ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, August 28, 2013

Wakubaliana kuoa mwanamke mmoja

maisha ni Nyumba, imewezekana kwa wakenya wawili kusainiana mkataba wa kuishi na mke mmoja katika ndoa, huu ni mfano wa nyumba tu si nyumba wanayoishi familia hiyo
Nairobi. Wanaume wawili wa Kenya, Sylvester Mwendwa na Elijah Kimani wamekubaliana kumuoa mwanamke mmoja baada ya kubainika kuwa kila mmoja alikuwa na uhusiano naye wa kimapenzi na hakuna aliyekuwa tayari kumwacha.
Wanaume hao wakazi wa Kisimani Kisauni, Mombasa walikubaliana kwa mkataba maalumu wa maandishi juzi, wakisema kwamba wako tayari kushirikiana kinyumba na mwanamke huyo na kumaliza ugomvi baina yao.
Walichukua uamuzi huo baada ya kubaini kwamba kwa pamoja wamekuwa na uhusiano na mwanamke huyo mjane, mama wa pacha kwa zaidi ya miaka minne bila ya kugundua. Walibaini ukweli huo baada ya fumanizi lililozuia ugomvi baina yao.
Hata baada ya mwanamke huyo, Joyce Wambui kuambiwa achague mmoja kati ya wanaume hao ambaye angeishi naye alisema hawezi kuishi bila mmoja kati yao.
Kwa mujibu wa Msimamizi wa Usalama, chini ya Mpango wa Ushirikiano baina ya Polisi na Raia, Abdallah Abdulrahman, Mwendwa na Kimani waliamua kuishi na Wambui baada ya kushindwa kuelewana ni nani kati yao anayestahili kuwa mumewe kwa sababu wote wanampenda naye anawapenda wote wawili.
“Kila mmoja alisema asingeweza kuishi bila mwanamke huyo ambaye ni mjane, ndipo wakaamua kuandikiana mkataba kuhusu namna ya kuishi na mwanamke huyo,” alisema.
Mkataba wa ndoa
Abdulrahman alisema uamuzi huo ulifikiwa ili kusuluhisha mzozo huo. Alisema mkataba waliotia saini unaeleza kuwa mmoja wa wanaume hao atakuwa na wakati wake wa kumtembelea mwanamke huyo.
Mkataba huo pia unasema kuwa wataishi kwa kuheshimiana na hakuna yeyote kati yao atakayechukua zamu ya mwenzake kumtembelea Wambui.
“Nilijaribu kwa kadri ya uwezo wangu kuwapatanisha lakini hakuna aliyetaka kumwachia mwenzake mwanamke huyo. Niliposhindwa niliwaacha nikarudi ofisini,” alisema Abdulrahman.
Alisema alishangaa wanaume hao walipofika ofisini mwake baadaye na kutia saini mkataba ambao walikubaliana kuishi na mwanamke huyo kwa zamu.
Mwendwa alisema Wambui akijifungua mtoto atakuwa wao wote kwa sababu itakuwa vigumu kujua baba yake isipokuwa kama watafanya uchunguzi wa vinasaba, DNA. Alisema wote wawili wanasimamia malipo ya kodi ya nyumba, chakula na matumizi mengine ya Wambui na watoto wake pacha.
Lakini mpango huo umepingwa vikali na wakazi wa eneo hilo wakisema ni kinyume na utamaduni wa Kiafrika na maandiko ya Biblia na Quran.
“Hawa watu wanafaa kushtakiwa kwa kuvunja sheria ya ndoa katika Katiba, huu ni unyama,” alisema mkazi wa Kisauni, Tumaini Juma.
Mwananchi

No comments: