ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 19, 2013

Wabunge wacharuka

  Washtushwa usiri wa mali za viongozi
  Sasa wataka ziwekwe kwenye tovuti
Andrew Chenge
Kamati tatu za Bunge zimelalamikia Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwamba haiweki uwazi wa kutangaza umiliki wa mali za viongozi hivyo kusababisha viongozi kutoweka wazi mali wanazomiliki.

Hayo yamo katika maazimio 22 ya Kamati hizo ambazo ni kamati ya Serikali za Mitaa (LAAC), Kamati ya Bajeti (BC) na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), baada ya mafunzo kwa wajumbe wa Kamati hizo yaliyofanyika wilani Bagamoyo.

Kwa mujibu wa maazimio hayo, kamati hizo zimesema kutokana na usiri huo wa mali za viongozi wa umma, ni rahisi mtu kuzushiwa umiliki usio wa ukweli.


“Ni vyema Sekretarieti wakafanya utafiti wa umiliki wa mali kwa viongozi wa umma na kuweka taarifa hizo katika tovuti ya Sekretariati ili kuwawezesha wananchi kuona mali zinazomilikiwa na viongozi wao na pale ambapo kiongozi hatakuwa ametoa taarifa ya umiliki huo, basi taarifa hiyo itolewe kwa Tume,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo iliyopatikana jijini Dar es Salaam jana.

Vile vile, kamati hizo zimependekeza Bajeti ya Bunge iongezwe kupitia Mfuko wa Bunge na iwe inawasilishwa bungeni na Naibu Spika na siyo Ofisi ya Waziri Mkuu.

Maazimio ya Kamati hizo yanasema kutokana na kutokuwapo kwa taarifa sahihi kuhusu deni la Taifa, kuna umuhimu wa kukutanisha wadau wakuu wanaohusika hususani Benki Kuu (BoT) Hazina,  Kamati za Bunge na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ili kujua kwa usahihi zaidi ukubwa wa deni hilo.

Vile vile, ilisema wameazimia kuwa serikali ishauriwe kuunda chombo huru kitakachosimamia deni la taifa.

Ilisema baada ya kuanzisha mfumo mpya wa bajeti ya serikali mwaka huu, kuna umuhimu wa kuandaa mkutano wa kutathmini mafanikio na changamoto za mfumo huo na kujadili mambo ya kuboresha zaidi mfumo mzuri wa bajeti ya serikali.

Kamati zimetaka serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge na Tamisemi, waanzishe utaratibu wa kuratibu mikutano na mafunzo ya wakurugenzi wa halmashauri kwa pamoja kuliko kila wizara kuwaita watendaji hao katika sehemu mbalimbali kwa muda tofauti na kuwafanya kutokuwapo ofisini kwa kipindi kirefu.

Pendekezo lingine la kamati hizo ni kuboreshwa kwa mfumo wa kutunza kumbukumbu za hesabu na nyaraka mbalimbali katika Serikali Kuu na Halmashauri ili zinapohitajika zipatikane kwa wakati mwafaka bila kisingizio cha aina yoyote.

Kuhusu ukaguzi wa ufanisi CAG, Kamati hizo zilipendekeza asisubiri mpaka asikie malalamiko kutoka kwa wananchi au kwenye magazeti bali akague mara kwa mara sehemu zote zenye matatizo.
“Taarifa za mwaka za Kamati za Bunge ziwe na kipengele cha kiwango cha utekelezaji wa mapendekezo ya Kamati yaliyotolewa awali," ilisema.

Taarifa hiyo ilisema Bunge litenge siku ya kuijadili serikali ilivyoshughulikia hoja za Kamati za Bunge na Spika ashauriwe kuhusu umuhimu wa kuunda Kamati ya Bunge ya kufuatilia ahadi za serikali.

Azimio lingine ni la kutaka mikataba katika ngazi ya serikali za mitaa iandikwe kwa lugha ya Kiswahili na serikali ifanye jitihada za ziada kuzalisha wataalam wa fani ya manunuzi.

Taarifa hiyo ilisema kuna umuhimu wa Mamlaka ya Manunuzi (PPRA) kuongezewa nguvu za ziada za kiutendaji ikiwa ni pamoja na fedha na wafanyakazi.

Aidha, ilisema serikali inapaswa kuandaa mjadala wa kitaifa wa kutafuta ufumbuzi wa kukabiliana na vitendo vya rushwa na mmomonyoko wa maadili vinavyoongezeka kwa kasi hapa nchini.

Taarifa hiyo ilisema  viongozi wa umma na watendaji wanapaswa kuongoza kwa mfano kwa kutojihusisha na vitendo vya rushwa katika kutekeleza majukumu yao.

Pia ilisema kwa kuwa leseni za udereva za sasa zinaweza kuweka kumbukumbu za makosa ya usalama barabarani, basi Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) ikishirikiana na  Wizara ya Mambo ya Ndani kuhahakikisha askari wa usalama barabarani wanatumia utaratibu huo wa kisasa wa kutoa  `notification' na kutoa risiti za malipo za elektroniki.

Kamati hizo zimendekeza Sheria ya `Anti Money Laundering' ya 2006 irekebishwe ili iweke viwango vya fedha ambazo mtu anaweza kuingia au kutoka nazo nchini bila kuzitaja na Waziri wa Fedha atengeneze kanuni za kutekeleza sheria hiyo.

“Benki Kuu iandae mfumo thabiti wa usimamizi wa Maduka ya Fedha (Foreign Bureau de Change), na kuhakikisha kutungwa kwa sheria inayozuia matumizi ya fedha za kigeni katika shughuli za kibiashara hapa nchini….The Proceeds of Crime Act, 1991” ifanyiwe marekebisho na kuweka kifungu kinachomwezesha AG/DPP kuwa na mamlaka ya kuomba mahakama kufungua kesi ya madai kwa watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi,” ilisema.

“Imesisitizwa kwamba CAG akague misamaha ya kodi na kuweka taarifa hiyo kwenye taarifa za kila mwaka na serikali iimarishe taasisi zinazoshughulikia maadili utawala bora na uwajibikaji kama vile Sekretariati ya Maadili ya Viongozi, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Takukuru, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Tume ya Utumishi wa Mahakama, Kamati ya Maadili ya Bunge ili ziweze kufanya kazi zake kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizoanzisha Taasisi hizo,” ilisema.

Aidha, ilisema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na vyombo vingine vinavyohusiana na kushughulikia masuala ya jinai, wawe waalikwa kwenye vikao vya Kamati za Bunge ili watoe ushauri kwenye kamati hizo.

Akizungumzia hatua ya kutaka Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma irekebishwe, Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uchumi, Andrew Chenge, alisema sababu kubwa ni kuwa Katiba iliyopo sasa inaweka usiri juu ya umiliki wa mali za viongozi wa umma.

Alisema Katiba ya sasa inapaswa ieleze kwa uwazi ili wananchi wafahamu umiliki wa mali za viongozi wao kwa kuwa Katiba ndiyo msingi wa kila kitu katika nchi.

Mbunge wa Chakechake Pemba (CUF), ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Rajab Mbarouk, alisema sababu kubwa ya kuazimia hivyo ni baada ya kubainika kuwapo kwa usiri mkubwa wa baadhi ya viongozi waliojilimbikizia mali  na kuzificha ndani na nje ya nchi.

Alisema kuna habari kwamba viongozi hao wameficha mali zao katika nchi ya Uswisi.

Aliongeza kuwa lengo lingine ni kutaka kuwapo kwa uwazi zaidi kama ulivyo kwa Serikali ya Kenya kwa viongozi wake kuweka mali zao katika mtandao ili wananchi waweze kufahamu.

Alisema Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma imeshindwa kufanya kazi kama Watanzania walivyotarajia.

Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1995, inasema : Orodhesha mali zako na mali unazomiliki kwa pamoja na mke au mume wako na pia mali za watoto wenye umri ulio chini ya miaka 10 na nane ambao hawajaoa au kuolewa.

Mjadala mkali ulizuka bungeni mwaka 1995 wakati sheria hiyo ikitungwa lakini mwisho wa siku ilikataliwa na wabunge wengi kwa madai kwamba itakuwa inaingilia uhuru wa watu.

Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa wakati huo, Andrew Chenge, ndiye aliyekuwa kinara wa kupinga kupitishwa kwa sheria inayotaka mali za viongozi ziwekwe wazi akijenga hoja kwamba sheria hiyo itaingilia uhuru wa viongozi wa umma.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: