YANGA imefanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya kirafiki dhidi ya timu ya 3Pillars FC ya Nigeria, uliopigwa jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, lakini jambo nzuri ni kwamba, mashabiki walishuhudia mchezo mzuri uliionyeshwa na vijana hao wa Jangwani.
Mbali na mchezo mzuri wa pasi nyingi na kasi ulioonyeshwa na Yanga, pia ilishuhudiwa kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Mrisho Ngassa, akikabidhiwa kitambaa cha unahodha katika kipindi cha pili cha mchezo huo mara baada ya beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kupumzishwa.
Mbali na matukio hayo, tukio lililowashangaza wengi ni jinsi umati wa mashabiki wa Yanga ulivyomvamia Ngassa, ambapo walikuwa wakimshangilia na kutaka kupiga naye picha, hali ambayo ilisababisha usumbufu mkubwa uwanjani hapo hadi askari kuingilia kati mara baada ya mechi hiyo.
Tukio hilo la Ngassa lilitokea kwenye eneo la kuegesha magari la uwanjani hapo, ambapo akiwa anaongozana na mwandishi wa gazeti hili, pamoja na kiungo Haruna Niyonzima na Jerry Tegete, ghafla lilitokea kundi la mashabiki hao ambao walionyesha kuwa na furaha na kufurahia uwezo wa juu aliouonyesha katika mechi hiyo.
Mara baada ya kumfikia mchezaji huyo, mashabiki hao walikuwa wakitaka kupiga naye picha, huku wengine wakitaka kumbeba, ndipo askari wakaingilia ili kuwatawanya, lakini ilikuwa kazi ngumu kwa kuwa mashabiki hao walionekana wazi kama ‘wamepagawa’.
Hali hiyo ilizua mvutano kwa muda lakini baadaye Ngassa alifanikiwa kuingia ndani ya gari lake aina ya Nissan yenye namba za usajili T421 BYT pamoja na Niyonzima na Tegete.
Mara baada ya kuingia ndani ya gari, mashabiki hao walilisukuma kwa hatua kadhaa huku wakiendelea kushangilia, kisha wakaliacha liondoke.
Ngassa amekuwa gumzo kubwa kwenye usajili huu, hasa baada ya jina lake kupelekwa katika orodha ya wachezaji wa timu mbili; Simba na Yanga, kila moja ikidai ina mkataba naye halali.
Katika mechi hiyo ya jana, Yanga ilipata bao lake kupitia kwa Hussein Javu ambaye alipiga shuti kali baada ya kupata pasi kutoka kwa Niyonzima, ambapo shuti hilo liligonga mwamba wa juu kisha kuzama ndani.
Wachezaji wa Yanga walionyesha kuelewana zaidi katika mechi hiyo ambapo kulikuwa na mabadiliko mengi ya wachezaji kila baada ya muda.
STORI: Marth Mboma, Wilbert Moland na Khatimu Naheka
No comments:
Post a Comment