ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, August 15, 2013

Wakala wa Kaseja ahukumiwa kifungo


Wakala Ismail Balanga Bandua
Wakala Ismail Balanga Bandua (41) wa Kipa wa zamani wa Simba, Juma Kaseja, amehukumiwa kwenda jela miezi mitatu au kulipa faini ya Sh.150,000 baada ya kukutwa na hatia ya makosa matatu ikiwa ni pamoja na kuingia nchini na kuishi bila kibali.

Mshtakiwa huyo ambaye ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo alihukumiwa adhabu hiyo jana baada ya kukiri makosa matatu yaliyokuwa yakimkabili mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Hellen Riwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Awali, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Patrick Ngayomela ulimsomea mshtakiwa mashtaka yake ambapo ilidaiwa kuwa Agosti 7 mwaka huu, eneo la Magomeni Kondoa jijini Dar es Salaam, mshtakiwa akijua yeye ni raia wa Kongo, alikutwa akiishi nchini kinyume cha sheria.


Ilidaiwa kuwa katika shtaka la pili, siku ya tukio la kwanza, katika mpaka wa kuingia nchini eneo la Tunduma mkoani Mbeya, mshtakiwa aliwadanganya maofisa wa Idara ya Uhamiaji kwamba anaingia nchini kwa nia ya kuwasalimia ndugu zake huku akijua yeye ni wakala wa wachezaji wa mpira wa miguu anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Katika shtaka la tatu, siku ya tukio la kwanza na la pili, mshtakiwa anadaiwa kujihusisha na kukuza vipaji vya soka nchini bila kibali.

Mshtakiwa alikiri mashtaka yote matatu ambapo aliomba mahakama kumpunguzia adhabu kwa sababu anapenda kufanya kazi nchini na kwamba atafuata taratibu zinazotakiwa za kuishi kihalali.

Hakimu Riwa alisema baada ya mshtakiwa kukiri mashtaka yake, mahakama inamtaka alipe faini na akishindwa kufanya hivyo aende gerezani kutumikia kifungo cha miaka mitatu.

Hadi NIPASHE inaondoka katika Mahakama ya Kisutu, mshtakiwa huyo alikuwa bado hajalipa faini na hivyo kuhifadhiwa kwenye mahabusu ya mahakama hiyo.

CHANZO: NIPASHE

No comments: