwa kila binadamu lakini tuangalie yupi wa kupenda kwa maana halisi ya kupenda. Tukumbuke hatuwezi kuwa na mapenzi ya kweli kwa zaidi ya mwanaume mmoja.

Na nyie wanaume...
Eleweni wapo wasichana ambao wanajua kujifanyisha sana kuwa wamependa. Ukiwa naye atakuonesha kukupenda sana lakini kumbe hana lolote, ni mwizi, tapeli mwenye lengo la kukuchuna kisha ukishaishiwa anaingia mitini.
Lakini muache pia tabia ya kutaka kujiweka kwa kila mwanaume mzuri. Huko mtaani wanasema, kila ukiona kichaka unataka kujisaidia. Hivi unadhani ukiwembe wako utakusaidia kitu kwenye maisha yako?
Unadhani sifa ya kwamba umetembea na mademu wengi tena wazuri itakuongezea kitu kwenye maisha yako kama siyo kujidhalilisha na kuonekana kila unakopita ni kama unatembea uchi? Tuna kila sababu ya kuamua kubadilika. Tuache ulimbukeni!
Mwisho naomba nizungumzie wale wenye pesa zao, wanawake kwa wanaume! Jamani hizo pesa zenu msizitumie kwenye kununulia mapenzi. Mapenzi hayauzwi jamani! Wewe mwanamke mtu mzima unatafuta ‘kijiserengeti boi’, unakiahidi kukihudumia kila kitu ili kikupe penzi, inakuja kweli?
Baba mtu mzima eti kwa kuwa una vijisenti vyako basi kila msichana hata yule ambaye ni kama mwanao unataka kumuonja, huko mnakotupeleka siko. Tunajua wengine na hizo pesa zenu mnataka kusambaza virusi vya Ukimwi, tumewashitukia!

GPL

No comments: